Babu azitega halmashauri, atoa mwezi mmoja kukusanya mikopo

Siha. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ametoa siku 30 kwa halmashauri za mkoa huo kufuatilia na kurejesha mikopo ya asilimia 10 iliyotolewa kwa vikundi na halmashauri hizo na hazijarejeshwe.

Hayo ameyasema leo Jumatano Julai 3, 2024 katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani lililojadili hoja za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Siha na kuhudhuriwa na viongozi wa dini, madiwani, na wakuu wa idara.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa Babu ametoa mwezi mmoja kwa wadaiwa wote kurejesha fedha hizo ili na wengine waweze kukopeshwa.

“Sasa natoa agizo na wala siyo ombi. Kote nilikopita nimetoa mwezi mmoja kuhakikisha fedha zote zinakusanywa. Hawa waliokopeshwa mnawajua, wengine wanatoka kwenye kata zenu, kwa nini hawarejeshi mikopo,” amehoji Babu.

Amesema kama wangechukua fedha benki, isingewaruhusu wachezee fedha hizo. “Sasa hivi wangeshauza nyumba, magari, wangeuza kila kitu kufidia mkopo wao.”

Hivyo amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri na wenyeviti wa halmashauri kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja fedha zote ziwe zimekusanywa.

Amesema mikopo iliyotolewa ni kati ya Sh15 milioni kwa baadhi ya halmashauri na nyingine zimetoa mikopo yenye thamani ya Sh83 milioni 83 (Bil zuzitaja majina) akiziagiza kuwa lazima fedha hizo zikusanywe.

Amesema Siha ipo kwenye kundi la wilaya 10 zinazokwenda kupatiwa fedha kwa ajili ya mikopo hiyo ambayo sasa itatolewa kupitia benki.

“Sasa hawa wakopaji hawatatuchezea tena, fedha watakazokopa zitalipiwa benki, kama ilivyo mikopo ya mabenki na wakichelewesha mkopo, kazi wanayo,” amesema Babu.

Wakati huohuo, mkuu huyo wa mkoa amewaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri mkoani humo kuhakikisha shule za msingi na sekondari mkoani humo zinapatiwa hati miliki za maeneo yao mara moja.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Dancani Urasa amesema maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa Babu watayafanyia kazi ili halmashauri iweze kusonga mbele na kuwaletea wananchi wake maendeleo.

“Haya ni maagizo, lazima tuyatekeleze, kama alivyosema lengo ni kutaka kuona wananchi wanapata maendeleo,” amesema Urasa.

Related Posts