FANYENI KAZI USIKU NA MCHANA JENGO LA TAMISEMI LIKAMILIKE – MHA. MATIVILA 

OR-TAMISEMI

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Miundombinu Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhandisi Rogatius Mativila amemuelekeza mkandarasi anayejenga Jengo la Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mtumba kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kwa haraka.

Mhandisi Mativila ameyasema hayo wakati wa ziara yake katika Jengo hilo ambalo linajengwa kwenye Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma leo Julai 3, 2024 ambalo hadi kukamilika kwake litagharimu Sh.Bilioni 20.2.

Amesema Jengo hilo lilianza kujengwa Oktoba 2021 na muda wa ujenzi ulikuwa miezi 24 hivyo lilitakiwa kukamilika Oktoba 2023 lakini Mkandarasi aliomba muda wa nyongeza mpaka Juni 29, 2024 lakini hadi sasa jengo limefikia asilimia 76.

“Ninaziona dalili kabisa za wewe kuomba tena muda wa nyongeza inamaana utakuwa umejenga jengo hili kwa muda wa miaka tatu, sasa kwa muda utakaoomba tena wa nyongeza tutakupa kwa gharama na hatutegemei ichukue muda mrefu tena tunataka mwezi wa kumi mwaka huu tuhamie hapa kwenye jengo hili,”amesema.

Akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa Jengo hilo, Kaimu Meneja Mradi kutoka Vikosi vya Ujenzi, Mhandisi Deogratius Japhet amesema sehemu kubwa ya ujenzi wa jengo hilo umeshakamilika kwa kazi za ndani pamoja na nje kazi kubwa iliyobakia ni kwenye umaliziaji tu hivyo wanategemea kwa muda watakaopewa wa nyongeza wataweza kukamilisha kwa asilimia 100.

Amesema jengo hilo la Gorofa sita litakuwa na uwezo wa kuchukua wafanyakazi 600.

Naye, Mhandisi Mshauri kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Arch. Weija ng’olo
amesema jengo hilo litakuwa na ubora wa hali ya juu na thamani ya fedha itaonekana kwa kuwa wameshauri ipasavyo,kukagua pamoja na kupima kila malighafi na vifaa vilivyoletwa kwa ajili ya ujenzi wa Jengo hilo.

Related Posts