Baada ya Korea Kaskazini, Vietnam sasa Putin atua Kazakhstan

Moscow, Urusi. Taarifa ya leo Jumatano, Julai 3, 2024 ya Ikulu ya Urusi inasema Rais wa nchi hiyo, Vladimir Putin amewasili nchini Kazakhstan ambapo atahudhuria mkutano katika mji mkuu wa Astana.

Shirika la Ushirikiano la Shanghai (SCO) lenye wanachama tisa, linajumuisha sehemu yake ya wanachama kutoka Moscow hadi Beijing, China huku ikitajwa kujumuisha karibu nusu ya idadi ya watu duniani.

Wanachama wake wa kudumu ni mwenyeji wa mwaka huu ambaye ni Kazakhstan, India, China, Kyrgyzstan, Pakistan, Russia, Tajikistan, Uzbekistan na Iran.

AFP imesema mwaka huu Belarus inatarajiwa kujiunga baada ya kuambiwa katika mkutano wa kilele wa SCO wa 2023, kwamba nchi hiyo itakuwa mwanachama.

“Mnamo Julai 3 hadi 4, viongozi wa nchi wanachama wa SCO watajadili hali na matarajio ya kuimarisha zaidi ushirikiano baina yao na kuboresha shughuli zake,” Ikulu ya Kremlin imesema na kuongeza Putin atakutana na viongozi wenzake katika mkutano huo.

Putin anafanya ziara hiyo ikiwa zimepita wiki chache tangu alipofanya ziara za kiserikali katika nchi za Korea Kaskazini, na Juni 20 akaenda nchini Vietnam kuendelea na ziara hiyo.

Awali, Putin alipokuwa Korea alitia saini mkataba wa ushirikiano wa kimkakati na Pyongyang. Katika Safari hiyo ya kihistoria ilitajwa kama ya kirafiki ya kitaifa wakati ambao nchi hizo zikiwa ni mojawapo ya nchi zilizowekewa vikwazo duniani.

Aidha, baada ya Korea Kaskazini Putin alienda Vietnam ambapo alikutana na Rais wa nchi hiyo To Lam katika mji wa Hanoi.

Related Posts