Dar es Salaam. Shahidi wa nne katika kesi ya ukahaba inayowakabili washtakiwa watano katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive, ameikera mahakama kwa majibu ya ‘sijui’ kwa maswali aliyoulizwa na mawakili wa utetezi.
Shahidi huyo ambaye ni polisi wa kike (WP) Konstebo Masadi Madenge kutoka Kituo cha Polisi Magomeni Usalama ametoa majibu hayo jana Julai 2, 2024 alipohojiwa na mawakili wa utetezi maswali ya dodoso kuhusu ushahidi alioutoa mahakamani.
Licha ya kuwa maswali mengi alijibu hajui, hata kwa mambo aliyazungumzia katika ushahidi, mahakama iliendelea kurekodi kama alivyojibu.
Hata hivyo, jibu la kwamba hajui alikokuwa akiishi kabla ya kuajiriwa na Jeshi la Polisi lilimkera Hakimu Mkazi Mfawidhi Lugano Kasebele anayesikiliza kesi hiyo, ambaye alimuonya, akimwamuru kujibu swali hilo kama inavyotakiwa.
Hakimu Kasebele amewahoji waendesha mashtaka iwapo walitimiza wajibu wao, akisema hawezi kuvumilia kuendelea na kesi katika hali kama hiyo. Amesema ikiendelea atachukua hatua zaidi.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 17277/2024, washtakiwa wanakabiliwa na shtaka moja la kufanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa ajili ya kufanya ukahaba kinyume cha kifungu cha 176 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 na marejeo ya mwaka 2022.
Washtakiwa ni Mariam Yusufu Mkinde (25) mkazi wa Magomeni, Mwazani Nassoro (25) mkazi wa Kigogo, Mwanaidi Salum (25) mkazi wa Mabibo, Faudhia Hassan (35) mkazi wa Ubungo, na Tatu Omary (40) mkazi wa Ubungo.
Wanadaiwa Juni 17, eneo la Manzese Tiptop wilayani Ubungo, Dar es Salaam, walikutwa wakifanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa kusimama hadharani, wakiwa wamevaa mavazi yasiyo ya heshima kwa lengo la kufanya ukahaba.
Washtakiwa wanatetewa na jopo la mawakili Peter Madeleka, Jebra Kambole na Maria Mushi.
Akiongozwa na waendesha mashtaka, mawakili wa Serikali, Winfrida Ouko na Cuthbert Mbilinyi shahidi ameieleza mahakama yeye ni miongoni mwa askari polisi waliowakamata washtakiwa kwa tuhuma za kufanya ukahaba.
Ameieleza mahakama Juni 17, 2024, miongoni mwa majukumu aliyoyafanya ni kukamata ‘madada poa’ (makahaba) sita, eneo la Manzese Midizini, saa 9.00 usiku, akishirikiana na askari wenzake waliokuwa doria.
Amedai walikuwa wamevaa mavazi ya nusu uchi, yakionyesha maumbile yao kama vile matiti, tumbo na mapaja.
Shahidi alishindwa kujibu swali la mwendesha mashtaka kuhusu hatua za awali za ukamataji mtuhumiwa, kwamba huwa wanafanya nini.
Licha ya kuulizwa swali hilo mara kadhaa na mwendesha mashtaka na hata kufafanuliwa na hakimu, shahidi alikaa kimya mpaka mwendesha mashtaka alipoamua kuachana na swali hilo.
Akiendelea na ushahidi amedai baada ya kuwakamata watuhumiwa (washtakiwa) waliwahoji kwa tuhuma za kujiuza, akidai walijibu kazi hiyo ndiyo inawafanya wanalipa kodi, wanasomesha watoto, kununua mavazi, chakula na malazi. Amedai waliwapeleka Kituo cha Polisi Mburahati.
Alipotakiwa kueleza maana ya kujiuza shahidi amesema: “Kujiuza ni kitendo ambacho mwanamke au mwanaume hujirahisisha mwili wake.”
