Sativa afanyiwa upasuaji kwa saa sita

Dar es Salaam. Mkazi wa Mbezi, jijini Dar es Salaam, Edgar Mwakabela maarufu Sativa aliyetoweka Juni 23 na kupatikana Juni 27 pori la Hifadhi ya  Katavi akiwa na majeraha katika mwili wake, amefanikiwa kufanyiwa upasuaji wa taya la kushoto lililosagika baada ya kudaiwa kupigwa risisa ya kichwa.

Sativa alipatikana Juni 27, katika hali mbaya akiwa anavuja damu baada ya kuteswa na watu waliomchukua, huku akilalamika maumivu ya kichwa, miguu na mikono iliyokuwa na michubuko ya panga.

 Sativa anayejishughulisha na biashara ya miamala ya fedha, anapatiwa matibabu Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam baada ya kubainika kupata mpasuko wa taya la kushoto lililosagika uliotokana na risasi anayodaiwa kupigwa maeneo ya kichwani.

Kwa mujibu wa wasimamizi wa matibabu ya Sativa, wamesema madaktari bingwa wa Aga Khan jana Jumanne Julai 2, 2024 wamefanikiwa kumfanyia upasuaji uliochukua saa sita kukamilika kwake.

Taarifa aliyoaichapisha leo Jumatano Julai 3, 2024 katika mtandao wake wa X (zamani Twitter), Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa baada ya Sativa kufanyiwa upasuajia anaedelea vizuri katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU).

“Mapema asubuhi ya leo Julai 3, Paul Kisabo ambaye ni wakili wa Sativa na Mkuu wa Idara ya Ulinzi wa @THRDCOALITION alitembelea chumba cha ICU pamoja na mama yake Sativa, mjomba wake, shangazi yake na mdogo wake na kumkuta akiendelea vizuri,” ameandika Ole Ngurumwa.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Kisabo amesema Sativa anaendelea vyema huku akipatiwa uangalizi wa karibu na madaktari wa Aga Khan. Amesema upasuaji wa Sativa ulianza saa 11 jioni hadi saa nne usiku.

“Kama hali yake itazidi kutengemaa basi atarudishwa katika wodi ya kawaida, lakini kwa hatua ya sasa tunamshukuru Mungu upasuaji wake umekwenda vizuri,” amesema Kisabo.

Ujumbe kama huo wa Ole Ngurumwa uliandikwa na Martin Masese maarufu ‘MMM’ akisema: “Ndugu yetu @Sativa255 amefanikiwa kufanyiwa upasuaji mkubwa katika taya lake la upande la kushoto. Amerudishwa ICU kwa ungalizi hadi atakaporejea katika hali yake, tuendelee kumuombea. 

Wakati Sativa akiendelea na matibabu hospitalini hapo, wadau mbalimbali wanaendelea kujitokeza kufanikisha mchakato pia Rais Samia Suluhu Hassan jana Jumanne alichangia Sh35 milioni.

Related Posts

en English sw Swahili