Unguja. Wakati Yusuph Mwenda akiteuliwa kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mambo sita yanatajwa kumbeba katika ufanisi na kuimarisha mapato wakati akiwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) ikiwa ni pamoja na kujenga ukaribu na wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari.
Mwenda anakuwa bosi wa TRA baada ya aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo, Alphayo Kidata kuteuliwa kuwa Msaidizi wa Rais Ikulu. Uteuzi huo umefanyika jana Jumanne, Julai 2, 2024.
Mwenda aliteuliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kuwa Kamishna Mkuu wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Machi Mosi 2022 kabla ya kubadilishwa kuwa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) mwaka 2023. Mwenda alichukua nafasi ya Salum Yussuf Ali ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.
Wakati anateuliwa na Dk Mwinyi kushika nafasi hiyo, Mwenda alikuwa ofisa TRA. Pia aliwahi kuwa Diwani wa Mikocheni (CCM) na Meya wa Kinondoni, Dar es Salaam kuanzia mwaka 2010/2015 na wakati akihudumu umeya alikuwa mtumishi wa TRA.
Wakati Mwenda anateuliwa kushika nafasi hiyo, alikuta makusanyo kwa mwaka Zanzibar yalikuwa Sh374 bilioni (mwaka 2021) ikapanda hadi kufikia Sh374 bilioni, kisha kafika Sh565.8 bilioni na mwaka huu 2023/24 hadi kufikia Juni ZRA imekusanya Sh718.7 bilioni kati ya lengo la kukusanya Sh675.6 bilioni sawa na ufanisi wa asilimia 106 ya lengo la makusanyo ya kodi tarajiwa.
Taarifa iliyotolewa na Mwenda mwenyewe kabla ya kuteuliwa kwenda TRA jana Julai 2, 2024 kwa vyombo vya habari, alisema makusanyo hayo yameongezeka kwa asilimia 27.01 sawa na Sh152.8 bilioni ikilinganishwa na mapato halisi ya mwaka wa fedha uliopita 2022/23 ambayo yalikuwa Sh565.8 bilioni.
Mwananchi Digital linaangazia safari ya Mwenda ndani ya ZRA ambaye wakati anashika nafasi hiyo alibadilisha mtazamo wa wafanyabiashara na wafanyakazi kuwaweka karibu na mamlaka hiyo badala ya wafanyabiashara kuiona mamlaka hiyo kama maadui bali waone kama marafiki na kuwa sehemu ya kutatua changamoto zao.
Hakuwa mtu wa kukaa ofisini
Tofauti na ilivyo kwa watendaji wengine, Mwenda alikuwa akitoka na timu yake kwenda katika maeneo mbalimbali kuzungumza nao na kusikiliza kero zao huku akiwauliza ni namna gani wanaona utendaji wa ZRA na nini cha kufanya ili kubadilisha utendaji huo.
Alianzisha utaratibu wa kutembelea wafanyabiashara mmojammoja na makundi kuzungumza nao na kusikiliza kero zao jambo ambalo lliliwaweka wafanyabaishara hao karibu na kuona hakuna sababu ya kukimbia watendaji hao.
Wakati akizungumza nao walimueleza jinsi ambavyo kuna unyanyasaji wa ulipaji kodi, kukadiriwa tofauti huku wakituia nguvu kudaiwa mapato.
Hatua hiyo ilisaidia ambapo waliweka mifumo mizuri ya ulipaji, kuna wakati wafanyabaishara walisamehewa kupeleka makusanyo ya kodi ya nyuma, kisha wafanyabiashara ambao mtaji wao haufiki milioni tano walisamehewa kulipa kodi.
“Nakumbuka kabla ya hapo wafanyabiashara walikuwa wakiona watumishi wa ZRA ni maadui na walikuwa wakitumia nguvu kubwa kudai, biashara zilikuwa hazifanyiki lakini alipoingia huyu bwana (Mwenda) alituliza jambo hilo,” amesema mmoja wa wafanyabiashara wa Darajani, Haroun Saleh
Mfanyabiashara mwingine, Khamis Sultan amesema ukaribu wa Mwenda na wafanyabaishara ndio jambo lililombeba kwani hakuwa mtu wa kutumia ubabe na kutaka kulazimisha mambo ili yaende.
