Dar es Salaam. Kiongozi mstaafu wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe ameitaka Serikali kufanya uchunguzi huru na wa kina kuhusu vitendo vya utekaji vinavyojitokeza mara kwa mara nchini Tanzania, ili wanaohusika wafikishwe katika vyombo vya sheria.
Amesema vitendo vya utekaji vilishaanza kusahaulika nchini, lakini hivi sasa vimeanza kurejea upya na kuzua hofu kwa Watanzania, hasa katika familia ambazo ndugu zao wanakumbwa na hali hiyo.
Zitto ametoa ushauri huo siku chache tangu kuripotiwa tukio la mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam, Edgar Mwakabela maarufu kama ‘Sativa’ anayedaiwa kutoweka Juni 23, 2024 na kupatikana Juni 27, 2024 katika pori la Hifadhi ya Katavi akiwa na majeraha.
Sativa ambaye amepata majeraha, ikiwemo mpasuko wa taya zilizosagika huku baadhi ya mifupa ikionekana na mipasuko midogo, hivi sasa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.
Zitto ameeleza hayo leo Jumanne Julai 2, 2024 alipozungumza na wanahabari muda mfupi baada ya kwenda kumjulia hali Sativa aliyelazwa Aga Khan.
“Uchunguzi huru ufanyike, ili kukomesha matukio haya yaliyoanza kushamiri katika siku za hivi karibuni. Matukio haya yanaharibu taswira ya nchi yetu, yanaturudisha katika zama ambazo wengine tuliamini tumeshatoka.
“Njia pekee ya kukomesha haya ni kufanyika uchunguzi huru na wa kina, ili hatua stahiki zichukuliwe kwa watu watakaohusika na matukio haya,” amesema Zitto.
Zitto ambaye ni mbunge wa zamani wa Kigoma amewapongeza vijana wa mitandao ya kijamii ambao bila kujali itikadi za kisiasa walipaza sauti kuhusu kupotea kwa Sativa hadi kupatikana na kushiriki kugharamia matibabu yake.
“Ni mshikamano unaopaswa kuwepo hasa kwa vijana kushirikiana katika mambo kama haya, ili yasitokee tena na njia mojawapo ya kukomesha ni uwajibikaji, hatua stahiki kuchukuliwa na uchunguzi wa kina,” amesema Zitto.
Kwa mujibu wa Zitto, baada ya jana Jumatatu kufanya mazungumzo ya kina na Sativa alimtafuta kwa simu Rais Samia Suluhu Hassan, ili kumpa ushauri wa kufanya kwa uchunguzi wa sakata hilo ambalo halileti taswira nzuri katika Taifa.
Katika hatua nyingine, mratibu wa matibabu ya Sativa, Martin Masese maarufu MMM amesema hali ya Sativa inaendelea vema na leo Jumanne atafanyiwa upasuaji wa taya, ili lilirudi katika hali ya kawaida.