Mwanza. Wakati Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) likitarajia kupokea ndege mpya aina ya Boeing 787- 8 Dreamliner, shirika hilo limeshauriwa kuboresha huduma kwa wateja na kuongeza idadi ya safari ili kuvutia wateja na kustahimili kwenye soko la usafirishaji wa anga nchini.
Wito huo umetolewa leo Jumatano Julai 3, 2024, na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jengo maalum la wateja wa hadhi ya juu ‘Business Class’ lililojengwa na Shirika la VIA Aviation katika Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Mwanza.
Huku akidokeza ofisi yake ofa nane za kampuni za ndege za kimataifa kuhitaji kufanya safari katika uwanja huo, Mtanda ameeleza kutofurahishwa na tabia ya safari za ndege za shirika hilo kuahirishwa bila wateja kujulishwa jambo alilodai ni kufanya kazi kwa mazoea na kusababisha usumbufu kwa wateja.
“Ninayasema haya kwa sababu hii ni biashara na tusipozungumza wakati wateja wenu wanalalamika kwenye suala hilo tutakuwa hatutendi haki. Ili muweze kushindana na wengine lazima muboreshe huduma kwa wateja kwa sababu biashara ni ushindani na huduma kwa wateja,” amesema Mtanda.
Kupitia mkoa huo wenye wakazi zaidi ya milioni 3.6 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022, Mtanda amesema wageni na wenyeji wake wanategema huduma ya usafiri wa anga huku kimbilio lao likiwa ni ATCL. Pia ameiomba ATCL kuweka unafuu wa gharama ya nauli ili kumwezesha kila mwananchi kutumia huduma zake.
“Hapa Mwanza ili upate tiketi ya Air Tanzania lazima uikate siku tatu, nne au tano kabla ya safari ndani ya siku mbili kuelekea safari yako huwezi kupata tiketi maana yake watu wenye haraka na wenye dharura hawawezi kusafiri,” amesema.
“Hata mimi RC nikiitwa Dar es Salaam inabidi nibanane na meneja nimwambie nimeitwa pale Ikulu sasa atalazimika atafute abiria mwenye unyenyekevu ampunguze kwa sababu Serikali lazima iwe kazini muda wote. Matindi ututafutie ndege nyingine ikibidi hiyo inayokuja ileteni Mwanza,” amesema Mtanda.
Kiongozi huyo amesema katika kutambua changamoto ya usafiri wa anga mkoani Mwanza, Serikali inatumia Sh13 bilioni kufanya maboresho katika jengo la abiria ambalo likikamilika litahudumia abiria wa kitaifa zaidi ya 800 na kimataifa zaidi ya 600 kwa wakati mmoja.
“Yale mambo ya ku-cancel (kuahirisha safari za ndege) halafu tunakuja hadi uwanjani hata meseji hakuna, Matindi hilo lifanyieni kazi. Siku moja nakuja hapa naambiwa eti hiyo ndege imeahirisha safari leo sasa simu zetu si hawa watu wa ATCL wanazo. Wananyue simu watuarifu,” amesema.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Biashara ATCL, Patrick Ndekana, shirika hilo limesafirisha
Mkurugenzi Mkuu ATCL, Ladislaus Matindi amekiri mahitaji ya Mkoa wa Mwanza kwa huduma hiyo kuwa makubwa huku akidokeza kuwa shirika hilo lazima lihakikishe huduma hiyo inafikishwa kila eneo nchini ili kufikisha huduma kwa kila mtanzania bila kujali mahala alipo.
“Ndege kubwa inakuja asubuhi na jioni, mchana zinakuja hizo ndege ndogo bado hazitoshelezi mahitaji ya wenzetu wa Mwanza, ndani ya nchi tunakwenda vituo 10 ikiwemo Kilimajaro, Bukoba, Songea, Mbeya, Arusha, Kigoma, Zanzibar wote hawa lazima wapate huduma ili ni shirika la Watanzania lazima wahudumiwe wote hata kwa kiasi kidogo,” amesema Matindi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Biashara na Mauzo wa ATCL, Patrick Ndekana hadi kufikia Juni 2024, ATCL imebeba abiria 1,123,696, wastani wa abiria 93,000 kwa mwezi huku abiria 253,593 kati yao wakibebwa kutoka na kwenda kituo cha Mwanza pekee sawa na asilimia 23 ya abiria wote waliobebwa katika safari za shirika hilo.
“Wastani wa ujazo ni zaidi ya similia 90 hii ikiashirika kuna uhitaji wa kuongeza miruko kwa mkoa wa Mwanza. Kuanzia Julai 14, 2024, tutaanza kutumia ndege aina ya Boeing 737 Max 9 yenye uwezo wa kubeba abiria 181 kwa tripu moja na tani mbili za mizigo. Hii itakuwa chachu itatuwezesha kutoa huduma ya usafiri wa anga nchini na mizigo, hii ni ongezeko la viti takribani 49,” amesema Ndekana.
Ndekana amesema kwa sasa ndege kubwa inayofanya safari zake kwenda Mwanza ni Airbus 220 inayobeba abiria 132, hivyo, kuongeza uwezo wa abiria 49 kutaongeza ufanisi na huduma kwa wakazi wa mkoa huo.
“ATCL ina ndege 14 zinazoruka na tunategemea kupokea ndege moja aina ya Boeng 787-800 mwezi Agosti. Pia tuna ndege ndogo ya viti 50 ambayo ni Bombadier Q300 ambayo tunategema ilikuwa matengezo muda wowote kuanzia sasa itakuwa kwenye operesheni zetu,” amesema Ndekana.
Katika hatua nyingine, Ndekana amesema uzinduzi wa jengo hilo maarufu kama ‘Serengeti Lounge Via Aviation’ litasaidia kuboresha huduma kwa wateja wa waaminifu wa ATCL zaidi ya 58, 475, wateja 870 kati yao wakiwa wa daraja la juu. Pia amesema Novemba mwaka huu, shirika hilo litaongeza safari za ndege kwenda Dubai kutoa nne kwa wiki hadi kila siku.