Takukuru yataja athari za rushwa kwenye uchaguzi

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imesema rushwa ni chanzo cha kupatikana viongozi wasio na maadili, wasiozingatia misingi ya haki, usawa, uwazi, uwajibikaji na uzalendo.

Taasisi hiyo pia imesema rushwa inadhoofisha utawala bora na demokrasia na baadhi ya wananchi wenye sifa za uongozi bora hushindwa ama kugombea, kutoteuliwa au kuchaguliwa kwa kutokuwa tayari kutoa hongo.

Kutokana na hayo, taasisi hiyo imeainisha mbinu nne zinazotumika kufanikisha vitendo hivyo wakati wa uchaguzi, ambazo wananchi wanatakiwa kuwa makini nazo, matumizi ya fedha taslimu yakiongoza kwa asilimia 64.4.

Mbali na hiyo, uchambuzi huo uliotokana na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, umeonyesha kuwepo vitendo vya kugawa vitu/vifaa mbalimbali vinavyochukua asilimia 20, chakula na pombe ni asilimia 13.3 na kugawa mbolea asilimia 2.2.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Sulum Hamduni, alisema kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu 2025, viashiria vya vitendo hivyo vimeanza kujitokeza, hivyo ameitaka jamii kutoa taarifa.

Alisema miongoni mwa athari za rushwa ni upatikanaji wa viongozi wasio waadilifu, wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na kutozingatia misingi ya haki, usawa, uwazi, uwajibikaji na uzalendo.

 “Rushwa pia inasababisha uvunjifu wa amani kutokana na migogoro ya mara kwa mara ya kisiasa na husababishwa Taifa kuendelea kugubikwa na tatizo hilo, alisema Hamduni alipozungumza na wahariri wiki iliyopita”

Alisema wakati mwingine rushwa husababisha wananchi kukosa imani na Serikali, hivyo kuwapo machafuko.

“Vievile rushwa hudhalilisha utu kwa kufananisha thamani ya mtu na hongo ambazo zinaweza kutolewa kama vile fedha, nguo, chakula kwa lengo la kushawishi wananchi wamchague mgombea fulani au asimpigie kura mtu fulani,” amesema.

Hamduni amesema madhara hayo yanaweza kuepukika iwapo kutakuwa na mkakati wa pamoja na wadau katika kudhibiti vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi.

Alisema juhudi zikifanyika za kuongeza uelewa kwa wananchi kuanzia mtu mmoja mmoja kuhusu madhara ya rushwa kwenye uchaguzi, hali hiyo itadhibitiwa.

“Takukuru inaamini  mwananchi ambaye ni mpigakura anafahamu hadhi yake, na akitambua thamani yake hatakubali kurubuniwa kwa hongo na kudhalilisha utu wake kwa kupokea rushwa ili ama amchague kiongozi asiyefaa, aache kugombea au aache kupiga kura ambayo ni haki yake ya kikatiba,” alisema.

Alisema matokeo ya wananchi kushiriki vitendo vya rushwa ni kujikuta wanachagua bora viongozi na siyo viongozi bora.

Hamduni alisema upande wa Serikali umetimiza wajibu kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua kadhaa kuhakikisha uchaguzi ujao unakuwa huru na wa haki, usiogubikwa na vitendo vya rushwa.

Alitaja hatua hizo ni kuanzisha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kutunga Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani 2014, kutunga Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mtaa 2024.

Nyingine amesema ni kuendelea na maboresho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura 329, kuiwezesha zaidi Takukuru ili kwa kushirikiana na wadau wengine, iweze kuzuia na kupambana na rushwa katika uchaguzi.

Hamduni alisema Takukuru kwa kuzingati sura 329 imejizatiti kuendelea kutimiza wajibu wake wa kuzuia na kupambana na rushwa, ikiwamo katika uchaguzi.

Miongoni mwa hayo alisema ni kuelimisha wananchi kuhusu madhara ya rushwa katika uchaguzi ili waweze kuchagua viongozi waadilifu.

Pia kushirikina na wadau kuhamasiha wananchi kutojihusisha na vitendo vya rushwa, hasa nyakati za uchauguzi, na kufanya kazi za utafiti na udhibiti ili  kubainisha mianya ya rushwa katika uchaguzi na kushauri namna bora ya kuiziba.

“Kuchukua hatua za haraka za kuzuia vitendo vya rushwa, hatua za kisheria kuchunguza na kuendesha mashtaka kwa watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa,” alisema.

