Aliyekamatwa kwa kuchoma picha ya Rais jela miaka mwili

Mbeya. Msanii wa sanaa ya uchoraji, Shadrack Chaula (24), aliyekamatwa kwa madai ya kuchoma picha ya Rais Samia Suluhu Hassan na kushtakiwa kwa kosa la kutoa taarifa za uongo, amehukumiwa kulipa faini ya Sh5 milioni au kifungo cha miaka miwili jela.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Shamla Shehagilo leo Julai 4, 2024 katika Mahakama ya Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya, baada ya mshtakiwa huyo, mkazi wa Kijiji cha Ntokela, wilayani humo, kukiri kosa hilo.

Baada ya kukiri kosa hilo, Hakimu Shehagilo alimtia hatiani Shadrack kwa kosa la kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii wa TikTok, ambalo ni kinyume cha sheria ya makosa ya mtandao kifungu cha 16.

Awali alisomewa shtaka hilo na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Rosemary Mgenije, aliyekuwa akisaidiana na Wakili Veronica Mtafya.

Alidai Juni 22, 2024, eneo Ntokela lililopo Kata ya Ndato, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, mshtakiwa alitenda kosa hilo kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii @jet.fightershop akiwa ameshika picha inayomwonyesha Rais Samia, akisema:

“Kwa kuwa umeshindwa kutetea Taifa lako lisiathirike na ushoga, hii video inakuhusu wewe na si mtu mwingine wakati ukijua taarifa hizo ni uongo na upotoshaji kwa jamii,” amedai Wakili Veronika.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, upande wa mashtaka ulidai ingawa hauna kumbukumbu ya makosa ya nyuma, uliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa, ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia ya kumdhalilisha Rais wa nchi.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo alipopewa nafasi ya kujitetea, amekaa kimya.

Akitoa huduma hiyo, Hakimu Shehagiro amesema anamhukumu kulipa faini ya Sh5 milioni au kutumikia kufungo cha miaka miwili jela. Hadi muda wa mahakama unamalizika alikuwa hajalipa faini, akapelekwa gerezani.

Kijana huyo aliingia matatani baada ya kujirekodi video fupi akitoa maneno makali dhidi ya Rais Samia na kisha kuchoma picha ya kiongozi huyo, kitendo ambacho kiliwaibua viongozi mbalimbali na watu wengine kupinga tabia hiyo.

Juni 30, mwaka huu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga alieleza kuhusu kukamatwa kwa kijana huyo, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera aliyetaka kijana huyo akamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa kuchoma picha ya Rais.

Akitoa maelekezo yake kwa Kamanda Kuzaga, Homera alieleza kusikitishwa na kitendo hicho ambacho ni kinyume na maadili ya Kitanzania, akaliagiza Jeshi la Polisi mkoani humo kumsaka kijana huyo na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria.

Julai 3, mwaka huu Kamanda Kuzaga alieleza Shadrack kushikiliwa na Polisi kwa kosa la kuchoma picha ya Rais Samia na kutoa maneno makali kupitia video fupi.

Shadrack alikamatwa Juni 30 na kuwekwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Wilaya ya Rungwe kwa siku tatu na kufikishwa mahakamani jana.

Related Posts