Maswali ya dodoso na majibu yaliyoikera mahakama.
Wakili Kambole: Shahidi umesema umeajiriwa Jeshi la Polisi, miezi miwili kabla ya kuajiriwa ulikuwa wapi?
Wakili: Kabla ya kuajiriwa ulikuwa unaishi wapi?
Hakimu: Seriously? (kweli) Yaani wewe kila kitu hujui? No (hapana) hatuwezi kuendelea namna hii. Wakili kwani huwa hamuongozani huko?
Naweza kufunga na kutoa uamuzi, siwezi kuendelea namna hii. Kwani wewe ulikuwa huishi? Hebu jibu maswali, ulikuwa unaishi wapi kabla ya kuajiriwa?
Wakili: Mlipowakamata na kuwapeleka Polisi ambako umesema mliwaandikisha, mliwaandikisha kwa kosa gani?
Shahidi: Kujihusisha na vitendo vya umalaya?
Wakili: Umesema ni nani alijihusisha na nani kwa umalaya?
Wakili: Ni kweli wewe hukuwahi kushuhudia hivyo vitendo vya umalaya?
Shahidi: Siku hiyo Juni 17, 2024
Wakili: Nani alikuwa anafanya na nani?
Wakili: Wakati wanafanya hivyo vitendo vya umalaya wewe ulishuhudia ukiwa wapi?
Shahidi: Nilikuwa siko mbali sana na mahali walikokuwa.
Wakili: Ndiyo nakuuliza ulishuhudia nani na nani wakifanya hivyo vitendo vya umalaya?
Wakili: Shahidi ni sahihi kwamba wewe hujui hawa waliokamatwa hiyo miili kama waliuza walimuuzia nani?
Wakili: Wala kwamba waliuza kwa watu wangapi? Kwa hayo ambayo hujui ni sahihi kwamba hujui hawa waliowakamata ni malaya au si malaya?
Wakili Madeleka: Shahidi, umesema kwenye msafara (doria) ulikuwa na Assistant Inspector – Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Peter lakini alikuja hapa shahidi akasema anaitwa Inspekta Peter sasa kati ya huyu Inspekta Peter na huyo Mkaguzi Msaidizi Peter unayemtaja kuwa ulikuwa naye wewe ni yupi?
Shahidi: Assistant Inspector Peter.
Wakili: Kwa hiyo huyu Inspekta Peter na A/Inspekta Peter ni tofauti?
Wakili: Unafahamu A/Inspekta huwa ana nyota ngapi?
Wakili: Lakini unajua kuwa jeshini kuna askari wa nyota moja na wa nyota mbili?
Wakili: Hebu ieleze mahakama alama za huyo A/Inspekta Peter zilikuwa ni zipi?
Wakili: Sasa ulijuaje kuwa huyu ni A/Inspekta Peter?
Shahidi: Alivaa cheo chake.
Wakili: Hicho cheo kina alama gani?
Shahidi: Alikuwa amevaa nyota
Wakili: Ni nyota ngapi alikuwa amevaa?
Wakili: Ulisema mliwahoji hao washtakiwa, unakubaliana na mimi mahojiano kati ya mtuhumiwa na Polisi yanapaswa kuwa kwenye maandishi ni sawa?
Hakimu: Kwa hiyo hayapaswi kuwa kwenye maandishi?
Shahidi: Yanakuwa kwenye maandishi.
Wakili: Kwenye mahojiano hayo umesema wengine walisema hii kazi ya kujiuza wanayoifanya inawasaidia kulipa kodi, malazi, makazi na kupelekwa watoto shule, sasa mwambie mheshimiwa kwa kuwa umesema mahojiano hayo yanakuwa kwenye maandishi kama umeleta hayo maandishi hapa mahakamani?
Shahidi: Sijui, sijayaleta
Wakili: Umesema uliwakamata madada poa, madada poa maana yake ni nini?
