UKIONDOA umaarufu na hadhi yake katika soka la Afrika, kocha mkuu wa Al Hilal ya Sudan, Florent Ibenge ni miongoni mwa wanadamu wapole wenye ukarimu pale unapokutana nao.
Timu ya Mwanaspoti ilibahatika kufanya naye mahojiano kwenye moja ya hoteli jijini Dar es Salaam, ambako mbali ya kuikaribisha kwa bashasha na furaha, alikuwa mtulivu na mnyenyekevu ndani ya saa moja ya mahojiano.
Katika mahojiano hayo, Ibenge alimzungumzia nyota mpya aliyesajiliwa na Yanga kutoka Simba, Clatous Chama na kilichomkwamisha kufanya vizuri Morocco, huku akitia neno kwa kiungo wa wana Jangwani hao, Stephane Aziz Ki akisema ni miongoni mwa mastaa anaowakubali sana na kufichua maisha ya Sudan yalivyo.
Baada ya kiungo Clatous Chama kufanya vizuri msimu wa 2020/21 akiichezea Simba, uongozi wa RS Berkane ukavutiwa na kiwango chake ukamsajili msimu wa 2021/2022 ambao alidumu kwa miezi sita kisha akarejea tena kwa wana Msimbazi.
Ukimuuliza Chama alifeli wapi, Ibenge ambaye ndiye aliyemsajili Mwamba wa Lusaka pale Berkane, atakujibu: “Chama ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa, ana ujuzi, kipaji kikubwa, hakuna kocha ambaye anaweza asitamani kuwa naye kwenye kikosi chake.
“Kitu kilichomrudisha Tanzania ni suala la familia yake, ikumbukwe alipoteza mkewe, aliacha watoto wake Zambia, hivyo alihitaji ukaribu na watoto wake.
“Naheshimu sana familia nilimuelewa alivyosema anahitaji kukaa karibu na watoto wake, kama watoto hawana mama watahitaji kumuona baba yao.”
Kuhusu Tripple C kwenda Yanga, Ibenge anasema: “Kama nilivyosema, Chama ni mchezaji mzuri na kwenda kwake Yanga itakuwa faida kubwa kwa timu hiyo.”
Ibenge alizungumza kuhusu kiungo mshambuliaji Aziz Ki, ambaye amemaliza mkataba wake na Yanga mwezi uliopita, kama anavutuwa naye na angependa kumsajili katika kikosi cha timu yake ya Al Hilal.
“Niliwahi kumhitaji wakati anachezea ASEC Memosas, lakini alichagua kwenda Yanga, kiukweli ni mchezaji mzuri na sidhani kama kuna kocha asiyemtamani, ukiwa naye ni jambo zuri katika timu.”
Baada ya Simba kuachana na aliyekuwa kocha mkuu Mualgeria, Abdelhak Benchikha, kulikuwa na tetesi za Ibenge kuhusishwa na kikosi hicho cha Msimbazi, pia kuna kipindi aliwahi kutajwa kwenda Yanga, analifafanua hilo.
“Siwezi kusema timu mojamoja, imewahi kutokea kuzungumza na viongozi wa timu za hapa Tanzania, sio ajabu kwani nimefundisha maeneo mengi Afrika, hiyo ni kazi yangu, nimesema Tanzania ni sehemu nzuri na mpira unazidi kukua, hivyo kama itatokea siku nikaja hapa sioni kama ni jambo baya, bosi wa Al Hilal ni rafiki wa Mwenyekiti wa Simba na huwa wanazungumza kwahiyo hata kutakiwa na timu hiyo mimi hajawahi kuniambia,” anasema.
Ibenge pia amezungumzia kuvutiwa na mwenendo wa Simba na Yanga kimataifa, akisema: “Simba na Yanga kwa sasa zina hatua kubwa sana katika michuano ya CAF, naamini kadri muda unavyokwenda zitafanya makubwa na kutimiza malengo yao.”
