Huku idadi ya vifo ikiongezeka na mazingira yakizidi kuwa mabaya kwa Wagaza, pande zote mbili zinakabiliwa na shinikizo linaloongezeka la kimataifa kufikia mapatano ya kusitisha vita, kwa msingi wa mpanago uliopendekezwa na Rais wa Marekani Joe Biden.
Hamas imesema katika taarifa iliyotolewa Jumatano jioni kuwa kiongozi wake wa kisiasa aliepo nchini Qatar Ismail Haniyeh, alifanya mawasiliano na wapatanishi nchini Qatar na Misri kuhusu mawazo ambayo vuguvugu hilo linajadaliana nao kwa lengo la kufikia makubaliano, na kuongeza kuwa mawasiliano hayo pia yalifanyika kati ya mkuu huyo wa vuguvugu na maafisa nchini Uturuki.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na idara ya ujasusi ya nchi hiyo, Mossad, zilithibitisha mkakati huo mpya mara moja katika taarifa iliyosema Israel ilikuwa inatathmini msimamo wa Hamas na kwamba itatoa jibu lake kwa wapatanishi.
Kwa mujibu wa chanzo chenye ufahamu kuhusu mazungumzo hayo, Waqatari, kwa uratibu na Marekani, wamekuwa wakishirikiana na Hamas na Israel katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita kujaribu kuziba mapengo yaliyosalia.
Biden alisema mpango aliopendekeza Mei 31 ulianzia Israeli, na unajumuisha usitishaji vita wa wiki sita, kubadilishana mateka na wafungwa na ujenzi mpya wa Gaza.
Mpasuko kati ya jeshi la Netanyahu
Gazeti la New York Times liliripoti kuwa majenerali wakuu wa Israel wanataka kusitishwa vita Gaza hata kama hii itaibakisha Hamas madarakani kwa wakati huu, na hivyo kuongeza mpasuko kati ya jeshi na Netanyahu, ambaye amepinga makubaliano yoyote yanayoiacha Hamas kuendelea kutawala Gaza.
Soma pia: Israel: Hatutaiacha Rafah ikiwa na miundombinu thabiti
Makamanda hao wanaamini kusitishwa vita itakuwa njia bora zaidi ya kuachiliwa huru kwa mateka waliosalia Gaza, na wanafikiri vikosi vya Israel vilivyochoka na vinavyokabiliwa na uhaba wa silaha, vinahitaji kujipanga upya iwapo vita vikubwa zaidi vitazuka na kundi la Hezbollah la nchini Lebanon, inasema ripoti hiyo ikiwanukuu maafisa sita wa usalama wa sasa na wa zamani wa Israeli.
Shambulizi la Israel siku ya Jumatano lilimuua kamanda wa juu wa Hezbollah Mohammed Nasser kusini mwa Lebanon, ambapo kundi hilo lilijibu mauaji hayo kwa kufyatua mkururo wa maroketi kusini mwa Israel na kusababisha moto mkubwa.
Ndani ya Gaza kwenyewe, maafisa wa afya wameripti kuwa watu wasiopungua 12 wameuawa katika mashambulizi ya Israel katikati na kaskazini mwa ukanda huo.
Vikosi vya Israel vilifanya pia mashambulizi mapya kusini mwa Gaza, katikati mwa mapigano makali na wapiganaji wa Kipalestina usiku wa kuamkia leo, ambapo jeshi hilo limeripoti kuuawa kwa Kapteni wake mwenye umri wa miaka 21 katika mapambano Kaskazini mwa Gaza.
Shambulizi la Israel pia liliharibu shule ya Umoja wa Mataifa mjini Khan Younis, kusini mwa Gaza, ambako Wapalestina waliokosa makaazi wanajihifadhi. Hata hivyo hakukuwa na taarifa zozote za vifo au majeruhi.
Chanzo: Mshirika