BINGWA wa zamani wa Kick Boxing wa Dunia, aliwahi pia kutamba kwenye Ngumi za Kulipwa nchini, Japhet Kaseba sambamba na Karim Mandonga ni miongoni mwa mabondi watakaozipiga katika mapambano maalumu ya hisani ya kusaidia jamii kupata Bima ya Afya.
Mabondia hao na wengine watapambana mapambano hayo ya ngumi yatakayofanyika mwishoni mwa mwezi huu yakiandaliwa na kampuni ya Lady in Red Promotion ikishirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afrika (NHIF) na Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi(Tasaf).
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam promota wa mapambano hayo ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu, Sofia Mwakagenda alisema lengo la ngumi hizo ni kusaidia watu masikini kupitia bima ya afya.
Sofia alisema wameamua kuja na pambano ili kurejesha kwa jamii na kuhamasisha mapromota wengine kufanya jambo kwa ajili ya watu wanaopitia changamoto mbalimbali.
“Msaada huo utaambatana na burudani ya ngumi Julai, 28 mwaka huu na pambano hilo litafanyika mikoa minne, tumeanza na Geita itafuata Pwani, Dodoma na Mbeya,” alisema mbunge huyo aliyeongeza kuwa, lengo la kupeleka pambano hilo mikoani na sio Dar es Salaam ni kutokana na mahitaji ya watu wa mikoani ambao ndio changamoto kubwa zinawapata.
Mkongwe wa ngumi nchini, Japhet Kaseba ni miongoni mwa mabondia watakaotoa burudani, na alisema kila kitu kipo sawa kilichobaki ni kumjua tu mpinzani.
“Hili jambo lilinigusa na niliposikia lengo ni kusaidia jamii nikaona niwajibike, nilimuomba dada yangu Mwakagenda naomba nisapoti, na nipo tayari kushirikiana nae ili kufanikisha mchakato huo,” alisema promota huyo.
Ukiachana na Kaseba mabondia wengine wanaotarajiwa kupanda ulingoni ni Ibra Class ‘Ibra Mawe’, Mada Maugo, Issa Mollel na Tatiana.