DC SAME AWAONYA WAFUGAJI WANAOHUJUMU SKIMU ZA UMWAGILIAJI.

NA WILLIUM PAUL, SAME. 

MKUU wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni amewatahadharisha wafugaji wanao hujumu miundombibumu kwa kuingiza mifugo kwenye maeneo ya Skimu za umwagiliaji za Ndungu na Kihurio kuacha mara moja. 

Aidha amewaagiza Viongozi wa Skimu na Serikali kwenye maeneo hayo lazima kuwe na usimamizi mzuri wa sheria na taratibu zote zinazohusiana na wafugaji kukiuka taratibu na kuamua kuingiza mifugo ili kumaliza hiyo migogoro pamoja na kuokoa fedha ambazo Serikali imewekeza kuwa na tija kwa Wakulima.

Ameyasema hayo kwenye mwendelezo wa ziara zake kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi ambapo akiwa katika Skimu ya Ndungu na Kihurio miongoni mwa changamoto zilizoelezwa na Wakulima wa Skimu hizo ni pamoja na uwepo wa baadhi ya wafugaji wanaokiuka miongozo ya kisheria ikiwemo mpango wa matumizi bora ya ardhi.

“SITAKI kuona Mifugo ya aina yeyote ile kwenye Skimu za umwagiliaji wanaharibu miundombinu ya Skimu zetu, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza fedha nyingi kwenye Skimu hizi mbili na Kata ya Ndungu na Kihurio ni mongoni mwa maeneo ambayo tayari Serikali imefanya mpango wa matumizi bora ya ardhi” Alisema Kasilda. 

Na kuongeza ” Ni vyema kuanzaia sasa kila kundi lifuate utaratibu uliopo kisheria kwa kufanya shughuli zake kwenye eneo lake husika, sipo tayari kuona fedha za zilizoletwa na Mama Samia zinapotea kwasababu Wakulima au Wafugaji wameshindwa kufuata utaratibu uliowekwa na Serikali”.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya amewaonya baadhi ya watu wanaopotosha Wakazi wa Kata ya Kihurio na Ndungu juu ya utekeleaji wa mradi wa ukarabati wa Skimu za umwagilijai Ndungu na Kihurio kufuatia mradi huo kuchelewa kuanza utekelezaji wake kwa mujibu wa mkataba ambapo mkandarasi alitakiwa kuanza kazi hiyo Juni 01, 2024.

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imetoa kiasi cha shilingi bilioni 7 kwaajili ya ukarabati wa miundombinu ya Skimu hizo, mradi ambao kwamujibu wa mkataba utatekelezwa na Kampuni mbili za wazawa ambazo ni Hamieri Tanzania Ltd na Ansil Tanzania Ltd ambapo zitafanya kazi hiyo kwa muda wa mwaka mmoja na nusu.

Amewatoa hofu wananchi kuwa hakuna mabadiliko yeyote ya matumizi ya fedha hizo Serikali inakamilisha taratibu za malipo ya mkandarasi ili aje eneo la mradi kuanza kazi na wananchi watapewa taarifa sahihi kutoka kwa Serikali yao pindi utekelezaji utakapoanza rasmi.

Related Posts