Kesi za mauaji kuendelea kuunguruma Geita leo

Geita. Wakati Mahakama Kuu Masijala ndogo ya Geita ikiendelea na kikao cha pili cha kesi za mauji hapa Mjini Geita leo, tayari kesi mbalimbali zimesikilizwa na kutolewa hukumu ikiwemo ya Anold Shemasi aliyedaiwa kumuua mtoto wake mchanga kwa kutofanana nae.

 Mahakama hiyo ilimehukumu kunyongwa hadi kufa Shemas, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumuua kwa kukusudia mtoto wake Anna Shemas  mwenye umri wa mwezi mmoja kutokana na mtoto huyo kutofanana nae.

Kikao hicho cha pili cha Mahakama Kuu kilianza Juni 18, 2024 na kwa wiki mbili mfululizo Mahakama hiyo ilisikiliza kesi ya washtakiwa watano wanaodaiwa kumuua kwa kumpiga na kitu chenye ncha kali, Milembe Suleman (43) aliyeuawa Aprili 26, 2023.

Katika kesi hiyo ambayo iko chini ya Jaji Mfawidhi, Kevin Mhina, mshtakiwa mmoja aliachiwa huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha makosa yake huku washtakiwa wanne wakisubiri hukumu inayotarajiwa kutolewa Julai 19, 2024.

Washtakiwa katika kesi hiyo namba 39/2023 ni Dayfath Maunga, Safari Lubingo, Genja Pastory na Musa Pastory waliokutw na kesi ya kujibu baada ya ushahidi wa watu 29 na vielelezo 19 kutolewa mahakamani hapo na upande wa mashtaka huku washtakiwa hao wakijitetea wenyewe.

Mahakama hiyo pia imemuachia huru Stephano Mlenda (31) Mkazi wa Chigunga, Wilaya ya Geita aliyekuwa akishtakiwa kwa kosa la kumuua mtoto wake mwenye umri wa miaka 9 kwa kutokukusudia baada ya kumchapa kwa fimbo alipoiba Sh700 na kwenda kununua soda.

Kesi hiyo namba 12,387 ya mwaka 2024 ilikuja mahakamani hapo kwa ajili ya upande wa mashtaka kuleta mashahidi na kabla ya ushahidi kuanza kutolewa mshtakiwa alikiri kutenda kosa la kuua bila kukusudia.

Akitoa hukumu hiyo Jaji Mhina ameeleza kilichotokea siku hiyo ilikua lengo la mzazi kumuadhibu au kumuonya mtoto kwa kuwa aliiba pesa na siyo kuua.

Katika kikao hicho pia kesi iliyokuwa ikiwakabili washtakiwa wanne walioshtakiwa kumuua Alphonce Mawazo aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita waliachiwa huru baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi hiyo.

Juni 18, 2024 kesi hiyo ilianza kusikilizwa upya baada ya Mahakama ya Rufani  iliyoketi Mwanza mbele ya Majaji watatu, Ferdinand Wambali, Issa Maigena Leila Mgonya kutengua hukumu ya kesi hiyo na kuamuru ianze kusikilizwa upya, baada ya kubaini kasoro za kisheria  katika mwenendo wa kesi hiyo Mahakama Kuu.

Mahakama hiyo pia imemuachia huru Mshtakiwa Bahati Shija aliyekuwa akikabiliwa na shitaka la kumuua mkewe Grace Daud kwa kukusudia kwa kumpiga na chuma kichwani baada ya mkewe huyo kukataa kurudiana.

Mshtakiwa huyo aliachiwa huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kama kweli yeye ndiye aliyemuua.

Leo Mahakama Kuu Masijala ndogo ya Geita chini ya Jaji Graffin Mwakapeje, inaendelea na kesi ya Zephania Ndalawa anayeshtakiwa kwa kosa la kumuua Thomas Masumbuko kwa kumnyonga kinyume na kifunge cha 196 na 197 cha Kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Endelea kufuatilia mitandao ya Mwananchi kwa habari zaidi.

Related Posts