“Unajua shida moja ya watendaji wetu akishepewa malengo na nguvu kimaamlaka wanaamini kutumia nguvu na ubabe ndio itasaidia, lakini kumbe mambo mengine yanahitaji ubunifu na kutengeneza mikakati, katika hili Mwenda alifanikiwa kwa kiasi kikubwa.” amesema
Kingine kilichoanzishwa na Mwenda ni kuwafunda watumishi wa mamlaka na wakati mwingine kuchukua hatua iwapo wakibaini kuna mtumishi amekwenda kinyume na maadili. Katika hili alipiga marufuku hakuna mtumishi kwenda kwa wafanyabiashara bila kuvaa kitambulisho chake na kutumia kauli za kiungwana.
Kuanzisha ofisi za mikoa kimamlaka
Mambo mengine aliyofanya Mwenda ni kufungua Ofisi za Mikoa mpaka sasa kwa upande wa Unguja kuna ofisi tano ambazo zina wasimamizi na iwapo wafanyabiashara wakiwa na shida wanamaliza changamoto zao huko walipo bila kufuata huduma hiyo makao makuu ya ZRA Mazizini.
Awali, wafanyabiashara walilazimika kutembea umbali mrefu kupanga foleni kutoka mikoa Kusini na Kaskazini kufuata huduma makao makuu lakini kwasasa zipo ofisi katika miji mikuu ya mikoa hiyo, Paje Kusini Unguja na Nungwi Kaskazini Unguja huku Mkoa wa Mjini wa Magharibi kiserikali ukiwa na mikoa miwili ya ZRA, ambayo ni Aman na Michenzani Mall.
Wakizungumzia jambo hilo baadhi ya wafanyabiashara walieleza jinsi ilivyoondoa changamoto hiyo.
Motisha utoaji wa risiti za kielektroniki
Katika kuangalia namna ya kuendelea kukusanya kodi kwa hiari, Mwenda alianzisha utoaji wa motisha kwa wananchi wanaodai risiti za kielektroniki na wafanyabiashara wanaotoa risiti hizo hivyo kuongeza kasi ya wananchi wanaodai risiti na wafanyabiashara kutoa risiti kwa hiari.
Katika kipindi cha Mwenda imeboreshwa na kuanzishwa mifumo mipya ikiwemo ambayo wafanyabiashara wanatuma changamoto zao moja kwa moja na kupeleka mauzo yao bila kuwapo uhitaji wa kufika ofisi za ZRA.
Mara kadhaa Mwenda alikuwa akisema kinachosaidia kukiwa na mifumo mizuri ya ulipaji kodi inajenga usawa hakuna anayependelewa wala kuonewa kila mtu analipa anachokistahili.
Pamoja na mafanikio aliyoonyesha Mwenda amekuwa akisema bado kuna wafanyabiashara wachache wanaondelea kukwepa kodi kwa kuendesha biashara zao bila kusajili na kutotoa risiti.
Hata hivyo, alikuwa akiendela na mipango ya kuhakikisha wanawatumia masheha wa shehia kuwatambua watu wanaoendesha biashara kinyume na utaratibu ili wawafikie na kuwapa elimu kabla ya kuwachukulia hatua.
Kutokana na utendaji kazi uliotukuka Rais wa Zanzibar, Mwinyi Desemba 29, 2023 wakati wa kilele cha mwezi wa shukrani na furaha kwa mlipakodi sherehe za mlipa kodi alimpongeza kuwa ni mbunifu na kuleta mabadiliko makubwa katika utendaji wa mamlaka hiyo ikilinganishw ana kipindi kilichopita.
