KLABU ya Dodoma Jiji imekamilisha uhamisho wa aliyekuwa mshambuliaji wa Mashujaa, Reliants Lusajo kwa mkataba wa mwaka mmoja huku kukiwa na kipengele cha kuongeza mwingine baada ya kuvutiwa na uwezo aliouonyesha msimu uliopita.
Nyota huyo aliyeanza msimu na Namungo kisha Januari akajiunga na Mashujaa kwa miezi sita, amejiunga na kikosi hicho baada ya kuvutiwa na uwezo wake kufuatia kufunga jumla ya mabao manane ya Ligi Kuu Bara akiwa na timu zote mbili.
Taarifa kutoka ndani ya Dodoma Jiji zililiambia Mwanaspoti kwamba baada ya Mashujaa kushindwa kuketi naye mezani kuhusu kumpa mkataba mpya, mabosi wa Dodoma Jiji wakaingilia kati dili hilo na kilichobaki ni kumtangaza.
“Ni kweli Lusajo tumepata saini yake na tunaendelea na uhamisho wa nyota wengine na tutakapokamilisha tutaweka wazi kwa wote tutakaowasajili na kuwaacha, ni mchezaji mzuri ambaye amependekezwa na benchi la ufundi,” alisema kiongozi mmoja.
Ofisa Habari wa Dodoma Jiji, Patrick Semindu alisema, ni mapema sana kuweka wazi kwa sasa kwa sababu kuna taratibu hawajazikamilisha, hivyo kila kitu kitakapokamilika watatangaza rasmi ingawa mashabiki watarajie mambo mazuri.
“Kuhusu usajili huu ni wakati wake na siwezi kuzungumza kwa sababu yapo mambo mengine ambayo viongozi hawajayakamilisha hivyo yatakapokuwa sawa tutawatangazia mashabiki zetu, kikubwa wajue tumesajili wachezaji bora na wenye uwezo mkubwa,” alisema.
Lusajo alipotafutwa kuzungumzia hilo, alisema muda muafaka utakapofika ataweka wazi timu atakayoichezea kwa msimu ujao.