Akaipongeza pia Yanga kwa kufika fainali ya Kombe la Shirikisho la Afrika msimu wa 2022-2023 huku akiweka wazi ni moja ya mafanikio mazuri ambayo yanaonyesha jinsi soka la Tanzania linavyopiga hatua kubwa kila uchao.
“Msimu huu pia zimefanya vizuri kwa sababu zimeishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, pia niipongeze Azam FC kwa kumaliza nafasi ya pili msimu uliopita, kwa hakika wamefanya kazi kubwa kwa sababu haikuwa rahisi kushindana na timu za Simba, Yanga.”
Miezi kadhaa iliyopita kulikuwa na taarifa za Al Hilal inaweza kuja Tanzania kucheza Ligi Kuu Bara, Mwanaspoti lilimuuliza Ibenge kuhusu hilo akajibu: “Kwangu lilikuwa ni jambo zuri na ninashukuru mamlaka za soka Tanzania kwa kuonyesha nia ya kukubali ombi letu hapo awali, lakini sasa mambo yamebadilika, Mauritania ilitupa ofa ya kucheza katika Ligi yao kama timu ya kawaida tofauti na ilivyokuwa hapa ambapo tulipewa nafasi japo ilikuwa ni kama kucheza mechi za kirafiki tu.”
Kwa uzoefu wake, anasema amegundua tabia za wachezaji wa Afrika, wanapenda zaidi muziki na kudansi, jambo analoliona linawasaidia kuzifanya akili zao ziwe na utulivu mkubwa, kabla na baada ya majukumu yao uwanjani.
“Asilimia kubwa wengi wao nawaona wakisikiliza muziki na kucheza, hilo ni jambo nzuri kupata muda wa kufurahia maisha yao, mchezaji hatakiwi kuwa na msongo wa mawazo, muziki unawasaidia kuwaweka sawa,” anasema.
Kuna wanamuziki wa hapa Tanzania anaowafahamu, wengine wakiwa ni kutokana na kolabo walizozifanya, ni Ali Kiba, Diamond Platnumz, Harmonize na Zuchu.
“Kuna wanamuziki ambao wamefanya kolabo na wasanii kutoka Congo, huwa naziona nyimbo zao, nyingine zinapigwa na wachezaji wa timu hii ya Al Hilal na wanacheza,” anasema Ibenge.
Kutokana na uzoefu wake wa kuzifundisha timu mbalimbali barani Afrika, jambo la msingi analoliona na linalopaswa kufanyiwa kazi kwa bidii ni michakato ya kuibua vipaji na kuvijengea misingi mizuri kuanzia chini, itakayokuwa mwongozo kwao kufika mbali.
“Afrika kuna vipaji vikubwa, lakini jambo la msingi na muhimu ni kuanza kuwatengeneza watoto kuanzia chini wakiwa na misingi sahihi, katika soka hakuna siri wala njia za mkato, kila kitu ni lazima kizingatiwe.”
Mbali na kusisitiza misingi ianzie chini kwa wachezaji, alitoa rai kwa wazazi kuwapa sapoti vijana wao katika vipaji wanavyoamini vinaweza vikabadilisha maisha yao.
“Wazazi wawe mstari wa mbele kuzifanikisha ndoto za watoto wao, mfano kuna shule za soka, muziki, ufundi, ili wapate elimu na kukuza vipaji vyao wawapelekee katika fani zao,” anasema.
Kiwango walichokionyesha kwa nyakati tofauti wachezaji Watanzania, wanaocheza nje, Mbwana Samatta, Simon Msuva, Abdi Banda, Thomas Ulimwengu, anasema kimetoa picha ya vipaji vilivyopo Tanzania.
“Samatta na Ulimwengu wana heshima kubwa sana TP Mazembe, walifanya makubwa wakati wanacheza hapo, hivyo siwezi kusema wamefeli, kwani kuna wakati wanaweza wakakumbana na nyakati tofauti.
