HOFU kubwa ya mashabiki wa soka mkoani Geita ilikuwa ni hatma ya Geita Gold baada ya kushuka daraja kutoka Ligi Kuu kama Halmashauri ya mji huo itaendelea kuimiliki na kushiriki Championship, lakini wameshushwa presha kwani uongozi umekubali na sasa mipango imeanza kusukwa.
Timu hiyo ilishuka daraja msimu ulioisha na sasa inajiandaa kushiriki Ligi ya Championship msimu ujao kusaka nafasi ya kurejea Ligi Kuu, huku ikiondokewa na mastaa wake mbalimbali wa kikosi cha kwanza ambao wanasaka malisho kwingine.
Akizungumza na Mwanaspoti, ofisa habari wa klabu hiyo, Samwel Dida, alisema uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Geita chini ya Mkurugenzi, Yefred Myenzi umekubali na kutoa ruhusa ya timu hiyo kujiandaa na Ligi ya Championship huku ukitenga bajeti kubwa ya kuirejesha Ligi Kuu.
Alisema kulikuwa na ukimya wakisubiria kauli ya mkurugenzi huyo kama wanaitema timu na halmashauri kujikita kwenye mambo mengine, lakini sasa wamepata uhakika na kwamba vikao vya mwisho kupitisha bajeti ya takribani Sh400 milioni vikitarajiwa kumalizika wiki hii.
“Jambo la kwanza lilikuwa ni mkurugenzi kuridhia. Sasa kama ameridhia mambo na mipango inaanza, bado vitu vichache vinawekwa sawa wiki hii tutakuwa tumepata mwanga,” alisema Dida na kuongeza;
“Mpaka sasa matarajio yalikuwa ni bodi ya klabu kutenga karibu Sh400 milioni za kushiriki Championship na habari njema ni kwamba mdhamini wetu (GGML) ameahidi kuweka nguvu kwenye usajili na mishahara.
“Kwa hiyo tutakuja na kikosi bora kwenye Ligi ya Championship tutafanya pia usajili wa kimataifa.”