TETESI ZA USAJILI BONGO: Onyango kupisha na Rashid Juma, Lusajo Kutimkia Pamba

BEKI raia wa Kenya, Joash Onyango, yupo kwenye hatua za mwisho kumalizana na Dodoma Jiji ili kuitumikia msimu ujao.

Onyango aliyewahi kucheza Simba, ni miongoni mwa wachezaji waliomaliza mikataba Singida Black Stars ambayo awali ilikuwa inatumia jina la Ihefu FC.

WINGA wa zamani wa Simba, Rashid Juma yupo kwenye hatua za mwisho kusaini mkataba wa kuitumikia Singida Black Stars (SBS).

Nyota huyo anakwenda Singida Black Stars akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na Mtibwa Sugar huku ikielezwa ni chaguo la Kocha Patrick Aussems ambao waliwahi kufanya kazi pamoja ndani ya Simba.

RELIANTS Lusajo yupo kwenye hatua za mwisho kukamilisha usajili wa kujiunga na Pamba ambayo imepanda daraja msimu huu.

Lusajo ambaye alikuwa akiitumikia Mashujaa msimu uliopita, atajiunga na timu hiyo akiwa mchezaji huru baada ya kumalizana na waajiri wake hao aliowatumikia msimu uliopita akitokea Namungo.

BEKI wa kulia wa Yanga Princess, Lucy Mwenda yupo kwenye mipango na Alliance Girls kwa ajili ya msimu ujao, akitajwa kutakiwa Jangwani.

Kocha wa timu hiyo, Ezekiel Chobanka inadaiwa kwamba amewaeleza viongozi wa klabu hiyo kuwa anahitaji beki aina yake.

SIMBA Queens na Yanga Princess zimeingia kwenye rada za kumuwania straika wa JKT Queens, Stumai Abdallah.

Straika huyo aliyemaliza msimu na mabao 18 akiwa kinara kwa JKT, bado ana mkataba wa miaka miwili na klabu yake lakini watani hao wameanza mazungumzo naye kuona namna ya kuipata saini yake.

NAHODHA wa Fountain Gate Princess, Aquila Gaspar anatajwa kuhitajika ndani ya kikosi cha JKT Queens.

Inaelezwa kwamba mchezaji huyo bado ana mkataba wa mwaka mmoja na klabu yake, lakini JKT Queens ipo tayari kuuvunja ili kupata saini yake.

YANGA Princess imeanza mazungumzo na kipa wa Amani Queens (sasa Mashujaa Queens), Asha Mrisho kwa ajili ya kumsajili msimu ujao ili kuboresha eneo hilo.

Kipa huyo wa timu ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’ msimu uliopita alikuwa akicheza kwa mkopo wa miezi sita akitokea katika kikosi cha JKT Queens.

Related Posts