Wakili: Hiyo tafsiri ya dada poa ni malaya umeitoa wapi?
Wakili: Ni kwa mujibu wa sheria au unavyofahamu wewe?
Shahidi: Ninavyofahamu mimi.
Shahidi: Ni kitendo ambacho mwanamke au mwanamke anauza mwili wake kwa njia ya kingono
Wakili: Uliiambia mahakama walikuwa wanawauzia nani?
Wakili: Ni sehemu gani za mwili ambazo huwa zinauzwa?
Wakili: Umesema hawa washtakiwa walikuwa wanauza mwili, hiyo miili walikuwa wanauza kwa bei gani?
Wakili: Waliokuwa wananunua hiyo miili wako wapi?
Wakili: Unataka kumaanisha wanunuzi walikuzidi mbio?
Wakili Maria: Shahidi, utakubaliana na mimi kwamba hakuna sheria inayomzuia mwanamke kusimama pembeni mwa barabara usiku?
Wakili: Ni kweli leo hujaleta ushahidi wa mavazi ambayo mliwakamata nayo?
Wakili: Kwa kuwa hujatuletea ushahidi huo ni sahihi kwamba inawezekana walikuwa wamevaa hayo mavazi ya nusu uchi au hawakuwa wamevaa?
Baadhi ya maswali ya ufafanuzi ya waendesha mashtaka
Wakili Ouko: Umeulizwa kama ushahidi wa mavazi umeletwa mahakamani na ukasema haujaletwa hebu ieleze mahakama ni kwa nini?
Shahidi: Mavazi hayakuletwa kwa sababu walikuwa wamevaa hayohayo hatukuweza kuwavua.
Wakili: Umeulizwa walikuwa wanauza viungo gani ukasema hujui hebu fafanua na uvitaje viungo usiogope
Awali shahidi wa tatu, Juma Ramadhani, Mkazi wa Manzese Midizini, ambaye ni dereva wa pikipiki za abiria maarufu bodaboda ameieleza mahakama alishuhudia washtakiwa wakikamatwa na askari polisi.
Amesema katika kazi yake huwa anakesha kwa kuwa mahali hapo kuna klabu.
“Hiyo klabu ambayo awali ilikuwa Tiptop Bar, ndiyo inafuga madada poa wote wanaovaa mavazi hayo, sisi tuko pale tunavumilia tu kwa kuwa ni wateja wetu lakini ni kero sana,” amedai Juma.
Amedai Juni 17, 2024 kati ya saa 9.27 na saa 9.30 usiku lilifika gari la polisi likiwa na askari wa kike, ambao waliwakamata wanawake sita wanaozurura waliokuwa wamevaa nguo zinazoonyesha maumbile yao, wakaondoka nao.
Nguo hizo amedai ni vitopu ambavyo viliacha matiti nje, tumbo na vitovu, pia walivaa ‘vikaptura’ vyepesi vya kubana na vifupi vilivyoacha mapaja wazi.
“Hao madada huwa wanazurura, yakipita magari wanasimamisha wanasema baby baby yaani ni kama wao ndio wanawatongoza wanaume wanaoingia nao kwenye magari wanaondoka nao baada ya dakika 10 au 20 wanarudi tena,” amedai shahidi.
Juma amedai, “Wanachozungumza na wenye magari sijui, wala wanachokwenda kufanya huko.”
Sehemu ya maswali ya dodoso
Wakili Madeleka: Shahidi, kwenye hiyo gari ya Polisi askari walikuwa wangapi?
Wakili: Hukuhesabu askari kwa sababu ulijikita kwenye kazi yako ya bodaboda ni sahihi?
Wakili: Lakini umesema dada poa waliokamatwa ni sita, kwa hiyo ni sahihi kwamba wewe kazi yako ni bodaboda na kuhesabu dada poa ni wangapi?
Shahidi: Siyo sahihi, mimi nafanya kazi yangu tu.
