Mambo ya kuzingatia kuwa na afya bora, wanaopenda soda wapewa neno

Dar es Salaam. Wataalamu na wadau wa afya nchini Tanzania wameshauri mambo saba yatakayosaidia mlo wa siku kutoharibu mwili ikiwemo kuepuka chumvi nyingi na sukari.

Mambo mengine ambayo endapo hayataepukwa huleta shida kiafya, ni unywaji wa pombe uvutaji wa tumbaku, kutoshughulisha mwili na kutozingatia usafi wa mazingira na chakula.

Wataalamu hao wa afya ya binadamu, wamesisitiza kama mtu hatozingatia lishe bora kama dawa basi atatumia dawa kama lishe.

Aina ya lishe anayopaswa kula mtu kwa siku, ni vyakula vyenye asili ya wanga, nyama, jamii ya mikunde, mbogamboga, matunda na mafuta yatokanayo na mimea, unywaji wa maji safi pamoja na kufanya mazoezi.

Wataalamu hao wametoa elimu hiyo kupitia mjadala ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Comunications Limited (MCL) kwenye mtando wa X space kwa ushirikiano na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) mada  ‘Mlo wa siku unavyoweza kuimarisha au kuharibu afya yako, tufanye nini. Umefanyika leo Jumatano, Julai 3, 2024.

Akichangia mjadala huo, Ofisa Lishe Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Maria Ngilisho amesema ni muhimu kuepuka matumizi kupita kiasi ya chumvi na sukari.

Amesema mtu anayekunywa soda huingiza kiwango kikubwa cha sukari mwilini, huku ulaji wa chipsi na vyakula vya kuongezwa chumvi akisisitiza siyo salama kwa afya.

“Ni muhimu kuwa na mazingira safi na chakula salama kwani ukila chakula kichafu utaharisha na mwili utapoteza virutubisho,” amesema.

Kuhusu mfumo wa ulaji, Maria amesema kisayansi mwili wa binadamu umeumbwa kula mara tatu kwa siku kwa wastani wa saa nane kutokana na mmeng’enyo na aina ya chakula.

“Kula mara tatu kwa siku sio lazima kuwa na makundi yote sita kwa kila mlo ila tunasisitiza angalau kuwe na makundi manne kwa kila mlo. Ikiwa hivyo kupata makundi yote sita kwa siku inawezekana,” amesema.

Maria amesema maziwa ndiyo chakula chenye virutibisho vyote hivyo kwa mtoto wa binadamu anapaswa kunywa maziwa ya mama yake.

“Mtoto akiwa na umri chini ya mwaka mmoja asipewe maziwa ya ng’ombe hadi pale kunapokuwa na changamoto inayolazimu lakini hadi pale yatakaporekebishwa na mhudumu wa afya ndipo apewe,” amesema.

Amesema maziwa hayo yatarekebishwa kulingana na umri wa mtoto na uzito wake na mwenendo wa ukuaji kwa ujumla.

Kwa upande wake, Daktari wa Binadamu Edger Rutaigwa amesema ni muhimu nusu ya sahani ya chakula anachokula mtu iwe ni matunda na mboga za majani.

“Mboga za majani fungu ni Sh500 hadi Sh1,000 hii ni tofauti na kuku waliotengenezwa viwandani, kwahiyo vyakula vinavyopatikana kwa bei nafuu ndio vina afya zaidi,” amesema.

Kuhusu vinywaji vya sukari nyingi hasa soda amesisitiza kuepukwa kwani kinywaji hicho kwani chupa moja mwilini ni sawa na vijiko 10 hadi 12 za sukari.

Amesema wapo watu kwenye jamii hutumia chupa tatu za soka kwa siku akisema hali hiyo ni hatari kwani mwili unakuwa na kiwango kikubwa cha sukari.

Dk Rutaigwa amesema kama mtu hatozingatia lishe kama dawa basi atatumia dawa kama chakula.

Mtaalamu huyo amesisitiza umuhimu wa kunywa maji ya kutosha wakati wote pamoja na kula parachichi na karanga kuongeza mafuta yasiyo na athari mwilini.

Awali, akichokoza mada hiyo, Mhariri wa Afya Gazeti la Mwananchi, Harieth  Makweta amesema kutokana na ulaji usiozingatia lishe, Mkoa wa Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza wanawake wamebainika kuwa na uzito mkubwa kutokana na lishe wanazotumia na kutoshughulisha miili yao.

Amesema kutokana na ulaji usio sahihi kundi la vijana wmekuwa waathirika akiwataja wanafunzi kushindia miogo kitendo anachotaja kunasababisha mwili kukosa virutubisho mbalimbali.

Akinukuu utafiti uliotolewa na Wizara ya Afya ukiangazia hali ya malaria na lishe kwa wanafunzi wa miaka mitano hadi 19 mwaka 2019, Harieth amesema asilimia 25 ya wanafunzi hao walibainika kuwa walidumaa.

Pia asilimia 33.7 ya wanafunzi wenye miaka mitano hadi 19 walibainika kuwa na upungufu wa damu wakati asilimia 6.2 walikuwa wanene kupita kiasi na asilimia 11.2 walikuwa wakondefu.

Akizungumzia suala la utapiamlo na udumavu, Herieth amesema Tanzania inazalisha chakula kwa asilimia 100 lakini bado kuna utapiamlo na udumavu kwa asilimia 30.

“Udumavu siyo tu kwa watoto bali huwa unakwenda maisha yako yote kama hukupata lishe bora utotoni. Hata katika hali ya utu uzima unaweza ukapata maradhi kama hauzingaiti afya. Wataalamu wa afya wanashauri watu kula makundi sita ya chakula mara tatu kwa siku,” amesema.

Amesema mlo wa siku unapaswa kuwa na vyakula vinne kwa siku na hiyo itawezesha mtu kupata makundi sita ya chakula kwa siku.

Mchangiaji mwingine kwenye mjadala huo, Mwemba Burton maarufu kama Mwijaku amesema anapitia magumu katika kuhakikisha anazingatia mlo, amesema kutokana na mtindo wake wa maisha inamuwia vigumu kuacha kula ambavyo vinakatazwa na wataalamu wa afya.

“Nilinunua vifaa vyote vya mazoezi lakini mtindo wa maisha unafanya nashindwa kufanya kwa kukosa muda, kuna vyakula vinakatazwa lakini nashindwa kuacha najikuta nakula kwa kusema ngoja nionje kidogo. Sasa swali langu kwa madaktari nifanyeje niwe na tamaduni ya kuzingatia mlo,” ameeleza.

Related Posts