“Nimekuwa nikisema hapa kama mtu akifanya vibaya mseme hadharani, vilevile akifanya vizuri pia mseme hadharani, Kamishna nikupongeze na watendaji wako haya mapato tunayoyapata kama sio mabadiliko ya ZRA tusingeyapata,” alisema Dk Mwinyi
Alisema kwa kipindi kirefu Zanzibar ilikuwa haitekelezi miradi mikubwa kama ambavyo imetekelzwa kwa sasa ikiwemo miradi ya maji, barabara, afya, elimu na viwanja vya michezo na ndege na kwamba hayo yote yanafanyika kwasababu ya ufanisi wa makusanyo na matumzi sahihi ya fedha hizo.
Alitumia fura hiyo kuiagiza Wizara ya Katiba, Utumishi na Utawala Bora kuangalia namana kubadilisha mishahara ya watumsihi wa mamlaka hiyo kutokana na utendaji mzuri unaotukuka akisema taasisi inayoongeza mapato kwa silimia 51 hakuna budi na serikali kuiangalia kwa namna ya pekee.
Kibarua kinachomsubiri TRA
Wakati akienda kuanza majukumu yake mapya TRA, Mwenda anasubiriwa na kibarua kizito katikati ya mgomo wa wafanyabiashara wakilalamikia utitiri wa kodi na madai ya watumishi wake kutumia ubabe na kamatakamata ya wafanyabiashara na wateja wao.
Hatua hiyo ilisababisha mgomo wa wafanyabiashara ulioanziaKariakoo, jijini Dar es Salaam na kusambaa mikoa ya Mbeya, Dodoma, Iringa, Kigoma, Ruvuma, Morogoro, Kagera na Mwanza.
Wakizungumza kuhusu hatua hiyo ya Mwenda kuchukua kijiti, baadhi ya wafanyabaishara wa Zanzibar wamesema iwapo akienda na falsafa yake ya kusikiliza kwanza kero za wafanyabiashara na kuzitafutia ufumbuzi kabla ya kuchukua uamuzi, atavuka kihunzi hicho. Kinyume chake atapata wakati mgumu.
Abubakar Mohmud, maarufu Mudi amesema Mwenda anakibarua kigumu kwasababu kila kitu kinabadilika kuanzia mazingira na ukubwa wa eneo hivyo vinaweza kumpa changamoto.
Hata hivyo, amesema kwa uzoefu na uwezo alioonyesha kwa kipindi cha miaka takribani mitatu ameonyesha ubunifu kwahiyo akijipanga vyema anaweza kukabiliana na changamoto za biashara kwa upande wa ZRA.
Mwingine Ashuna Sharif amesema: “Mimi sina wasiwasi na huyu baba (Mwenda), kwa mtu aliyeona alipoitoa Zanzibar sidhani kama atakuwa na ugumu isipokuwa ni kuendeleza mifumo ileile na kuwapa somo watendaji wake kwenda katika mazingira anayoyataka yeye.”
Kauli hiyo haikutofautiana na Khatib Suleiman aliyesema ubunifu ndio unamsaidia mtu badala ya kutumia mabavu na kutaka kuzingatia sheria.
“Sheria zipo na lazima zifuatwe lakini kuna wakati mwingine unahitaji kutumia busara kwanza kabl ya kutekeleza sheria, sasa hiki watu wengi wanashindwa. tunaamini ataendeleza mazuri aliyokuwa nayo huku na atafanikiwa kuwaweka wafanyabaishara na TRA pamoja,” amesema.
Alipotafutwa na Mwananchi Digital leo asubuhi Jumatano, Mwenda licha ya kutotaka kuzungumza zaidi akisema protokali hazimruhusu kwasababu hajaapishwa, lakini amesema atafanya kazi anayotumwa na kushukuru kwa kuendelea kuaminiwa zaidi na mamlaka za juu.
“Nashukuru lakini niwapongeze na nyie waandishi wa habari tumefanya kazi kubwa kwa pamoja, lakini kwasababu sijaapishwa siwezi kuzungumza zaidi. Najua wewe unayafahamu tuliyofanya pamoja lakini ninayokwenda kufanya TRA nitazungumza vyema mikaati yangu baada ya kuapishwa, lakini hata ZRA sitawatupa si unajua kwamba hata huku (Zanzibar) ZRA ipo,” amesema Mwenda.