Lema ataka kauli ya Rais matukio ya utekaji

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema Rais Samia Suluhu Hassan hakutakiwa kutoa mchango wa kugharamia matibabu ya mtu anayedaiwa kutekwa bali aagize vyombo vyake vya ulinzi na usalama kuwakamata watekaji na waliotekwa wapatikane.

Lema amesema Rais kwa nafasi yake ya Amiri Jeshi Mkuu anapaswa kuhakikisha anasimamia usalama, ulinzi na ustawi wa jamii ikiwa ni pamoja na kukomesha vitendo vya utekaji vinavyoanza kuota mizizi nchini.

Julai 2, 2024 Rais Samia alikuwa miongoni mwa waliojitokeza kuchangia matibabu ya Edgar Mwakalebela maarufu Sativa ambaye alitoweka Juni 23,2024 jijini Dar es Salaam na kupatikana Juni 27 katika Hifadhi ya Katavi akiwa na majeraha.

Kupotea kwake kuliibua mijadala katika mitandao ya kijamii na alipopatikana kampeni ya kumchangia fedha za matibabu ziliendeshwa na watu mbalimbali wakiwemo makada wa Chadema. Rais Samia amechangia Sh35 milioni.

Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika leo Jumatano, Julai 3, 2024 Korogwe mkoani Tanga, Lema amesema Rais hakuwa na sababu ya kutoa mchango wa matibabu.

“Utekaji umeanza, kiongozi wetu wa chama Handeni ametekwa, gazeti la Mwananchi jana limetoa picha nyingi za watu waliotekwa. Rais nimeona umetoa mchango kwa kijana aliyetekwa na kuvunjwa taya, mchango wako sio wa muhimu wewe ni Amiri Jeshi Mkuu wa nchi, unasimamia usalama, ulinzi na ustawi wa jamii.

“Tunataka kauli yako kwa IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi) kwamba watekaji wote wawe kwenye mikono ya polisi ndani ya saa 12 na waliotekwa wote wapatikane. Tunataka wewe kama Amiri Jeshi Mkuu uzuie utekaji na watekaji wakamatwe mara moja la sivyo masuala ya utekaji yana mkono wa Serikali yako.”

Kauli hii ya Lema imekuja ikiwa ni saa chache kuputa baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amesema suala la uhalifu wa utekaji halipaswi kukaliwa kimya.

Amesema uhalifu huo kwa sasa umekuwa gumzo na unahusianishwa na siasa kwamba kuna baadhi ya wanasiasa wanaufanyia siasa uhalifu huo.

Mbali na hilo, Masauni amesema kibaya zaidi uhalifu huo unahusishwa na vyombo vilivyopewa dhamana ya kulinda watu kwa maana Jeshi la Polisi au Serikali.

“Uhalifu huu nahusishwa na wanasiasa na Serikali na kuna gazeti moja la Mwananchi limeandika suala hili pia kuna maswali ni mengi ya nani mtekaji nihakikishe tu Tanzania iko salama,” amesema.

Waziri huyo amebainisha jukumu la Serikali ni kuhakikisha usalama wa wananchi wake na amewatoa hofu wananchi kwamba hali ya usalama hapa nchini iko salama.

“Usalama wa jamii maaana yake tunapambana na aina zote za uhalifu na hata suala la mmonyoko wa maadili hatuwezi kutenganisha na uhalifu,” amesema Masauni.

Kwa mujibu wa waziri huyo katika kipindi cha miezi sita kuanzia Januari hadi Juni 2024 yameripotiwa matukio nane ya utekaji.

Akiyataja matukio hayo amesema la kwanza lilikuwa Juni 24, 2024 Dar es Salaam ambapo mtuhumiwa aliteka msichana na kumbaka kwamba mtuhumiwa ameshapatikana.

“Jingine lilitokea Katavi linahusiana na migogoro ya ardhi watuhumiwa wanne wako kesi yao iko mahakamani, Juni 17, huko Muleba Kagera kuna mtoto alitekwa ana ulemavu wa ualbino alitekwa akapatikana amekufa hivi sasa watuhumiwa tisa pamoja na vidhibiti wamekamatwa na kesi ipo mahakamani,” amesema.

“Juni 24 mkoani Geita kuna mtoto alitekwa na walipigiwa simu wazee wake ili ilipwe fedha mtoto na mtuhumiwa wamepatikana. Pia Februari 12, huko Handeni pamoja na Mei 15, Mbeya kesi za kuteka nyara ili kujipatia kipato watuhumiwa wote wamepatikana,” amesema.

Aidha Mei 29, mkoani Geita lilitokea tukio la utekaji ambalo watuhumiwa wanaendelea kusakwa na uchunguzi unaendelea.

“Mwisho hapa juzi kuna mtu alisemekana ametekwa na kwa sasa yuko Aga Khan hospitali kwa sasa Serikali inaendelea na uchunguzi,” amesema Hamad Masauni.

Waziri huyo amesema Serikali inachukua hatua na hao waliopatikana kwa uthibitisho na inaendelea kuwasaka ambao hawajapatikana vyombo vinaendelea kuwatafuta kwakuwa vina uwezo wa kuwakamata.

Related Posts