Dar es Salaam. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ametoa maagizo matano kwa Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), Mkama Bwire ikiwemo kushughulikia changamoto ya mishahara kwa wafanyakazi.
Mengine ni ukamikishaji wa ujenzi wa Ofisi ya Dawasa Kigamboni, kutafuta mambomba na kuwaunganishia maji wananchi, kuwapatia usafiri watumishi wa Kigamboni, kudhibiti upotevu wa maji na kutafuta wataalamu wa kuunganisha mita za maji.
Bwire amepokea maagizo hayo huku akisema anahitaji zaidi ushirikiano kutoka kwa watumishi wa taasisi hiyo.
“Bado naendelea kujifunza kwa watumishi wenzangu na Mheshimiwa Waziri nikuahidi kufanyia kazi maagizo yaliyotolewa na pale panapohitaji kufanyiwa maboresho tutafanya hivyo,” amesema.
Bwire aliyetambulishwa Kigamboni aliteuliwa jana Jumatano, Julai 4, 2024, kupitia kikao cha bodi ya taasisi hiyo, akishika mikoba ya Kiula Kingu ambaye pamoja na Shaban Mkwanywe, mkurugenzi wa uzalishaji na usambazaji maji, waliwekwa kando Juni 30, 2024 na Waziri Aweso akichunguzwa kwa kushindwa kuwajibika.
Waziri huyo aliyesema kwa kipindi ambacho Kingu amesimamishwa, Dawasa itakuwa chini ya Wizara ya Maji, leo Julai 4, 2024 amemtambulisha Bwire kwa wafanyakazi wa Dawasa akiwataka kumpatia ushirikiano kwa kuwa anaijua kazi yake.
“Nikusihi Bwire ukitaka kufanikiwa washike mkono wafanyakazi wako, ukitaka kukaa ofisini bila kuzunguka utaletewa taarifa za uongo. Na kuna watumishi hawapati stahiki zao pamoja na kwamba wanafanya kazi,” amesema.
Amesema katika taasisi hiyo kuna baadhi ya watumishi kwenye mikoa ya kihuduma wamepoteza kazi kwa sababu ya kupikiwa majungu na watendaji, hivyo amemtaka Bwire kuwasaidia kama anataka kustarehe kwenye nafasi hiyo mpya.
“Nahitaji mazingira mazuri kwa watumishi kama madai yake ya kufanyakazi apewe na muache visingizio. Na ukitaka kiongozi ufanikiwe wewe wajali watu wako, inakuwaje kiongozi unafurahia majungu, ni muhimu majungu na fitina mkaacha,” amesema.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri amemtaka kiongozi Bwire kwenda kusimamia nidhamu kwa watendaji huku akieleza baadhi wamekuwa waongo na hawawajibiki.
“Watendaji wanaongea uongo, nikuombe ukadhibiti jambo hili na nahitaji kuona watendaji wakichapa kazi kuwaletea wananchi maji na kuwaunganishia,” amesema.
Mwajuma amesema anahitaji taasisi hiyo ijitofautishe na taasisi zingine katika utoaji huduma, kwa kuwajibika pale wanapohitajika badala ya kuwadanganya watu kwani huduma ya maji haina mbadala.
“Wizara imeweka macho yake katika taasisi hii, mkafanye kazi kwa watendaji wazembe hatutakuwa na subira,” amesema.
Mjumbe wa Bodi ya Dawasa, Evarist Ndikilo akizungumza kwa niaba ya mwenyekiti wake Davis Mamunyange, amesema wamechoka kupokea kero nyingi kutoka kwa wananchi na watumishi kutoa lugha mbaya, hivyo watakuwa wakali.
“Hamuunganishi maji kwa watu, lakini baadhi ya mameneja hawajui mahitaji wala upotevu wa maji. Sisi kama bodi tutafanya kila lililo chini ya uwezo wetu ili wananchi wapate huduma ya maji,” amesema.
Amesema kutokana na changamoto hizo katika kikao kilichofanyika jana Jumatano wamekubaliana watakuwa wanafanya vikao vya mara kwa mara na mameneja wote wa Dawasa, kuwahoji kinachoendelea katika maeneo yao ili kujiridhisha kama wanajua wanachokifanya.
“Bodi tunahitaji kuona mapato mazuri, waziri hatutakuangusha. Tunahitaji kudhibiti changamoto hizi, waziri tunakuachia ushughulike na mambo ya kisera,” amesema Ndikilo.