Watanzania wapewa mbinu kupata fursa za Kiswahili kimataifa

Dar es Salaam. Wataalamu wa lugha ya Kiswahili wamewataka Watanzania wenye uweledi katika taaluma ya Kiswahili kujisajili katika kanzi data ya Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) ili zinapotokea fursa mbalimbali zinazotokana na kukua kwa lugha hiyo iwe rahisi kuwafikia.

Fursa hizo ni pamoja na ufundishaji wa lugha hiyo katika nchi mbalimbali, Tafsiri na Ukalimani wa taarifa mbalimbali pamoja na uandishi wa vitabu kwa lugha, muziki na filamu pamoja uuzaji na machapisho yaliyoandikwa katika lugha hiyo.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano, Julai 3, 2024 na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Mbarouk katika kongamano la kitaaluma kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani Julai 7, lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Amesema wataalamu wote wa lugha hiyo wanapokuwa katika kanzi data inarahisisha hata balozi za Tanzania zilizopo katika nchi mbalimbali pale zinapotokea fursa.

Pia, ametoa wito kwa Watanzania kuzibaini na kuchangamkia fursa hizo zinazojitokeza katika nchi mbalimbali ulimwenguni.

 “Lugha ya Kiswahili inazidi kukua hadi sasa inakadiriwa kuwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 500 duniani kote, kutambuliwa kwa Kiswahili duniani kutaendelea kuzalisha fursa mbalimbali, tuzitumie,” amesema.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Anna Moise ambaye ni mfanyakazi kutoka Pan African Mobile Library aliyesema lugha ya Kiswahili ikitiliwa mkazo inaweza kuzalisha fursa kwa vijana wengi hivyo kupunguza changamoto ya ajira.

Akitola mfano wake anasema ameweza kuajiriwa na taasisi hiyo kwa sababu ya kuwa mtaalamu wa lugha ya Kiswahili.

Hivyo ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanawahimiza watoto kujifunza lugha ya Kiswahili kwa ufasaha ili kunufaika na fursa hizo.

Hata hivyo, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Bakita, Dk Seleman Sewangi amesema ili Watanzania kunufaika na fursa hizo za kimataifa haikwepeki kuwa mahiri wa lugha zaidi ya moja.

Sewangi amesema kuwa mahiri katika lugha ya Kiswahili pekee bila kujua lugha nyingine kunawasababishia Watanzania wengi kushindwa kunufaika na fursa hizo.

Akitolea mfano fani ya tafsiri na ukalimani au ujifunzaji wa lugha ya Kiswahili kwa wageni haziwezi kufikiwa kama mtu ana umahiri katika lugha moja pekee.

“Hivyo nitoe wito kwa wanataaluma wa Kiswahili wasibaki kujinoa katika Kiswahili pekee jifunzeni na lugha nyingine ili kama wazawa tunufaike na lugha yetu,” amesema.

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda amesema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Kiswahili wamekuwa wakihakikisha Kiswahili kinazidi kukua na kuenea zaidi duniani.

Amesema katika Balozi za Tanzania zilizopo nchi mbalimbali duniani kuna vituo maalumu ambavyo vimeanzishwa kwa ajili ya kufundisha lugha ya Kiswahili hivyo inasaidia katika kuongeza wataalamu wa lugha hiyo.

Naye Profesa Flora Maggie akimuakilisha Makamu Mkuu wa UDSM, amesema vyuo vikuu navyo vina wajibu wa kuhakikisha Kiswahili kinaendelea kukua zaidi.

Amesema moja ya jukumu lao ni kuhakikisha wanatengeneza wanataaluma mahiri wa lugha hiyo ili kufikia vigezo vya kimataifa.

Pia, amesema hamasa ya watu kujifunza lugha hiyo imeongezeka na hilo linajidhihirisha kupitia ongezeko la wanafunzi wanaodahiliwa kusoma lugha hiyo.

Ameongeza wao kama chuo kikuu wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha Kiswahili kinakua nje ya mipaka ya Tanzania kwa kuanzisha programu ya kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wanaotaka kujifunza lugha hiyo kutoka nchi mbalimbali za Afrika.

“Pia tumekuwa na programu ya kuweka unafuu wa ada kwa wanafunzi wa kutoka nje wanaokuja kujifunza Kiswahili hivyo kuwafanya kulipa kiwango sawa na wanafunzi wazawa,” amesema.

Related Posts