Lembeli: Operesheni Tokomeza ilinipa presha, iking’oa mawaziri wanne wa JK

Moja ya operesheni za Serikali zilizofanyika nchini na kugubikwa na mauaji ya watu, dhuluma na ukatili kwa wananchi ni Operesheni Tokomeza, iliyolenga kukabiliana na ujangili kwenye hifadhi za Taifa uliokuwa umekithiri wakati huo.

Operesheni hiyo ilianza Oktoba 2023 hadi Novemba 2014, baada ya Serikali kusitisha kutokana na malalamiko ya wananchi kuhusu vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vilivyotekelezwa na askari wa wanyamapori.

Operesheni Tokomeza ilibuniwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kupambana na ujangili, japo baadaye ililalamikiwa na baadhi ya wabunge na Mei Mosi, 2014, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete aliunda Tume kuchunguza jambo hilo.

Tume iliongozwa na Balozi Jaji (Mstaafu) Hamisi Msumi (Mwenyekiti wa Tume), Jaji (Mstaafu) Stephen Ntashima Ihema (Kamishna), Jaji (Mstaafu) Vincent Lyimo (Kamishna) na Frederick Manyanda (Katibu wa Tume).

Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na mbunge wa zamani wa Kahama (CCM), James Lembeli ambaye wakati wa operesheni hiyo, alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.

Kamati yake ilifanya kazi kubwa katika kufuatilia jambo hilo hadi dakika ya mwisho walipowasilisha ripoti yao bungeni, Aprili 2015, siku ambayo anasema alipata mshituko uliomsababishia ugonjwa wa presha.

Katika mahojiano hayo, Lembeli anasema hakuwahi kuugua ugonjwa huo, hadi siku alipotakiwa kusoma taarifa ya kamati bungeni na kuhitimisha kujibu hoja za wabunge kuhusu walichobaini kwenye operesheni hiyo.

“Wakati nakwenda kusoma ile taarifa, vikao vya CCM vilikuwa vimetoka kufanyika na walinisema na kunitukana sana,” anasimulia mbunge huyo wa zamani wa CCM.

Anasema akiwa bungeni Dodoma, akijiandaa kusoma taarifa ya operesheni hiyo ili ahitimshe kwa kujibu hoja za wabunge, ndipo akaletewa ki-memo (ujumbe kwenye kikaratasi) ambacho kilimpa wakati mgumu.

“Nakumbuka siku hiyo kabla sijaenda kuhitimisha kujibu hoja za wabunge, Spika (Anna Makinda) akaniambia Mheshimiwa Lembeli, subiri kidogo, nikaletewa ki-memo (ujumbe kwenye kikaratasi) ambacho kilisema ‘Mheshimiwa Rais ametengua uteuzi wa wafuatao’,” anasema Lembeli.

“Nusura nidondoke, ilikuwa ni meseji ambayo ilitoka kwa Rais Kikwete kuwatumbua mawaziri watatu, nilipata shock, japo nilijikaza lakini hali yangu ilikuwa mbaya na hata summary yangu nilianza kwa kushukuru na kusema pamoja na hoja zote za wabunge nasisitiza kwamba majibu ya hoja zao yapo kwenye taarifa yetu.”

Anasema memo hiyo ilionyesha waliotenguliwa ni mawaziri watatu ambao ni Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Mathayo David Mathayo (Mifugo na Uvuvi) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii) ambaye alijiuzulu.

Anasema anaamini wakati ule Serikali ilikubaliana na ile taarifa yao kwani kama isingekubaliana nayo, isingetengua uteuzi wa mawaziri wale.

“Niliogopa kilichotokea, usiku uleule saa 8, niliondoka Dodoma, bahati mbaya watoto wangu walikuwa pale Dodoma, nikasema kama lolote linakwenda kutokea bora nikafie mbele, nikaenda mbali kijijini bila kumuaga yeyote,” anasema.

Lembeli anasema operesheni hiyo ilianzishwa kwa nia njema ya kukabiliana na ujangili, baadaye iligeuzwa kuwa mateso, hasa kwa wafugaji na katikati yake uliingizwa mchezo mbaya uliowaathiri wananchi.

“Wengi walidhulumiwa, hasa wafugaji, waliteswa, walinyang’anywa mali zao kwa sababu watu waliingilia kati na kuharibu process (mchakato), wakati ule Waziri wa Maliasili na Utalii alikuwa Kagasheki, lakini kumbe hakushirikishwa kwenye hatua zote zile,” anasema Lembeli.

Anasema hata wale waliobainika kushiriki kwenye kashfa ile hawakuwajibishwa, na wakati wanakusanya taarifa za Operesheni Tokomeza, walikwenda Bukombe na kufanya kikao na wafugaji ambacho anadai kilikuwa kigumu.

