Mvutano wa kisheria, tuhuma kuchoma picha ya Rais

Dar/Mbeya. Siku nne tangu Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limkamate Shadrack Chaula (24), kijana anayetuhumiwa kuchoma moto picha ya Rais Samia Suluhu Hassan, suala hilo limeibua mvutano wa kisheria, ikielezwa hakuna sheria iliyovunjwa.

Akizungumza na Mwananchi leo Julai 3, 2024 kuhusu kosa la kijana huyo na lini atafikishwa mahakamani, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema jukumu lao liliishia kumkamata suala la kupelekwa mahakamani linabaki kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

“Siwezi kusema ni lini atapelekwa mahakamani, kazi yetu ilikuwa ni kumkamata, Ofisi ya Mashtaka ndiyo itaandaa mashtaka kwa kuangalia ushahidi na kuonyesha ni vifungu gani vya sheria mtuhumiwa amekiuka,” amesema.

Mmoja wa wanasheria katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoa wa Mbeya (jina lihifadhiwa kwa kuwa si msemaji), amesema hawana mamlaka ya kulizungumzia zaidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

“Hata kama jalada litafika mezani kwetu, tutaangalia kisheria ikoje baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kubaini kama kuna kesi, kisha inaangaliwa sheria na mwenye mamlaka wa kulisemea hili, kwa sasa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” amesema mwanasheria huyo.

Hata hivyo, juhudi za kumpata Mwanasheria mkuu wa Serikali, Eliezer Feleshi zinaendelea.

Suala hilo pia limeibua mjadala kwenye mitando ya kijamii na miongoni mwa waliolijadili ni Wakili Peter Kibatala aliyeandika ujumbe kupitia ukurasa wake, na baadaye alipotafutwa na Mwananachi kuufafanua, amesema amewaelekeza mawakili wiwili kwenda kutoa msaada wa kisheria kwa kijana huyo.

“Hatutaingilia maamuzi ya mkuu wa mkoa aliyetaka kijana huyo ahojiwe, lakini atakapopelekwa mahakamani ana haki ya kupata msaada wa kisheria, ndiyo maana niliwagiza mawakili wenzangu wawili kwenda kumsaidia kijana huyo,” amesema.

Wakili wa kujitegemea, Philip Mwakilima akizungumza na Mwananchi amesema hakuna sheria wala kifungu kinachoonyesha kuchoma au kutochoma picha ya kiongozi huyo ni kosa na hakuna athari yoyote kwa jamii.

Amesema hakuna uthibitisho wa moja kwa moja kwa mtu kuonyesha uhalisia au usahihi kuwa picha iliyochomwa ni ya Rais, kwani hakuna ushahidi.

“Je, hiyo picha iliyochomwa ilipigwa na mpigapicha wa Serikali? Atoke hadharani kueleza umma athari yake kwa jamii na Taifa, Nia ya huyo mchomaji ilikuwa na athari gani, ni nani anayeweza kuonyesha kifungu cha sheria kuwa kuchoma picha ni kosa?” amehoji.

“Kama picha ni ya kuchora, imefanana na sura ya Rais? Kwani imeonyesha uhalisia wa kuwa ni yeye? Hapo hakuna kinachoweza kuendelea,” amesema.

Chaula, mkazi wa Kijiji cha Ntokela wilayani Rungwe inaelezwa ni msanii wa sanaa ya uchoraji.

Alikamatwa akituhumiwa kurekodi video na kuisambaza mitandaoni akichoma picha ya Rais Samia.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, akizungumzia tukio hilo alisema: “Nimeona video ikionyesha mwananchi mmoja wilayani Rungwe akimkashifu Rais Samia. Mimi kama mkuu wa mkoa sijaridhishwa na jambo hilo, kwanza si utamaduni wa wana-Mbeya kukashifu viongozi wetu wa kitaifa, tuwaache wafanye kazi za kutuhudumia ili walete mabadiliko makubwa kwenye jamii.”

“Jambo la pili namwelekeza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga kuhakikisha anamsaka kijana huyo ambaye ametoa maneno ya kashfa kwa viongozi wetu wa nchi, hasa Rais Samia.”

Wakili Michael Lugina amesema wanaendelea kufuatilia taratibu za kijana huyo kupelekwa mahakamani na endapo atafikishwa watampatia msaada wa kisheria.

“Kijana alikamatwa baada ya agizo la mkuu wa mkoa, hasa kutokana na ile video yake, sisi tumeona kijana yule huenda asipate msaada wa kisheria, ndiyo maana tumeamua kumsaidia,” amesema.

Amesema kulingana na sheria, mkuu wa mkoa ana haki ya kuagiza mtu akamatwe pale anapoona anahatarisha usalama lakini mtuhumiwa hapaswi kushikiliwa zaidi ya saa 24 bila kufikishwa mahakamani.

“Tunaendelea kufuatilia utaratibu wa kupelekwa mahakamani, kama hawatampeleka sisi tutakwenda kuwashtaki polisi na mkuu wa mkoa kumlipa huyo kijana fidia,” amesema.

Wakili Michael Mwangasa amesema ni mtazamo wake kuwa hakuna kosa lililotendeka na hakuna anayeweza kueleza iwapo ni kweli alichoma picha.

Amesema na hata kama aliichoma, amehoji ni wapi imeandikwa ni picha Rais na si ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Diwani Kata ya Ndato, Samweli Majuto amesema tukio hilo limezua taharuki kwani jamii imeshindwa kuelewa alitumia muda gani kujipiga picha na kutuma kwenye mitandaoni. 

“Hata sisi tukio hilo tulishtuka baada ya kusambaa mitandaoni, mlengwa ni kijana mtiifu na anaishi vizuri na jamii, hana matukio mabaya na anashirikiana vyema katika maendeleo,” amesema.

Amesema hawatambui ilikuwaje kama alikuwa peke yake au kuna watu waliohusika kumpiga picha na kutuma kwenye mitandao ya kijamii.

Mkazi wa Kijiji cha Ntolela, Jeremia Peter amesema kitendo hicho kimejenga taswira mbaya.

Related Posts