Anaongeza: “Mfano Msuva alionyesha kiwango kikubwa sana wakati anaichezea Difaa El Jadida (2017-2020) na Wydad Casablanca (2020/2021), kitu kilichomtoa mchezoni ilikuwa ni kudai maslahi yake, hivyo huwezi kusema alikuwa mbaya, kuna Banda kacheza kwa kiwango kikubwa sana Afrika Kusini ni beki ninayemkubali sana.
“Wengine ambao hawachezi nje ila wana uwezo mkubwa ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyetoka Yanga na sasa Azam FC na mzaliwa wa Zanzibar, Waziri Junior anayecheza KMC… wapo wengi siwezi kumtaja mmoja baada ya mwingine,” anasema.
Wakati kiungo, Fabrice Ngoma anajiunga na Simba, alitokea Al-Hilal ya Sudan ambayo anafundisha Ibenge, jambo ambalo kocha huyo, limemfanya amchambue.
“Aliniambia kocha nimepata ofa ya kwenda Simba, nilimruhusu kwa moyo mkunjufu, kwenye maisha yangu siwezi kuthubutu kuzuia riziki ya mtu, wanafanya kazi kwa ajili ya familia zao na kipato ndio jambo ambalo kila mmoja wetu anajitafuta.
“Sio Ngoma peke yake, wapo wengi hata kama nilikuwa nawategemea kwenye kikosi cha kwanza, endapo wakipata sehemu watacheza na watapata pesa nawaambia waende kwa sababu hayo ni maisha, mwisho wa siku wasije wakajuta huko mbele.”
Ibenge pia anamzungumzia nyota wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele ambaye kwa sasa anacheza Pyramids ya Misri akisema Mkongomani mwenzake huyo ana sifa zote za kuitwa mshambuliaji.
“Kwa mara ya kwanza nilipomuona katika timu ya AS Simba Kamikaze (2019) ya Congo alikuwa anafunga sana, akaja AS Vita Club akawa anafunga, akaenda Yanga akafanya hivyo hivyo, namfuatilia pia huko Misri bado anaendeleza moto ule ule, timu ya taifa pia anafunga, hilo linathibitisha habahatishi kile anachokifanya,” anasema.
Mbali na kufundisha soka na umaarufu mkubwa alioupata katika kazi hiyo, Ibenge ana shahada ya uchumi, “Wakati nacheza soka, baba yangu alikuwa ananikataza, lakini nilikuwa nafeli kama sichezi na nikicheza nafaulu, hivyo aliniacha nifanye vyote, kwani yeye ni msomi na amesomea udaktari hivyo aliamini katika elimu.”
Ibenge anasema Tanzania ni nchi ya amani kwani tangu waweke kambi katika hoteli iliyopo Dar es Salaam anatembea bila shida na anafurahia kuona vitu mbalimbali. “Natembea huko nje kwa amani na bila ulinzi tofauti na Sudan ambako huwezi kutembea hovyo hovyo,” anasema.
Anasema katika kikosi cha timu anazofundisha, huwa anaangalia wachezaji ambao wanajituma na wanaoweza kuleta matokeo mazuri uwanjani na sio majina au sura za watu ambavyo haviwezi kusaidia kufikia malengo ya klabu.
“Ndani ya kikosi cha timu ninayofundisha, mchezaji akiwa na jina kubwa lakini hana anachokionyesha uwanjani, sioni kama anakuwa na sababu ya kuwepo kikosini, kupata nafasi, akiwa na jina kubwa awe na uwezo mkubwa,”
Anaongeza, “ingawa ni jambo zuri kuwa na wachezaji wenye majina makubwa, ila yaendane na kazi uwanjani.”
Mwanaspoti lilimuuliza kuhusu hali ya kiusalama ya Sudan na kutokana na machafuko yanayoendelea mara kwa mara na kusababisha ligi ya nchini humo kutochezwa na baadhi ya timu kuamua kutafuta mataifa mengine kwa ajili ya kuchezea.
