SPOTI DOKTA: Euro 2024 haya yamewabeba kufika robo fainali

HATUA ya 16 Bora ya Euro 2024 ilimalizika juzi usiku na kesho, Ijumaa, robo fainali ya kundi la kwanza kwa mechi kali mataifa yenye ligi bora katika soka duniani Hispania vs Ujerumani na Ureno vs Ufaransa itaanza.

Nchi ambazo zimefanikiwa kuingia robo fainali ni zile ambazo ndizo zina wachezaji wengi ambao walitoka kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuzipa klabu zao mafanikio.

Hatua hii ina mvuto wa kipekee kwani imejaa ushindani mkubwa kukiwa na mastaa wakubwa wenye umri mkubwa wakiwa wanazibeba timu.

Ukiachana na ufundi mwingi wa kisoka toka katika benchi la ufundi ambao mataifa hayo wanayo, lakini bado kuna mambo mengine ya kitabibu ambayo yanachangia kuzibeba timu hizo.

Haraka haraka ukitazama timu zote hizo hazikuita wachezaji ambao ni majeruhi au wenye historia ya majeraha ya mara kwa mara. Hii ilikuwa ni faida kwao kuweza kuvuka hatua hizi wakiwa imara.

Katika kuelekea hatua ya robo fainali timu hizo zimepata pia nafasi ya wachezaji kupata mapumziko marefu. Hii  inasaidia kuwawezesha wachezaji kupona vijijeraha vidogo vidogo vya misuli ya paja.

Mtakumbuka beki wa kati wa Ujerumani, Antonio Rudiger anayechezea Real Madrid alipoitwa katika timu ya taifa alikuwa na jeraha la wastani la misuli ya paja ambalo halikuwa tishio katika utimamu.

Kipindi wanapopata mapumziko kama hayo ndicho hutoa nafasi kwa mwili kuweza kukabiliana na majeraha ya ndani hasa yale yatokanayo na michezo wakati wakicheza.

Utimamu wa jumla wa wachezaji hao ndio unawabeba kuweza kustahimili mikikimikiki ya mashindano hayo ambayo mechi zake huwa zina ratiba yenye mpishano wa siku chache.

Angalau katika hatua hii ndipo ambapo wachezaji hupata nafasi za kupata huduma mbalimbali ikiwemo za kuusaidia mwili kuweza kupona haraka vijijeraha vya misuli.

Mchezaji wa soka sio lazima apate majeraha kwa kuchezewa faulo, anaweza kupata majeraha ya ndani kwa ndani ya misuli wakati akicheza au anapofanya mazoezi ya timu.

Hii ni kutokana misuli ya mwili inafanya kazi, wakati wakucheza au kufanya mazoezi huwa inavutika na kutulia. Kipindi hii hiki huweza kuvutika kupita kiasi na kupata vijeraha vya ndani kwa ndani.

Kwa hatua kama hii na kufika hapo vitu vinavyochangia kuwabeba ni ustahimilivu wa mwili uliojengwa kwa mazoezi na lishe, mwili kupata huduma saidizi za uponaji vijeraha vya ndani kwa ndani ikiwamo usingaji wa misuli yaani massage.

Vile vile matumizi ya tiba ya kisasa ya majeraha wastani ya maumivu ya misuli kwa mabafu au mapipa ya baridi kali ambayo husaidia kuondoa mkazo wa misuli na uchovu mkali.

Mchezaji anapopata huduma hii huweza kujiona mpya kutokana na kuondoka na maumivu na uchovu wa mwili. Hii inawafanya kucheza michezo inayofuata akiwa imara kiafya.

Faida kubwa ambayo wachezaji katika hatua hii wanapata ni kupata muda mwingi wa mapumziko na kulala masaa mengi hivyo kuwezesha mwili kujikarabati na kusahihisha matatizo ya ndani ya mwili.

Ukiacha kupumzika na kulala, mchezaji anapopata muda mwingi huweza kupewa muda wa kupata burudiko yaani relaxation. Hupewa nafasi binafsi ya kuwa katika mazingira mazuri kusikiliza muziki, kuogelea, kucheza michezo ya tv pamoja na burudani zingine.

Hii inawafanya kuweza kuwa na utulivu wa kimwili na akili hatimaye mwili mzima kuwa imara katika kila eneo.

Ukiacha mlo mkubwa unaozingatia maelekezo ya mtaalamu wa lishe wakati wa mapumziko hutakiwa muda mwingi kunywa maji na juisi au matunda mara kwa mara ili kuufanya mwili kuwa na maji mengi.

Wataalamu wa afya ikiwamo wale wa saikolojia huwa hawapo mbali na wachezaji wao. Wanahakikisha kuwa wanakuwa sawa katika afya ya akili kuweza kujiamini na kushinda.

Ndio maana utaweza kuona tofauti kubwa wachezaji watakavyocheza katika hatua ya robo fainali na ukilinganisha katika hatua za makundi ambayo miili ili bado hajapata mikikimikiki mikubwa.

Mojawapo wa adui wa hatua hii kwa wachezaji huwa ni majeraha ya misuli ya paja ambayo wachezaji wa soka huwa ni vigumu kuyakosa.

Ukiacha kupata kila mara majeraha ya mvutiko na mchaniko wa misuli ndani kwa ndani ambavyo mwili huweza kusahihisha na kupona siku chache.

Saa zingine ni kawaida kwa mchezaji ambaye anatumika sana  kuweza kupata majeraha makubwa ya misuli ikiwamo yale ya michaniko mkubwa wa misuli ya paja.

Ni kawaida pia kwa mchezaji asipate matatizo makubwa ya paja lakini akapatwa na tatizo la uchovu mkali wa mwili. Hii inaweza kujitokeza kama mchezaji atakuwa mwili wake umetumia nguvu nyingi.

Na inaweza kuchochewa na vijeraha sugu vya ndani kwa ndani au kuzembea kupasha mwili moto au kutofanya mazoezi lainishi ya viungo yanayowezesha kuwezesha uponaji.

Vile vile kupata tatizo la mkazo mkali wa misuli wakati wakucheza inaweza kutishia mchezaji kucheza vizuri kwani hiyo ni ishara ya msuli kuwa katika tishio la kufanya kazi ya kukunjuka.

Vile vile katika maeneo ya maungio makubwa kama vile pajani na kiunoni, goti na kifundo huweza kupata vijeraha hasa katika ligamenti na tendoni.

Tishu hizo ndio zinaunda maungio yaani joint, maeneo haya yakipata majeraha ya wastani mpaka makubwa yanaweza kuwa adui kwa machezaji katika hatua hii.

Majeraha ya maungio huwa yanachelewa kupona kwa wakati kutokana na aina za tishu katika maeneo hayo kupata shinikizo kubwa la uzito wa mwili na huku yakipata damu chache ukilinganisha na misuli.

Katika hatua hii, pamoja na timu hizi kuundwa na wanasoka wenye pesa nyingi. Ni vigumu kusikia wameonekana klabu wakila raha na kunywa pombe. Wanatambua vitu hivi ni adui mkubwa kwa mchezaji na hivyo havipaswi kupewa nafasi.

Related Posts