Baba adaiwa kumbaka mtoto wake, kumpa ujauzito kisha atoweka

Morogoro. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linachunguza tukio la mkazi wa Kitongoji cha Mwidu, mkoani hapa, Azizi Hussein anayedaiwa kumbaka mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka 14 na kumpata ujauzito.

Tukio hilo linadaiwa kutokea mapema Januari 2024 na Jeshi la Polisi limeanza kuchunguza kitendo hicho cha mtuhumiwa kuzini na maharimu wake, jambo ambalo ni kinyume na sheria na maadili ya Kitanzania.

Akizungumza na Mwananchi leo Juni 4, 2024 mjini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema baba huyo amezini na mtoto wake wa kike, kisha kutoroka na Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka ili afikishwe mahakamani.

 “Tayari shauri limefunguliwa Kituo cha Polisi Mikese kwa namba 229/2024 la kuzini na maharimu na upelelezi umeanza,” amesema Kamanda Mkama.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Tomondo, Kornelly Mkombo amesema familia ya Azizi Hussein ilifika ofisi za kata hiyo ili ipewe ushauri, lakini yeye aliwaelekeza kwenye Kituo cha Polisi kwa kuwa  matukio ya jinai yanatakiwa kuripotiwa huko.

“Kesi za kubakwa huwa zinaripotiwa polisi, sio ofisi ya mtendaji kata, hiyo kesi imeripotiwa huko na inaendelea. Kwangu walifika kupata ushauri na niliwaongoza kituoni,” amesema Mkombo.

Akisimulia mkasa huo, mwathirika wa tukio hilo (jina limehifadhiwa), amesema Januari mosi, 2024, saa 3 usiku, baba yake aliingia chumba cha watoto ambacho alikuwa amelala yeye na kumuamsha akiwa usingizini na kumbaka kwa nguvu na vitisho.

“Niliandaa chakula siku ya tukio na tunakaenda kulala na ilipofika saa 3 usiku, baba aliingia chumbani kwetu moja kwa moja na kuniamsha, akanieleza nikae naye na nisipokaa naye, mama na mimi tutakufa,” amesema msichana huyo.

Ameongeza kuwa baba yake alimweleza akiendelea kukataa, atawaua wote. Amesema aliendelea kukataa, ndipo baba yake akatumia nguvu kumwingilia hadi kumpa ujauzito.

“Baba aliniingilia kwa kunibaka na nilipata maumivu makali, nikapata ujauzito ambao ulitoka ukiwa na umri wa miezi mitatu. Lilikuwa ni tukio la kulazimishwa lililoambatana na vitisho kuwa nisipolala naye, ataniua mimi na mama. Niliogopa sana, akaniambia nisimwambie mama tendo lililofanyika,” amesema msichana huyo, amesema binti huyo ambaye amehitimu elimu ya msingi mwaka 2023.

Ameiomba jamii, taasisi na mashirika kumsaidia kutoka kijijini hapo ili ajifunze ufundi wa kushona nguo.

Mama mdogo wa msichana huyo, Aziza Ramadhani amesema msichana huyo alikutwa na ukatili huo mama yake akiwa amesafiri kwa siku kadhaa.

“Ni aibu tumeipata familia na ukoo, namna jamii inavyotutazama kwa ukatili uliofanywa na shemeji yangu, kwa kweli ametuvua nguo kwa kumwingilia mtoto wake wa kumzaa na kumpa ujauzito, ni tukio la aibu kwetu,” amesema Aziza.

Aziza amesema baada ya dada yake, Khadija Ahmad kurudi safari aliona tafauti kwa binti yake, hali iliyomshtua na kuanza kumuuliza maswali ndipo alisema haoni hedhi.

“Baada ya kujua siri imefichuka, Azizi aliandika talaka kumuacha mke wake na kutoroka kusikojulika baada ya kuuza shamba na alifanikiwa kutoroka.

Aziza amesema hilo sio tukio la kwanza kwa shemeji yake kuhusishwa na ukatili wa kingono kwani amewahi kudaiwa kumbaka shemeji yake na kumpa ujauzito na mtoto amezaliwa.

Katibu wa Kituo cha Taarifa na Maarifa chini ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), kata ya Tomondo, Doris Richard amesema uongozi wa kituo hicho baada ya kupata taarifa za tukio hilo walimfuatilia msichana huyo na kupata ukweli.

Doris amesema kituo hicho kimebaini ukatili dhidi ya mtoto huyo siku chache kabla mimba haijaharibika na walichangishana fedha kunusuru maisha ya msichana huyo mdogo.

Related Posts