Ili kufanikisha hayo, Hamduni alitoa wito kwa wananchi kutambua rushwa ni kosa la uhujumu uchumi na linaingia katika makosa ya jinai.

Aliwakumbusha kwamba dhamana ya uchaguzi ni kuamua kuchagua watu wanaopenda maendeleo au kuamua kuchagua umasikini, yaani watu waliotanguliza masilahi yao kwa kivuli cha rushwa.

­Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma, Joseph Mwaiselo alisema lengo la kudhibiti na kupamba na rushwa ni kuboresha utawala bora.

Alisema jamii ikichukia rushwa kutakuwa na ustawi katika maendeleo na utoaji haki kwa wananchi utaimarika.

“Tumejiimarisha kuongeza uelewa kwa wananchi, kubadilisha mitazamo, kutoa elimu watu watoe taarifa na wachukue hatua wanapoona vitendo vya rushwa katika jamii,” alisema.

Kwa mujibu wa Mwaiselo, dhana ya rushwa inatofautiana nchi na nchi lakini kwa muktadha wa Tanzania inatafsiriwa kwamba ni matumizi mabaya ya ofisi ya umma kwa manufaa binafsi.

Alisema wamezindua kampeni inayojulikana kama Takukuru Rafiki itakayosogeza ukaribu wao na wananchi ili kushiriki kikamili kuzuia vitendo vya rushwa.

Akizungumzia mapambano ya jumla ya rushwa, Mwaiselo alisema “miongoni mwa kesi 41 zilizokwenda mahakamani makosa ambayo yaliibuliwa na taafira za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), tumeshinda kesi 40.”

Mkurugenzi wa Uzuiaji Rushwa, Sabina Seja alisema ni matarajio yake jamii inaweza kukomesha kabisa vitendo vya rushwa kwa sababu hayo yote yanayotokea yapo katika mazingira yao.

Alisema wananchi wanapasa kuwa tayari kutoa taarifa na ushahidi mahakamani.

“Wananchi wanapotoa taarifa ni vyema wailinde, kwani taarifa za uchunguzi zinapotoka huwa zinapoteza ushahidi. Tusipopambana na rushwa kuna uwezekano wa kupata viongozi wasiowajibika na wasio na maadili,” alisema.

Alisisitiza watu wakuze uzalendo kwa nchi na mali za Taifa kuzuia ufujaji wa fedha za Serikali katika miradi ya maendeleo.

Katika kutekeleza majukumu, Takukuru mwaka 2014 na 2019 ilifanya uchambuzi na ufuatiliaji wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwaka 2020 ilifanya uchambuzi wa mfumo wa uendeshaji wa uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani katika kata yote ya uchaguzi Tanzania Bara.

Taasisi hiyo imesema katika chaguzi hizo, yalikuwapo malalamiko ya vitendo vya rushwa.

Imesema vihatarishi vya rushwa vilionekana wakati wa utangazaji wa majina na mipaka ya mitaa, vijiji na vitongoji.

Kipindi cha kujiandikisha, maandalizi ya orodha ya wapigakura na uteuzi wa wagombea katika nafasi mbalimbali.

Pia wakati wa kampeni za wagombea, upigaji kura na kutangaza matokeo.

Takukuru imesema matokeo ya uchambuzi huo yalionyesha uzingatiaji wa maadili ya uchaguzi na mwenendo wake, huku vitendo vya rushwa vikiongoza kwa asimilia 72.6.

Vilevile ripoti ya Takukuru ilibainisha maeneo kinara yenye ushawishi wa rushwa katika uchaguzi ni wakati wa uteuzi wa wagombea ngazi ya chama.

Mchakato wa ndani ya chama kutia nia, kuchukua fomu na ujazaji, mchujo, kura, kutangaza matokeo na kufanya uteuzi wa mgombea kwa tiketi ya chama.

Kipindi cha kampeni imeelezwa matumizi ya fedha hufanyika kwenye kampeni za uchaguzi ngazi ya chama, tume na mgombea.

Wakati wa upigaji kura ni katika usimamizi wa kura na upigaji kura, kuhesabu na kutoa matokeo, kujumlisha na kutangaza matokeo katika kuandaa takwimu za wapiga kura na kura.

Kuhusu kushughulikia malalamiko, imeelezwa ni fedha hutumika katika kuweka pingamizi, kushughulikia kura zenye mgogoro, kufungua na kuendesha kesi za uchaguzi na kukata rufaa.

Related Posts