“Nimeshuhudia nyakati ngumu zaidi za maisha nikiwa Sudan. Nilipotezana na mwanangu siku nane. Wakati vita inaanza alikuwa hotelini na bomu lilipigwa hapo. Nilipata nafasi ya kuongea naye baadaye akiwa katika uwanja wa ndege ambapo pia bomu lilipigwa, kiukweli hali ni mbaya na imekuwa hivyo kwa muda mrefu, wakati naondoka nchini humo nilikuwa napishana na miili ya watu waliofariki njiani.”
“Hali hii pia ipo hata kwa wachezaji nilionao, nafikiria ningekuwa mimi ndio nacheza kwa kweli ningeshaacha zamani, lakini jambo la kuwapongeza wameweza kuyashinda magumu yote na kuendelea kuitumikia timu, wana wakati mgumu sana kuna muda hawawezi kabisa kuwasiliana na familia zao kwa sababu kuna muda intaneti huwa inakata.”
Wachezaji wengi wa Kitanzania wamekuwa na wakati mgumu Uarabuni, baadhi wameishia kucheza msimu mmoja na kurudi nchini, miongoni mwao ni Shaban Idd Chilunda, Yahya Zayd na Nickson Kibabage, Ibenge anaeleza sababu.
“Unajua ni tofauti na wachezaji wa Congo, Watanzania wengi wameanza kwenda huko katika miaka ya hivi karibuni lakini mbali ya baadhi kufeli, Simon Msuva alifanya vizuri na nafikiri aliondoka kwa sababu ya matatizo ya pesa na timu aliyokuwa anaichezea, lakini kwa Wacongo wamekuwa wakipata mafanikio kwa sababu tumeanza kucheza kule kwa muda mrefu.”
Kuhusu burudani, Ibenge ambaye pia mwishoni wa mahojiano haya alikuwa akiimba wimbo unaobamba wa msanii Dimond Plutnumz na Khalil Harrison uitwayo, Komasava, anasema: “Nawafahamu wasanii wengi wa hapa Tanzania, miongoni mwao ni kama Zuchu, Diamond, Alikiba, Harmonize.”
Ibenge anasema aliwahi kuhusika kumshawishi beki wa kulia wa Manchester United, Aaron Wan-Bissaka aje kuitumikia timu ya taifa la DR Congo.
Bissaka ambaye ana uraia wa England na DR Congo hadi sasa bado hajacheza timu ya wakubwa ya taifa lolote kati ya hayo mawili na inaelezwa kwamba nia yake ni kuitumikia England.
Ibenge alianza kuifundisha DR Congo kwa mara ya kwanza mwaka 2008 hadi 2009 kama kocha msaidizi na alihudumu pia kuanzia mwaka 2014 hadi 2019 kama kocha mkuu.
“Ndio nimewahi kuzungumza na mchezaji na familia yake pia husususani baba yake, lakini unajua lazima pande mbili zote zifikie makubaliano, yeye hawezi kuamua tu bila ya wazazi wake. Kwa muda ule alikuwa bado ana umri mdogo na hatukufikia makubaliano ya kuja kucheza Congo, unajua wachezaji wengi wa kimataifa huchukua muda kukubali kucheza mataifa haya ya Afrika, muda mwingine unaongea na wachezaji na familia zao miaka 10 kabla,” anasema Ibenge (62).
“Nafikiri hadi sasa kuna mazungumzo yanaendelea ili kumshawishi aje kucheza timu ya taifa ya DR Congo.”
Bissaka aliwahi kucheza timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ya Congo mwaka 2015, kisha akahamia kuichezea England katika timu zao za vijana chini ya miaka 20 na 21 mwaka 2018, tangu hapo hakuwahi kulichezea taifa hilo linaloshiriki Euro na DR Congo imekuwa ikimshawishi awatumikie.
Staa huyu alizaliwa London, lakini wazazi wake wote wanatokea DR Congo na walihamia England mwaka 1997.
Baada ya kucheza katika timu za vijana za Crystal Palace, Bissaka alipandishwa timu ya wakubwa mwaka 2018 ambapo alicheza kwa mwaka mmoja tu kabla ya kutua Man United kwa ada ya Euro 55 milioni.