Stars mtegoni Afcon 2025 | Mwanaspoti

WAKATI droo ya kuwania Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 zitakazopigwa Morocco ikifanyika leo, timu ya taifa ‘Taifa Stars’ ipo katika mtego wa kuangukia kundi gumu au mchekea kwenye droo hiyo ya upangajwaji wa makundi itakayochezeshwa leo Afrika Kusini.

Katika droo hiyo ambayo itachezeshwa jijini Johannesburg kuanzia saa 9:30 alasiri kwa muda wa Afrika Mashariki, Taifa Stars itakuwa katika chungu cha tatu ambapo katika kundi itakalopangwa, itakuwa na timu moja kutoka chungu cha kwanza, moja kutoka chungu cha pili na moja kutoka chungu cha nne.

Timu 48 zitagawanywa katika makundi 12 yenye timu nne kila moja ambapo timu mbili zitakazoongoza kila kundi zitafuzu fainali za Afcon 2025 ambazo zitafanyika Morocco kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026.

Upangaji wa vyungu vinne vyenye timu 12 kila kimoja umezingatia viwango vya ubora vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa) vilivyotolewa mwezi uliopita ambapo chungu cha kwanza kinaundwa na timu ambazo zipo katika nafasi nzuri zaidi katika viwango hivyo vya ubora zikifuatiwa na zilizo katika chungu cha pili, chungu cha tatu na chungu cha nne.

Timu tishio zaidi ni zile zilizopo katika chungu cha kwanza kutokana na ubora wa vikosi vyake huku kile cha pili kikiwa na mchanganyiko wa baadhi ya timu ngumu na zile ambazo zinaonekana kuwa katika mzani mmoja na Taifa Stars huku za chungu cha nne nyingi zikiwa ni mchekea.

Kwa mujibu wa utaratibu wa uchezeshaji wa droo hiyo, Taifa Stars haiwezi kupangwa na timu yoyote kati ya zile ambazo ipo nazo katika chungu kimoja ambacho ni hicho cha tatu na timu hizo ni Kenya, Mauritania, Congo, Guinea Bissau, Libya, Comoro, Togo, Sudan, Sierra Leone, Malawi na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Chungu cha kwanza kina timu 12 vigogo ambazo zimekuwa na historia ya kushiriki na hata kufanya vizuri mara kwa mara kwenye fainali za Afcon ambazo mojawapo ni lazima ikutane na Taifa Stars na timu hizo ni Morocco, Senegal, Misri, Ivory Coast, Nigeria, Tunisia, Algeria, Cameroon, Mali, Afrika Kusini, DR Congo na Ghana.

Katika chungu cha pili ambacho pia kitatoa timu moja ya kuumana na Taifa Stars kwenye vita ya kuwania kufuzu fainali zijazo za Afcon kuna timu za Cape Verde, Burkina Faso, Guinea, Gabon, Guinea ya Ikweta, Zambia, Benin, Angola, Uganda, Namibia, Msumbiji na Madagascar.

Timu 12 ambazo zimepangwa katika chungu cha nne ni Niger, Zimbabwe, Rwanda, Gambia, Burundi, Liberia, Ethiopia, Botswana, Lesotho, Eswatini, Sudan Kusini na Chad.

Mechi za makundi za kuwania kufuzu Afcon 2025, zimepangwa kuchezwa kuanzia Septemba 10, 2024 na zitafikia tamati Novemba 19, 2024. Septemba 2 hadi 10 kutachezwa mechi za raundi ya kwanza na ya pili, raundi ya tatu na ya nne zitachezwa kati ya Oktoba 7 na 15 na Novemba 11 hadi 19 kutachezwa michezo ya raundi ya tano na ya sita.

Bahati kubwa kwa Taifa Stars ni kuanzia mechi hizo za makundi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam lakini pia itamalizia nyumbani kama ilivyo kwa timu kutoka chungu cha kwanza.

Mkurugenzi wa ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Oscar Milambo alisema kuwa shirikisho limejipanga kuhakikisha Taifa Stars inakuwa na ushiriki mzuri kwenye mashindano hayo.

“Ukitaka kuwa mkubwa lazima uwe na uwezo wa kushindana na wakubwa. Kuwekwa kwenye chungu cha tatu inaonyesha kwamba kuna hatua tumepiga lakini hatupaswi kufanya sherehe tunapaswa kufanya kazi ambazo zitatufanya tuwe miongoni mwa timu kubwa. Kama unavyoona tunaendelea na program za maendeleo kwa ukubwa wake lengo likiwa mwisho wa siku kuzalisha wachezaji wengi ambao sio watakuwa wengi bali wenye ubora,” alisema Milambo.

Kocha msaidizi wa Taifa Stars, Juma Mgunda alisema kuwa timu yake ipo tayari kukabiliana na mpinzani yoyote ambaye itapangwa naye kundi moja katika mashindano hayo ya kuwania kufuzu Afcon.

“Hakuna mashindano rahisi na hatuwezi kusema timu fulani ni ngumu na timu fulani ni nyepesi. Kila timu inayoshiriki mashindano ina lengo moja ambalo ni kufuzu Afcon kama ilivyo kwetu hivyo tunafahamu kwamba hakutakuwa na mshindani rahisi kwenye kundi lolote ambalo tutapangwa.

“Jambo la msingi ambalo tunatakiwa kufanya ni kujiandaa vyema kukabiliana na timu yoyote ambayo tutapangiwa nayo. Tunaamini kwa sasa tuko kwenye ubora na Mungu akipenda tutatimiza lengo letu,” alisema Mgunda.

Tanzania itaingia katika makundi ya mashindano hayo ikiwa inasaka kushiriki Afcon kwa mara ya nne baada ya kufuzu katika fainali za mwaka 1980, 2019 na 2023 ambapo mara zote iliishia katika hatua ya makundi.

Related Posts