Dar es Salaam. Matukio ya waandamanaji wa Gen Z kuchoma moto mali na ulipuaji wa mabomu ya kutoa machozi yanaendelea kushuhudiwa nchini Kenya.
Manadamano hayo yanayofanywa ikiwa ni muendelezo wa kile walichokianza wiki mbili zilizopita, hoja yao kubwa ikiwa ni kukataa muswada wa fedha kwa mwaka 2024, Rais William Ruto kutangaza kutousaini na kuurudisha bungeni.
Hatua hii ya pili ya maandamano ambayo sasa hufanyika kila wiki, lengo lake ni kukamata maeneo yote dhidi ya utawala wa Rais Ruto, yaani ‘Occupy everywhere protests against President William Ruto’s regime.’
Wakati hayo yakifanyika, Rais Ruto ameshaonyesha nia wiki iliyopita ya kukutana na vijana hao ana kwa ana au kupitia mjadala kwa njia ya mtandao wa X yaani X space (zamani Twitter).
Leo Jumanne Julai 2, 2024 waandamanaji eneo la Mombasa wamechoma moto magari, huku kaunti ya Nyeri waandamanaji wakitembea wakiwa na jeneza.
Kwa upande wa Nairobi, waandamanaji walipambana na polisi na kuwasha moto barabarani, hali ikishuhudiwa tofauti eneo la Waiyaki walikopanga mawe barabarani.
Wakati maandamano hayo yakiendelea, baadhi ya balozi kutoka mataifa mbalimbali nchini Kenya zimewataka wananchi kuchukua tahadhari ya usalama wao.
Ubalozi wa Marekani, Ukraine, Urusi, na Poland zimetoa ushauri kwa raia wao kuepuka maeneo yenye mikusanyiko mikubwa, hasa katika miji inayoonekana kuwa vitovu vya maandamano.
Ubalozi wa Marekani jijini Nairobi, Kenya umetangaza kufuta ratiba ya kazi ya kawaida leo Jumanne na kufunga ofisi zake.
Pia Ubalozi huo umeelezea “masikitiko” kuhusu kuingiliwa kwa ratiba yao ya kawaida kutokana na maandamano yanayotarajiwa kuendelea kwa wiki nzima katika kaunti kadhaa.
“Maandamano japo ni ya Amani, lakini muda wowote yanageuka kuwa vurugu. Maofisa wa usalama wametumia mitungi ya maji, gesi ya kutoa machozi na katika baadhi ya maeneo risasi halisi zimetumika,” imesema taarifa ya Marekani iliyotolewa jana Jumatatu, Julai mosi, 2024.
Imeandaliwa kwa msaada wa tovuti ya Daily Nation.