Uongozi wa Yanga huenda ukaachana na beki wa kati wa kikosi hicho Mganda, Gift Fred, licha ya kubakisha mkataba wa miaka miwili.
Beki huyo aliyejiunga na Yanga Julai 7, mwaka jana akitokea SC Villa ya Uganda, inaelezwa anaweza kuvunjiwa mkataba uliosalia ambao utafikia tamati Juni 30, 2026 ili kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni ambao wamekuwa hawana nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.
Nahodha huyo wa zamani wa mabingwa wa Uganda, SC Villa amekuwa hana nafasi mbele ya mabeki wenzake wa kati akiwano Dickson Job, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na nahodha Bakar Mwamnyeto ambao wamekuwa wakipishana kikosini.
COASTAL Union imeanza mazungumzo ya kumpata aliyekuwa kocha msaidizi wa Dodoma Jiji, Kassim Liogope ambaye yupo huru. Coastal inaoongoza kumtaka kocha huyo ili akawe msaidizi wa Mkenya, David Ouma baada ya Fikiri Elias kujiunga na KenGold ya jijini Mbeya, japo Tabora United na Kagera Sugar pia zimeonyesha uhitaji wa kuisaka saini yake.
UONGOZI wa Mtibwa Sugar, unataka kumrejesha aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Swabri Aboubakar baada ya timu hiyo kushuka daraja. Swabri aliondolewa Desemba 29, mwaka jana, lakini mabosi wa timu hiyo wanafikiria kumrejesha wakiamini uamuzi walioufanya mwanzoni ulichangia kwa kiasi kikubwa kikosi hicho kufanya vibaya na kushuka.
UONGOZI wa timu ya Singida Black Stars, uko katika mazungumzo ya kuipata saini ya aliyekuwa winga wa Namungo, Hamad Rajabu Majimengi. Nyota huyo wa zamani wa JKU, Coastal Union na Ruvu Shooting, inaelezwa mabosi wa Singida wameanza mazungumzo ili aitumikie kwa msimu ujao, wakiamini uwezo wake utakuwa chachu ya kufanya vizuri zaidi.