Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema kuna umuhimu mkubwa kwa jamii, wakiwamo vijana, wazazi, wanafunzi na Serikali kwa ujumla, kusimamia maadili ya Kitanzania.
Amesema ni bora mtu uitwe mshamba, lakini asimamie misingi na tabia zote njema zinazotambulika katika jamii na kuachana na maadili yasiyofaa.
Biteko ameyasema hayo leo Julai 3, 2024 wakati akizindua kitabu cha ‘Mmomonyoko wa maadili nani alaumiwe’ kilichotungwa na Mufti wa Tanzania, Abubakar Zubeir katika Msikiti wa Mohammed wa Sita uliopo Kinondoni, Jijini Dar es Salaam.
“Niwakumbushe Watanzania wenzangu, Taifa letu lazima lishiriki katika makuzi na maadili ya watoto kwa kutenga muda wa kuona watoto wetu wanaishije.
“Niwaambie, taifa lolote ambalo halina utamaduni unaojivunia na linakumbatia utamaduni wa wenzake, taifa hilo limekufa,” amesema.
Aidha, ametoa wito kwa wazazi kukuza uhusiano na watoto wao, huku taasisi za dini, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Maendeleo ya jamii kwa pamoja zikishikamana kudumisha kizazi chenye maadili mema.
Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Abubakar Zubeir amesema maadili yameharibika ndio maana akavutwa kuandika kitabu hicho kwa lengo la kuyarejesha.
“Taifa likiwa na watu wenye maadili mazuri ndilo lililo taifa jema, likiwa na watu wasio na maadili basi limeangamia, hivyo kila lenye kuwezekana lifanyike kwa umoja, ili kuwa na jamii bora,” amesema Mufti Zuberi.
Amesema kitabu hicho kitasaidia watu wajue wapi wanaenda na wanapokosea wajirekebishe.
Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu, Dk Doroth Gwajima amesema maendeleo ya Tehama yana madhara na kama viongozi na walezi, lazima wapande mbegu nzuri, ikiwamo ya hofu ya Mungu.
“Serikali kwa kushirkiana na wadau wake tulizindua kampeni ya kuelimisha jamii kuhusu usalama wa watoto na matumizi ya mitandao ya kijamii kwa kuwa na malezi chanya, ” amesema.
Waziri huyo amesema kitabu hicho kimeongeza rejea inayofanywa na Serikali ya kupambana na mmomonyoko wa maadili na watakuwa bega kwa bega kukiweka katika programu zao.
Waziri Gwajima amesema ili kufanikisha hilo, wizara itanunua vitabu hivyo vya thamani ya Sh7 milioni.
Akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule amesema; “Lazima tukubaliane kuna tatizo kwenye jamii, kuna mmomonyoko wa maadili, ikiwemo vipigo kwa watoto, kinamama, dawa za kulevya na mambo mengine yasiyofaa.”
Amesema yote hayo yanatokea, lakini Tanzania haijakaa kimya na Serikali imekuwa ikisisitiza wananchi watende mambo mema.
Amesema Tanzania itakuwa nchi ya ajabu endapo itayaachia mmomonyoko wa maadili uendelee kukua siku hadi siku.
Ali Ngeruko, Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Taifa amesema leo ni siku ya kihistoria kama Watanzania, kwa kuwa ni sehemu ya kutafuta mwarobaini wa mmomonyoko wa maadili.
Ngeruko ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya kitabu hicho amesema: “Kuna rushwa ya ngono, biashara ya ngono, tunasikia ulawiti, mapenzi ya jinsia moja, rushwa katika chaguzi na mengi machafu, ikiwemo ukatili kwa watoto wachanga wenye ualbino.
“Tusiishie kusikia katika vyombo na kutazama, ndio maana Mufti kaandaa jukwaa hili, ili jamii iyatafakari haya yote,” amesema Ngeruko.
Amesema wazazi wanapaswa wakae na watoto wao na familia zao kwa ujumla watafakari mmomonyoko wa maadili uliopo, kwa kutazama hata mavazi ya watoto wao hususani wa kike.
“Baba mzazi mtoto wako wa kike amevaa mavazi yaliyo nje na maadili halafu unamtazama, sasa wakati umefika wa kukemea maovu na kufundisha mema, ili jamii yetu itoke hapa ilipo iende kuwa bora na nzuri,” amesema.
Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa dini kuwa mpango huo usiwe wa Mufti pekee, bali kwa kila kiongozi katika jamii pamoja na viongozi wa dini kuwasikiliza waumini wao matatizo yanayowakabili na kuwashauri.
Mmoja ya wahudhuriaji wa uzinduzi huo, Nasra Jamal amesema umefika wakati wa kujadili tabia chafu katika jamii, kwani yanayoendelea kwa sasa yanaogopesha.
“Natamani kila mzazi nyumbani asisitize kila liwezekanalo, ikiwemo kuwafuatilia kila wafanyalo, ili watoto wakue katika tabia njema,” amesema.