Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amevitaka vyombo vya habari kujikita katika kutoa habari zinazowahusu wananchi zaidi badala ya viongozi.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, hivi sasa kumejitokeza baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vimegeuka kuwa vya propaganda.
Jaji Warioba aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, amesema chombo chochote cha habari kina sera ya chumba cha habari lakini pamoja na kuwapo, kazi yao kubwa ni kuhabarisha wananchi.
Amesema hayo leo Alhamisi Julai 4, 2024 alipozindua ripoti ya utafiti wa hali ya mwenendo wa vyombo vya habari kwa mwaka 2022/23 iliyoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
“Sasa sijui hii ndiyo sera ya chumba cha habari, inakuwa kama tunakwenda katika propaganda au kwa lugha ya kizazi cha sasa uchawa,” amesema Jaji Warioba akiibua kicheko kwa wadau wa habari walioshiriki uzinduzi huo.
Amesema zamani ukishika gazeti utakuta habari yenye utafiti uliowagusa wananchi, hivi sasa hakuna kutokana na alichoeleza ni woga.
Jaji Warioba ameitaka MCT kuweka mkazo katika suala hilo, kwa kuwa haitasaidia kama kutabaki kuwa na vyombo vya habari vya ‘uchawa’.
“Sijui chawa wa Serikali, chawa upinzani, hapana wananchi wanataka habari za kila aina ili wazitumie,” amesema.
Amesema kwa kawaida asubuhi huwa anasikiliza redio kujua vichwa vya habari vya magazeti, kwa nyakati tofauti habari nyingi hasa za ukurasa wa mbele zinazoandikwa zinawahusu viongozi na siyo wananchi.
Jaji Warioba amesema kumekuwa na woga kuanzia vyombo vya habari, viongozi hadi wananchi.
Amesema baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumteua katika Kamati ya Haki Jinai, alichukua muda kusoma ripoti za tume ya haki jinai na kubaini baadhi ya sababu zinazofanya baadhi ya taasisi za haki jinai zisifanye kazi ni kukosa ushirikiano na wananchi.
“Wananchi hawana ushirikiano na taasisi hizi kwa sababu ya woga. Mfano vyombo vya haki jinai vinatafuta habari, lakini mwananchi anazo na anaogopa kuwapa, wanasema wakiwaambia watapata madhara,” amesema.
Jaji Warioba amesema, “Kwa viongozi woga ndiyo mkubwa zaidi, unakuta ni rahisi kusifu tena imekuwa ni fasheni, lakini kukosoa kumekuwa na woga. Katika nchi hii kiongozi yeyote anayesimama hazungumzii sentensi mbili bila kumtaja Rais.”
Amesema kuna siku alikuwa akifuatilia Bunge, kila mbunge aliyesimama alikuwa anamtaja Rais, lakini mambo mengi wawakilishi hao wa wananchi wanasita kusema.
“Mara nyingi huwa nazungumza na wenzangu kuhusu hali ya nchi ipoje, lakini utakuta mtu anakueleza vizuri ukimwambia mbona haya husemi… anasema aah! nikisema sitaeleweka. Namwambia mbona mimi nakuelewa,” amesema Jaji Warioba.
Katibu Mtendaji wa MCT, Ernest Sungura amesema ripoti hiyo imeangazia maeneo tisa, yakiwamo mafunzo ya uandishi wa habari na weledi, usawa wa kijinsia, watu wenye ulemavu, sheria, sera na mazingira wanayofanyia kazi wanahabari.
“Ripoti imeibani bado kuna changamoto ya wanawake kupata usawa katika habari hasa Zanzibar, ingawa Tanzania Bara kumekuwa na maendelea kidogo. Ripoti imeonyesha hali ya vyombo vya habari bado ni ngumu,” amesema.
Sungura amesema ripoti ya utafiti imebaini wanafunzi wanaotoka vyuo vikuu na kwenda kwenye vyombo vya habari wanashindwa kufanya kazi kwa tija zaidi.
“Mapendekezo ni kwa wahariri wa vyombo vya habari wajitahidi kuwapa malezi bora ili kuendana na mazingira yatakayowasaidia kufanya kazi inayostahili,” amesema.
Mjumbe wa Bodi ya MCT, Dk Joyce Bazira ameipongeza taasisi hiyo, akisema ripoti ya utafiti itawezesha na kutumika kama vyanzo vya habari katika vyuo na ushawishi katika kuleta mabadiliko kwa tasnia ya habari.
Akizungumza wakati wa uwasilishaji ripoti hiyo, mwanahabari mkongwe, Neville Meena amesema licha ya uzuri wa ripoti hiyo, angetamani utafiti uzungumzie hali ya usalama wa waandishi wa habari wanapokuwa katika maeneo ya kazi.
“Hii ingetusaidia na ni muhimu hasa tunapoelekea katika uchaguzi ujao ukiwamo wa mwaka 2025, kwa sababu nyakati hizi ni ngumu ambazo vyombo vya habari vinapitia. Uchaguzi una masilahi kwa watu wengi, kwa wanasiasa kwa pande zote,” amesema.