Kanuni kutambua makazi nje ya hoteli kwa watalii zaandaliwa

Unguja. Baada ya kuwapo makazi holela ya watalii wanaofikia kwenye nyumba binafsi, Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kwa kushirikiana na Kamisheni ya Utalii Zanzibar, imeweka kanuni za makazi kwa watalii wasiofikia hotelini ambazo zitatumika kwa watoa huduma wa makazi hayo.

Akitangaza kanuni hizo katika mkutano wa wadau wa utalii Julai 4, 2024, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mudrick Ramadhani Soraga amesema kanuni hizo zitamtaka mtoa huduma anayemiliki makazi hayo kuomba usajili kutoka Kamisheni ya Utalii.

“Huduma hizi zinatumika kwa wazawa na diaspora, ili kupata leseni Kamisheni ya Utalii itafanya ukaguzi wa makazi kuhakikisha kiwango cha biashara hiyo kinakidhi mahitaji,” amesema.

Waziri Soraga amesema mchakato wa usajili wa leseni utagharimu Sh150,000 kwa Mkoa wa Mjini Magharibi na mikoa mingine itagharimu Sh250,000.

Kifungu cha 31(1) cha Sheria ya Utalii ya Zanzibar namba sita ya mwaka 2009 imempa mamlaka waziri kutunga kanuni hizo.

Sambamba na hayo amesema Kamisheni inaweza kusitisha leseni ikigundulika imetumika kwa taarifa za ulaghai, kuendeshwa kwa shughuli zilizokatazwa na kanuni hiyo na kukiuka vigezo na masharti ya leseni hiyo.

“Ikithibitika mtu yeyote ametenda kosa na kutiwa hatiani atalipa faini ya Dola za Marekani zisizopungua 1,000 sawa na Sh2.6 milioni na isiyozidi Dola 5,000 sawa na Sh13.2 milioni au kifungo kisichopungua miezi mitatu hadi miaka mitano,” amesema Soraga.

Hata hivyo, amesema si maeneo yote ambayo yameridhiwa kwa ajili ya biashara hiyo.

Kwa Mkoa wa Mjini Magharibi, maeneo yaliyoridhiwa ni Mji Mkongwe, Mlandege, Fumba, Bububu, Chukwani na Mbweni.

Katibu Mtendaji Kamisheni ya Utalii, Hafsa Hassan Mbamba amesema wapo baadhi ya watalii ambao wanahitaji kujitegemea ndiyo sababu ya kuanzisha kanuni hiyo.

Amesema mkutano huo umewasaidia kugundua baadhi ya changamoto wanazokutana nazo wadau utalii kisiwani Pemba, ikiwemo miundombinu ya barabara inayosababisha kutokufikika kwenye hoteli.

Amefafanua alichokiona ni kuwa kisiwani Pemba wadau hao hawana taasisi ya pamoja inayoweza kuwasilisha changamoto na mapendekezo yao katika kamisheni hiyo.

“Tumeshauri wadau kuweka taasisi ya pamoja kwani mtu yeyote anayetaka kuanzisha biashara katika Kamisheni lazima ajumuike katika taasisi husika na ndiyo sababu ya kuwataka wao kuanzisha yao,  ili iwasaidie kuwasilisha changamoto zao,” amesema. Mshauri wa jumuiya ya wawekezaji, Masoud Salim Mohamed.

Ameongeza kuwa jambo hilo ni zuri kwani linatoa fursa kwa wazawa kushiriki moja kwa moja katika sekta ya utalii.

Amesema kinachowavutia watalii kufika visiwani humo ni amani, hivyo uwepo wa kanuni hizo utawajengea usalama wa kuishi katika nyumba hizo.

Pia amewataka watu ambao wanataka kuwekeza katika biashara hiyo wasiziogope kanuni hizo kwani zinawafanya kutambulika kihalali.

Related Posts