Chuo hiki chazindua sherehe za miaka 60 ya kuanzishwa kwake

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dr. Hashil Abdallah, amezindua sherehe za miaka 60 ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) katika kampasi kuu ya CBE, Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo Dr. Hashil alitoa pongezi kwa CBE kwa mafanikio yake tangu kuanzishwa mwaka 1965 na kusisitiza umuhimu wa chuo hicho katika kutoa elimu bora ya biashara na kuandaa wataalamu wenye ujuzi. Pia, aliipongeza dira ya “CBE Vision 2074” inayolenga maendeleo ya teknolojia, utandawazi, na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi huku akisisitiza umuhimu wa taasisi za elimu kubuni mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa Chuo hicho, Prof. Wineaster Anderson, alieleza kuwa CBE imepiga hatua kubwa katika kutoa elimu ya biashara, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu tangu kuanzishwa kwake kwa Sheria ya Bunge Namba 31 ya mwaka 1965. Alibainisha kuwa chuo kimepanua wigo wake kwa kufungua kampasi Dodoma, Mwanza, na Mbeya.
Prof. Anderson alibainisha kuwa CBE imeimarisha miundombinu, rasilimali watu na uwezo wa kifedha. Chuo kimeanzisha miradi ya uwekezaji kwa ushirikiano na sekta binafsi ili kuongeza mapato na kuimarisha maendeleo ya kitaaluma na miundombinu.

Naye Mkuu wa Chuo, Prof. Edda Tandi Lwoga, alielezea historia na mafanikio ya CBE tangu kuanzishwa kwake mwaka 1965 na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Alisema CBE inajivunia kuwa na kampasi nne nchini Tanzania na kutoa elimu bora kwa wanafunzi zaidi ya 19,000. Prof. Lwoga alibainisha kuwa CBE imepanua programu zake hadi zaidi ya 22 mwaka 2024, ikijumuisha Biashara, Uhasibu, Masoko, Manunuzi na Ugavi, TEHAMA, na nyinginezo. Pia alitambulisha Dira ya miaka 50 ya CBE, “CBE Vision 2074,” inayolenga maendeleo endelevu kupitia teknolojia mpya na tafiti za kina.

CBE kilizinduliwa rasmi tarehe 21 Januari 1965 na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kikiwa na kampasi moja ya Dar es Salaam.

Sherehe za miaka 60 zitahitimishwa tarehe 21 Januari, 2025, na zitajumuisha matukio mbalimbali yatakayoadhimisha mafanikio ya CBE na mchango wake katika jamii na taifa kwa ujumla.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “MIAKA 60 YA UKUAJI, MABADILIKO NA UBORA

.
.
.
.

Related Posts