Wakili: Watu wanakwenda klabu wamevaa suti?
Shahidi: Wanaoingia ndani ni watu wenye heshima zao.
Wakili: Nani alikwambia hawa madada hawana heshima?
Shahidi: Nguo zao walizovaa hazina maadili.
Wakili: Hizo nguo ambazo hazina maadili wewe umeziona hapa mahakamani?
Wakili: Kuna Sheria inayozuia mwanamke kusimamisha gari usiku?
Wakili: Sasa wewe ulijua kwamba hawa wanaosimamisha magari huwa wanafanya kosa?
Shahidi: Si huwa nawaona kwa macho yangu, wanachofanya ni kosa maana huwa wanagombania gari moja wanawake watatu halafu mmoja anaambiwa panda wewe.
Wakili: Ni Sheria gani inayosema ni kosa wanawake kufanya hivyo?
Wakili: Mimi sijasoma sheria lakini huwa wanafanya biashara gani usiku?
Wakili: Kwani wewe huwa unafanya biashara gani pale?
Shahidi: Mimi nafanya biashara ya bodaboda yangu.
Wakili: Kama na wenyewe wanafanya biashara yao?
Wakili: Ya kuuza simu kwani wewe bodaboda yako umeileta hapa? Kwani mtu akifanya biashara mpaka ajitangaze?
Wakili Kambole: Shahidi, umesema hawa washtakiwa walikamatwa kwa sababu walikuwa wanazurura, ulieleza walikuwa wanazurura kutoka wapi kwenda wapi?
Wakili: Hebu ieleze mahakama kuzurura maana yake nini?
Shahidi: Unatoka kwako unakuja sehemu ambako huna kitu cha kufanya kwa hiyo kutoka kutembea huna kitu cha kufanya unazurura.
Wakili: Hiyo maana yako ya kuzurura ni kwa mujibu wa nini?
Shahidi: Hicho mimi sifahamu
Wakili: Kwa hiyo, hiyo tafsiri umeitoa wapi?
Shahidi: Ni kwa mujibu wa ubongo wangu.
Wakili: Kwa hiyo unataka mahakamani hapa watu waadhibiwe kwa sababu ya ufahamu wa ubongo wako?
Wakili: Ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni sheria gani ambayo inaongoza uvaaji wa mavazi?
Shahidi: Sikusoma sheria.
Wakili: Unadhani ni sahihi mtu kuadhibiwa kwa jambo ambalo haliko kwenye sheria?
Shahidi: Mimi hapo sielewi
Shahidi: Sijui hiyo sheria ya adhabu
Wakili: Kuita baby ni kosa?
Wakili: Baby maana yake nini?
Shahidi: Sijui, ina maana nyingi anaweza kuwa mtoto au mpenzi.
Wakili: Kwa hiyo inawezekana huyo aliyeitwa baby ni mpenzi wake?
Shahidi: Sielewi kama walikuwa wanamuita mpenzi wake au mumewe au mtoto.
Wakili: Hawa watu walikamatwa hujui kama walikuwa wanaingia klabu au walikuwa wanatoka?
Wakili Maria: Shahidi, uliwahi kujua wale waliokuwa wanaitwa baby kwenye magari walikuwa na mahusianao gani?
Maswali ya mawakili wa Serikali kwa ufafanuzi
Wakili Ouko: Umeulizwa kama ulitaja namba za gari la polisi, ukajibu kuwa hujataja, hebu ieleze Mahakama.
Shahidi: Gari likija hakuna mtu anakuwa na mawazo ya kuziangalia namba za gari.
Wakili: Uliulizwa kama huwa unawahesabu madada poa ukasema huwa hufanyi hivyo hebu ielezee Mahakama.
Shahidi: Mimi huwa sifanyi hivyo, huwa naangalia kazi yangu ya bodaboda na siku gari lilipokuja ndiyo nikaona wanakamatwa.
Kesi hiyo inaendelea leo Julai 3, 2024.