Mkoa wa Songwe umeendelea kukumbwa na matukio ya vifo vya wanamichezo wakiwa uwanjani baada ya Julai 2, 2024 mwamuzi Hedman Mwashoga kuanguka na kufariki.
Mwamuzi huyo alikuwa akichezesha mechi baina ya Monaco dhidi ya Viena FC kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Msanyila katika mwendelezo wa Ligi ya Kijiji cha Msanyila mkoani humo.
Hili ni tukio la tatu katika miaka miwili mfululizo ambapo Aprili 10, 2023, mchezaji Albert Andrea alipogongana na mwenzake alifariki.
Tukio kama hilo lilitokea tena Machi 28 mwaka huu, ambapo mchezaji Bille Mgalla alianguka wakati akijaribu kuufuata mpira wa juu akiwa na mpinzani wake, akafariki.
Julai 2, 2024 mwamuzi huyo akiwa katika majukumu yake alianguka ghafla na kupoteza fahamu, ambapo alikimbizwa katika Hospitali ya Isansa na kukutwa ameshafariki.
Mmoja wa wadau wa michezo na maendeleo mkoani humo ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo, Onesmo Mkondya amesema mwamuzi huyo amefariki akiwa katika majukumu yake.
“Ligi ni ya Kijiji cha Msanyila na aliyetoa zawadi katika mashindano hayo ni Mkuu wa Mkoa, Daniel Chongolo, hadi sasa imefikia hatua ya robo fainali, ambapo refa huyo akiwa katika kazi yake alidondoka na alipowahishwa Hospitali alikutwa ameshafariki,” amesema Mkondya.