“Hadi saa 9 usiku ndipo walikubali kusema ukweli, aliyeanza kutupatia taarifa (mfugaji) aliniambia, Lembeli, mimi sio kama nina ng’ombe 20, hapana, ninazo 600, hata yule (akimuonyesha mzee mwingine) anazo zaidi ya 2,000.

“Walifunguka vitu vingi, wakatueleza kwamba kila baada ya miezi mitatu wanalipa Sh6 milioni ambazo zinaingia mifukoni mwa watu, walitueleza namna ambavyo wengine wameuawa, kuna wengine ng’ombe zao zilikamatwa na kupigwa mnada na wao walizuiwa kwenda kwenye huo mnada, ajabu wote waliohusika, hakuna aliyefukuzwa wala kuwajibishwa,” anasema.

Lembeli anasema kuna mzee aliwahi kuwa mbunge wa Meatu, katika operesheni ile, alikamatwa, akateswa na kuanzia pale aliugua hadi mauti.

“Wakati tunafuatilia operesheni hii, tulikwenda Katavi, kuna diwani sijui alifanywa nini, tulimkuta ameoza makalio, nilimuuliza imekuwaje? Naye akasema hajui kilichotokea, alijikuta tu yuko vile, watu wengi walipoteza maisha nyakati zile.

“Yupo mwingine alikamatwa amebeba swala, akaulizwa wewe hiyo nini? Akasema kamboga tu haka, wakamchukua na swala wake, alining’inizwa miguu juu kichwa chini, baada ya saa kadhaa alishushwa tayari ameshakuwa chengu (amepoteza utimamu), tulipokuwa tunamhoji alisema mambo ambayo siwezi kuyaongea, lakini kwenye ripoti yetu yalikuwemo,” anasimulia Lembeli.

Julai 2015, muda mfupi baada ya Bunge kuvunjwa, Lembeli alihamia Chadema akiungana na viongozi wengine waliotoka CCM na kutimkia kwenye chama hicho cha upinzani.

Moja ya matukio yaliyogonga vichwa vya habari, ni baadhi ya wafuasi kumbeba kama mfalme katika mapokezi yake Chadema kule Kahama, tukio ambalo anasema hakulipenda na lilimtoa machozi.

“Nililazimishwa kubebwa, sikulipenda tukio lile, nakumbuka ilikuwa ni mapokezi yangu baada ya kuhama CCM na kujiunga na Chadema.”

Anasema alipoondoka CCM aliwaambia ni kwa sababu gani, hivyo tukio la kubebwa lilikuwa ni sapoti ya watu wa Kahama ambao alifanya nao kazi kwa miaka 10 kadiri alivyoweza.

“Nilitokwa na machozi, kwani sikuwahi kuona umati mkubwa kama ule, labda wakati wa Mwalimu Nyerere, tukio lile lilikuwa sapraizi kwangu,” anasema.

Mzazi wake alivyomrudisha CCM

Alipohamia upinzani, licha ya kuchukua muda kujadiliana na familia yake, Lembeli anasema mama yake (Maria) hakufurahishwa na uamuzi huo.

Anasema kuna wakati ulifika mama yake alimwambia kama ataendelea na msimamo huo, basi asubiri hadi afariki kwanza, kauli ambayo Lembeli anasema ilimuumiza.

“Baba yangu alikuwa mtemi, ni miongoni mwa walioshawishiwa na Mwalimu Julius Nyerere kuachia madaraka kwa ajili ya uhuru (wa Tanganyika mwaka 1961), hadi anakufa alikuwa ni mwanaCCM.

“Kilichomuumiza mama baada ya mimi kuhama, figisu ziliendelea, kule kwetu hadi leo watu wanaamini nyumba za watemi ni mahali patakatifu, hivyo walikuwa wanakuja kutambika,” anaeleza mwanasiasa huyo.

Anasema alipohama CCM ni kama watu wa kule waliwekewa kauzibe, ilifikia hatua hata kwenda pale kwao kufanya matambiko wakaacha.

“Mama aliniita akaniambia baba yako hakuacha hali hii, umefanya mji wetu, wananchi waususe wakati hapa ndipo lilikuwa kimbilio. Aliniambia nisubiri afe kwanza kama nataka kuendelea na ubabe wangu. Ile kauli iliniumiza, mama yangu ana zaidi ya miaka 90, kauli yake haikuwa nzuri, ilinilazimu kubadili msimamo na kurudi CCM,” anasema.

Julai 2016, Lembeli alirudi CCM na moja ya kauli yake wakati akirejea kwenye chama hicho, alisema: “Mimi sijakatika mkia” na alikaribishwa na Rais John Magufuli na hadi sasa ni kada wa chama hicho tawala.

Ingawa hana uhakika kama chama chake kitampa fursa tena ya kupeperusha bendera kwenye uchaguzi ujao, bado yupo kwenye siasa, anaendelea kufuatilia akijipanga kurudi upya kwenye uchaguzi mkuu wa 2025.

