Kidata na nyota ya uteuzi wa marais watatu

Dar es Salaam. Hii ndiyo safari ya milima na mabonde ya uongozi wa Alphayo Kidata mmoja wa viongozi wa ngazi juu anayehamishwa hamishwa kupelekwa ofisi muhimu za Serikali kuhudumu kwa nyakati tofauti.

Jina la Kidata lilianza kuchomoza zaidi mwaka 2013 alipoteuliwa na aliyekuwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Kabla ya kuishika wadhifa huo, Kidata alikuwa Naibu Katibu Mkuu (Ofisi ya Waziri Mkuu -Tamisemi) wakati huo.

Machi 2016, Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli alimteua Kidata kuwa Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na baadaye kumthibitisha kuwa Kamishna Mkuu.

Uteuzi wa Kidata kuongoza TRA ulitokana na mshikemshike ulioibuka katika mamlaka hiyo baada ya Novemba 27, 2015, Rais Magufuli kumsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade.

Bade alisimamishwa kazi baada ya kuibuliwa kwa upotevu wa makontena 249 yenye thamani ya Sh80 bilioni katika Bandari ya Dar es Salaam pasipo TRA kuwa na kumbukumbu zozote.

Hata hivyo, mwaka 2017 Hayati Magufuli alimuondoa Kidata TRA na kumteua kuwa Katibu Mkuu Ikulu, akichukua nafasi ya Peter Ilomo aliyestaafu.

Wakati nafasi ya Kidata TRA ilichukuliwa na Charles Kichere ambaye kwa sasa ni Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kidata alihudumu ukatibu mkuu Ikulu hadi hadi Januari 10, 2018 alipoteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada, nafasi alioitumikia kwa miezi 10.

Mwishoni mwa 2018, Hayati Magufuli alimrejesha nchini na kumvua hadhi ya ubalozi.

Septemba 20, 2019 Hayati Magufuli alimteua kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, nafasi aliohudumu hadi mwaka 2021.

Aprili 4, 2021 Rais Samia alimrejesha Kidata TRA na kuhudumu nafasi hiyo hadi jana Jumanne Jumanne Julai 2, 2024 alipomteua kuwa Mshauri wa Rais Ikulu.

Nafasi ya Kidata imechukuliwa na Yusuf Mwenda ambaye ni Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA).

Kidata ni miongoni mwa watumishi wa umma ambaye amebahatika kuteuliwa mara kadhaa na maraia watatu tofauti akianza na Jakaya Kikwete, John Magufuli na sasa Samia.

Akizungumzia safari ya Kidata, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Aviti Mushi amesema mtendaji huyo bado mtumishi wa umma anayepaswa kufanya kazi popote anatumwa na bosi wake kwa maslahi ya umma.

“Hata alivyoteuliwa kuwa balozi au katibu tawala ilikuwa sehemu ya kutimiza majukumu ya utumishi wa umma, pale unapoonekana unahitajika unaitwa. Kwa sababu Kidata anajua maana utumishi nini ndiyo maana akiitwa anaitikia wito ili kutimiza majukumu.

“Ni safari ya kawaida ya mtumishi wa umma yeyote yule anapohitajika anaitwa, ikitokea ametolewa kuna sababu zilizopo kulingana na mwenye mamlaka ya kumteua,” amesema Dk Mushi.

Dk Mushi amesema ukiwa mtumishi wa umma, lazima ukubaliane na kila jambo, akisema kuna mahali unaonekana unafaa kwa muda fulani kisha unaondolewa na kupelekwa eneo jingine kulingana na matarajio ya aliyekuwa kuteua.

“Ukiwa na nafasi haimaanisha ni yako milele bali unakuwa nayo kwa muda, ikionekana kuna mwingine anaweza kufanya zaidi yako unaondolewa na kupangiwa majukumu mengine,” amesema Dk Mushi.

Related Posts