Kiwango kibovu ilichokionyesha Mamelodi Sundowns msimu uliopita ikiwemo kushindwa kufurukuta mbele ya Yanga katika mechi mbili timu hizo zilipokutana kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika vimepelekea mabosi wa Mamelodi kusitisha mkataba wa kocha wake Rulani Mokwena.
Ikumbukwe Mamelodi ilikutana na Yanga kwa mara ya kwanza Machi 30 mwaka huu uwanja wa Benjamin Mkapa na mechi kumalika kwa suluhu ambapo marudio yalipigwa April 5, nchini Afrika kusini na kumalizika bila bao kisha Mamelodi kusonga mbele kwa ushindi wa mikwaju ya penalti 3-2 huku Yanga ikikataliwa bao lililofungwa na Stephen Aziz Ki.
Mwanaspoti limejiridhisha mapema wiki hii uongozi wa Mamelodi ulikaa kikao na Mokwena kutathimini, mafanikio na alichokifanya msimu mzima uliomalizika na kuamua kusitisha mkataba wake.
Mokwena ambaye wiki mbili zilizopita alikuwa visiwani Zanzibar kwa mapumziko anaondolewa Mamelodi kwa kushindwa kufika malengo licha ya kupewa mahitaji yote aliyotaka.
Kushindwa kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kupoteza ubingwa wa kombe la Shirikisho la nchi hiyo (Nedbank Cup) ikifungwa 2-1 na Orlando Pirates ni miongoni mwa malengo aliyoshindwa kufikia Mokena akiambulia ubingwa wa ligi pekee.
“Ameshindwa kufikia malengo. Ndiyo sababu inayotusukuma kuachana naye. Atatangazwa muda wake ukifika,” alisema moja ya viongozi wa Mamelodi.
Wakati ikisubiriwa kutangazwa kufutwa kazi kwa Mokwena, Mamelodi imetangaza kuachana na wachezaji wake wanne Bongani Zungu, Brian Onyango, Gaston Sirino na Thabiso Kutumela.