“Iko hivi, ukishaingia kwenye siasa si rahisi kutoka wala kuacha, hata mimi pamoja na kuwa nje ya ubunge tangu mwaka 2015, sijaacha siasa, bado nipo nipo, nafuatilia kwa karibu kila kinachoendelea Tanzania.

“Si kama nilipotoka kwenye ubunge niliacha, hapana, kuna kesho ikitokea yenye nuru narudi, hata suruali huwezi kuivaa ileile miaka 20, ukiibadilisha hata mwonekana wako utakuwa ni tofauti, kwani haiwezekani kuwa na watu walewale wamezoea kufanya mambo yaleyale, lazima tubadilike,” anasema Lembeli.

Hata hivyo, anasema ni wapi atagombea, kama ni jimbo lake la Kahama au kwingineko, hilo halimsumbui, ni suala la muda ukifika na upepo utakavyokuwa, atajitosa.

“Siwezi kusema sitorudi kwenye ubunge, japo dunia imechafuka lakini ukitaka kuingia baharini, cheki mawimbi kwanza, bado umri unaniruhusu, mvi sio ugonjwa, hizi zangu ni maua tu na hekima na itoshe kusema hadi leo hii naamini hakuna wa kunishinda Kahama, japo milango ya kugombea naiona kama imeshazibwa CCM.

“Nahisi jina langu watalikata, labda utokee muujiza na ninasema hivyo nikiwa na mifano hai, kuna maeneo kule kanda ya ziwa, mtu aliyepata kura 12 ndiye anachukuliwa na aliyepata kura 150 anaachwa, leo tujiulize Masele yuko wapi?

“Napenda kuendelea kuwa raia mwema ili pale ambapo naweza kutoa ushauri nitoe, lakini haya ya kugombeagombea, leo siwezi kusema sana, naomba Mungu anisaidie, wakati ukifika nitajitosa, kikubwa ni kuwa na uchaguzi wa amani kuanzia wa serikali za mitaa na hata ule wa 2025. Serikali isikilize vilio vya wananchi na yasitokee matatizo ambayo yataharibu umoja wetu,” anasema.

Mwaka 2015, Lembeli alijitosa kutetea ubunge jimbo la Kahama, jimbo aliloliongoza kwa vipindi viwili vya mwaka 2005 – 2010 na 2010 – 2015 kwa tiketi ya CCM, lakini wakati huo alikuwa mgombea wa upinzani (Chadema) kwa mara ya kwanza.

Anasema uchaguzi ule ulikuwa huru, japo kwa upande wake Kahama anaona yalifanyika mambo yasiyo kawaida. “Sababu natambua sikushindwa ndiyo sababu hadi leo nina amani kuishi Kahama, natembea muda wowote, siogopi na kwa kuwa nilifahamu kilichofanyika, nilisamehe,” anasema Lembeli.

Mwaka huo, Lembeli alishindwa uchaguzi dhidi ya mgombea wa CCM, Jumanne Kishimba aliyeshinda ubunge katika jimbo hilo. Lembeli alishika nafasi ya kwa kupata kura 54, akimfuatia Benjamini Ngaiwa aliyepata kura 181 na Kishimba aliyepata kura 234.

Baadaye, Lembeli alifungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga kuomba kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa mbunge wa jimbo la Kahama Mjini kwa madai kwamba taratibu zilikiukwa.

Hata hivyo, hakushinda kesi hiyo baada ya Jaji wa Mahakama hiyo, Moses Mzuna kueleza ushahidi uliotolewa na upande wa Lembeli haukuwa na nguvu za kutosha kuishawishi Mahakama hiyo kutengua matokeo ya uchaguzi.

Julai 2020, Lembeli alijitosa tena, safari hii akiwa CCM na kushindwa kwenye kura za maoni dhidi ya Kishimba, aliyekuwa akitetea kiti chake, hivyo akakosa fursa ya kugombea ubunge katika jimbo hilo kwa mara nyingine.

Lembeli anasema malalamiko ya wengi kuhusu uchaguzi wa wakati huo ni ya kweli, anaamini haukuwa uchaguzi, bali mchakato wa kupitishana.

“Sijui 2025 itakuwaje, lakini hadi hapa tulipofika nauona mwelekeo mzuri kama Rais Samia Suluhu Hassan atasimamia kile anachokisimamia sasa, japo CCM kuna baadhi ya watu hawapo tayari kubadilika. Natamani uchaguzi uwe huru, watu waruhusiwe kuchagua wanayemtaka, siyo walazimishwe mtu ambaye chama kinamtaka,” anasema.

Mwanasiasa huyo anasema uchaguzi huo utakuwa mgumu pia kwa wabunge wengi waliopo sasa, akisisitiza “wale wanaojijua hawakupita kwa ridhaa ya wananchi, 2025 ndiyo itakuwa bye bye (kwaheri), naona kabisa wengi mle bungeni itakuwa ni bye bye.

Related Posts