Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku 98 kabla ya Msumbiji kufanya uchaguzi wake mkuu, Rais wa Taifa hilo, Filipe Nyusi amewashukuru Watanzania kwa ushirikiano mkubwa waliompa katika safari yake ya utawala wa miaka 10.
Rais Nyusi amesema hayo leo Jumatano, Julai 3, 2024, katika sehemu ya hotuba yake ya ufunguzi wa Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba, jijini Dar es Salaam.
“Kwa niaba ya familia yangu na yangu binafsi, napenda kuwashukuru Watanzania kwa kunikubali na kunisindikiza kwenye upendo wa vitendo katika safari tuliyoifanya ya kuongoza nchi ya mashujaa,” amesema.
Oktoba 9, 2024, Msumbiji itafanya uchaguzi wa urais, wabunge, wakuu wa mikoa na wawakilishi wa Bunge, huku Rais Nyusi akiwa anang’atuka kwenye nafasi hiyo, aliyoanza mwaka 2015. Tayari chama tawala cha Frelimo, kimempitisha Daniel Francisco Chapo kuwa mgombea wake wa urais.
Chapo ni Gavana wa Inhambane, Mkoa wa Kusini mwa Msumbiji. Ni mtangazaji wa zamani wa redio ambaye alizaliwa mwaka 1977. Anakuwa mgombea wa kwanza wa chama tawala aliyezaliwa baada ya uhuru wa nchi hiyo uliopatikana mwaka 1975.
Katika maelezo yake, Rais Nyusi amesema safari yake akiwa kiongozi mkuu wa nchi ilikiwa kubwa na ndefu, lakini alikuwa na watu wanaomlinda, wakiwemo Watanzania, huku akisema anafanya kama alivyofanya Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
“Kwa utii wa dhati kwa Katiba niliyoapa kuilinda na kuiheshimu sitagombea tena urais, kwa hiyo kama Mwalimu Nyerere alisema nitang’atuka,“ amesema Nyusi.
Amesema katika uongozi wake zimepita nyakati za kumbukumbu kubwa na za milele, bila misaada ya kueleweka ya fedha kutoka nje chini ya vimbunga na dhoruba nyingi na wakati huohuo wakiwa wanatafuta amani ndani ya nchi yao.
“Tumeendelea kupata msaada wa karibu wa Tanzania. Bila kusahau changamoto ya ugonjwa wa Korona (Uviko 19),” amesema Rais Nyusi mwenye umri wa miaka 65.
Amesema kwa mara nyingine damu za watu wa nchi hizi mbili— Tanzania na Msumbiji zimekuwa zinachanganyika, hivyo ni vyema kuendelea kuwalinda watoto, wazee, wanawake, wanaume wanaouawa kikatili na watu wenye msimamo mkali.
“Tulikuwa na nyakati za kusherehekea mafanikio, asante Tanzania, Mungu aibariki Tanzania na watu wake,” amesema Rais Nyusi, huku akishangiliwa na washiriki wa maonyesho hayo waliokuwapo akiwemo Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Katika salamu zake za kuaga, Rais Nyusi amemkumbuka Rais wa Awamu ya Tatu wa Tanzania, Hayati Benjamin Mkapa, huku akituma salamu zake za shukrani kupitia mjane wake, mama Anna Mkapa.
“Mama Mkapa nataka nikushukuru pia kwa sababu nilikuwa na Mkapa kama mlezi wangu, sherehe zangu zote za uapisho alikuja na alikuwa anakaa na rafiki yake Chisano (Joaquim- aliyekuwa Rais wa Msumbuji) wananiusia na karatasi zake alizokuwa akiandika vitu vidogovidogo ananikabidhi namshukuru sana kwa hili,” amesema Nyusi.
Pamoja na hayo, amezitaka nchi mbalimbali Afrika kuangalia namna inavyoweza kutumia vitu vilivyomo nchini kwao, ili kujiendeleza.
Amesema baadhi ya vitu vinavyoonekana kama matatizo ya vijana wetu kukosa baadhi ya vitu vinasababishwa na vita mbalimbali zinazoendekea duniani.
Licha ya kuonekana vita hizo ziko mbali, amesema zinasumbua baadhi ya nchi za Afrika, kwani baadhi ya maeneo wamekuwa wakitegemea wageni kuchukua baadhi ya vitu, ikiwemo madini kwenda kutengenezea nchini kwao.
“Sasa kama hawatengenezi na hawakujenga tuna matatizo, sasa lazima tujifunze vitu vyetu viwe vinafanyika huku kwetu,” amesema Nyusi.
Amesema ni wakati sasa vitendo vya ugaidi vyenye hadhi ya kimataifa vikazuiwa haraka na kupigwa vita kwa njia ya ushirikano, hasa kwa nchi zinazoshirikiana katika mipaka ya nchi kavu na baharini.
Awali, akimkaribisha Nyusi, Rais Samia amesema tayari kampuni 11 kutoka Tanzania zimeanza kunufaika na uuzaji wa biashara katika Soko Huru la Ukanda wa Afrika (AfCTA).
Kampuni hizo zimeanza kutumia fursa hiyo kwa kusafirisha bidhaa za kahawa, katani, viungo, karanga na tumbaku kwenda nchi mbalimbali Afrika, ikiwemo Nigeria Ghana, Algeria na Morocco.
“Serikali itaendelea kutatua changamoto za wafanyabiashara na kwa wizara milango iko wazi kusaidia wafanyabiashara,” amesema Samia.
Pia washiriki watumie fursa hiyo kujifunza na kujipanga kuhudumia masoko makubwa ya ndani kikanda na kimataifa, kufika Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) kujisajili, ili kutumia fursa ya kuuza bidhaa zao katika soko la AfCTA.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Tantrade, Latifa Hamis amesema zaidi ya Sh1 bilioni zimeokolewa kwa kuboresha mabanda matano ambayo awali walikuwa wanakodi vifaa vya kutengenezea baadhi ya mabanda.
Mabanda yaliyoboreshwa yamepewa majina ya marais wastaafu, ikiwemo la Ali Hassan Mwinyi, Jakaya Kikwete na Benjamin Mkapa.
Kabla ya kuanza kuzungumza, Rais Samia na mgeni wake, Rais Nyusi wametembelea mabanda mbalimbali na kujionea bidhaa zilizomo.