USHIRIKA UTUMIKE KUWAKOMBOA WANANCHI KIUCHUMI- MHE. SILINDE

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde (Mb) ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika pamoja na taasisi nyingine zinazohusika na Ushirika kusimamia vyema uendeshaji wa Vyama vya Ushirika ili viweze kutumika kama nyenzo ya kuimarisha uchumi na kuondoa umasikini.

Akifungua Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani leo Julai 1, 2024 katika Viwanja vya Ipuli Mkoani Tabora amesema Serikali ina azma ya kuhakikisha inasimamia na kuimarisha Vyama vya Ushirika ili viwasaidie Wananchi wengi kiuchumi kupitia Vyama vya Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS), SACCOS na Ushirika wa aina nyingine.

Amesema mifumo ya Ushirika imewezesha bei za mazao mbalimbali kuongezeka, akibainisha mfano bei ya kakao kuongezeka kutoka wastani wa Shilingi 7,000 kwa kilo msimu wa 2022/2023 hadi wastani wa Shilingi 29,000 kwa kilo msimu wa 2023/2024.

Aidha, katika msimu wa 2021/2022 Vyama vya Ushirika vilitumika katika usambazaji wa pembejeo mbalimbali ili kuweza kuwafikia wakulima wake kwa urahisi zaidi, ambapo Jumla ya Shilingi. 1,172,239,240,501 zilitumika kuagiza Pembejeo za aina mbalimbali ikiwemo mbolea ya Ruzuku.

Kwa upande wake Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege amesema Tume itaendelea kusimamia Vyama kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu na kuwataka viongozi wa Ushirika kuendesha Vyama kwa Uadilifu na weledi.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Wadau mbalimbali ikiwemo Vyama vya Ushirika, Taasisi za Fedha, Makampuni ya Bima, TEHAMA, watoa huduma pamoja na Mashirika yasiyo ya Kiserikali.

Maadhimisho hayo yameongozwa kwa Kauli Mbiu isemayo “Ushirika Hujenga Kesho Iliyobora kwa Wote”.

Related Posts