KESI YA UKAHABA: Mahakama yaamuru washtakiwa watano wakamatwe

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive jijini Dar es Salaam imeamuru washtakiwa watano kati ya 18 katika kesi ya ukahaba wakamatwe kwa kosa la kuruka dhamana.

Amri hiyo imetolewa leo Alhamisi, Julai 4, 2024 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo maarufu Mahakama ya Jiji, Lugano Kasebele kufuatia maombi yaliyotolewa na upande wa mashtaka, baada washtakiwa hao kushindwa kufika mahakamani kusikiliza kesi yao hiyo.

Washtakiwa hao ni Aisha Iddi, Sabrina Gabriel, Recho Kindole, Diana David na Zainabu Hamis.

Mbali na hao, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Amina Ramadhani, Mariana Sia, Mwajuma Hamza na Mariamu Hassan.

Vilevile kuna Najma Hamisi Mariam Kitamoga Elizabeth Michael, Rosemary John, Lobi Daudi,  Jackline Daniel, Mwajuma Bakari, Jenifa John,  Recho Bakari.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka moja la kufanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa ajili ya kufanya umalaya kinyume na kifungu cha 176 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 Marejeo ya mwaka 2022.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo Juni 14, 2024 maeneo ya Sinza Mori, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam. Wanadaiwa kusimama hadharani wakiwa wamevaa mavazi yasiyo ya heshima kwa lengo la kufanya umalaya.

Kesi hiyo imetajwa leo Alhamisi, Julai 4, 2024 mahakamani hapo kwa lengo la kupangiwa tarehe ya usikilizwaji wa awali, ambapo watasomewa maelezo ya awali ya kesi inayowakabili.

Hata hivyo, mpaka saa nne wakati kesi hiyo ilipoitwa washtakiwa watano, ambao pamoja na wenzao wako nje kwa dhamana ya fedha taslimu Sh300, 000 kila mmoja, walikuwa hawajafika mahakamani bila taarifa.

Kutoka na hali hiyo upande wa mashtaka uliowakilishwa na mawakili wa Serikali Winfrida Ouko na Regina Kayuni, ukaiomba mahakama itoea amri ya kuwakamata washtakiwa hao kwa kuruka dhamana na mahakama ikakubalina na maombi hayo.

“Kwa washtakiwa ambao hawapo, mahakama hii inatoa amri ya kuwakamata kama ambavyo upande wa mashtaka umeomba ili liwe fundisho kwa wengine kuheshimu amri ya mahakama,” amesema Hakimu Kasebele.

Kesi hiyo itaendelea Julai 10, 2024 kwa ajili ya usikilizwaji wa awali na itasikilizwa na hakimu mkazi Francis Mhina baada ya Janeth Mgaya aliyeisikiliza awali kujiondoa.

Hakimu Mgaya alijiondoa katika kesi hiyo Juni 26, 2024, baada ya washtakiwa hao kumkataa.

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Juni 24, 2024 na Juni 25, 2024, washtakiwa hao kupitia kwa wakili wao Peter Madeleka walimwandikia barua ya Hakimu Mgaya kumtaka ajiondoe katika kesi yao.

Hivyo wakati kesi hiyo ilipoitwa Juni 26, 2024 wakili Madeleka alimweleza hakimu huyo kuwa wamemwandikia barua ya kumtaka ajitoe na aache kusikiliza kesi hiyo ili haki iweze kutendeka.

Madeleka alidai wateja wake walifikia uamuzi huo kwa kuwa hakimu huyo ni mkali, anawafokea mawakili na washtakiwa wenyewe kama watoto na kwamba alikuwa anaonyesha kuegemea upande mmoja.

Akitoa uamuzi wa kujitoa Hakimu Mgaya alisema jukumu la utawala ni kuwa mtu anayetenda haki na haoni shida kutokuendelea na kesi hiyo kwa sababu hana haja ya kuendelea na watu wasiofuata utaratibu wa kisheria.

Hivyo alitangaza kurudisha jalada la kesi hiyo kwa mfawidhi kwa ajili ya kupangiwa hakimu mwingine.

Waendesha mashtaka matatani

Katika kesi nyingine inayowakabili washtakiwa watano kwa tuhuma hizo za ukahaba, mahakama hiyo inatarajia kutoa uamuzi wake Jumatatu, dhidi ya waendesha mashtaka kwa kupuuza amri yake.

Amri hiyo inahusu kuwasilisha uthibitisho wa ugonjwa wa mmoja wa mashahidi wake ambaye alishindwa kutoa ushahidi mara mbili mfululizo ikidaiwa alikuwa mgonjwa.

Taarifa ya ugonjwa wa shahidi huyo ulipingwa na mawakili wa utetezi, Madeleka, Jebra Kambole na Maria Mushi ambao walitaka upande wa mashtaka uwasilishe mahakamani vyeti vya matibabu ya shahidi huyo kuthibitisha kweli alikuwa anaumwa.

Mahakama ilikubaliana na hoja ya mawakili wa utetezi na kuuelekeza upande wa mashtaka kuwasilisha mahakamani uthibitisho huo, lakini upande wa mashtaka haukutekeleza amri hiyo.

Badala yake jana, Jumatano baada ya shahidi huyo kutoa ushahidi wake, upande wa mashtaka ulidai hauna uthibitisho huo na kwamba si wajibu wao, bali ni wajibu wa shahidi ambaye alipaswa kufanya hivyo juzi (Jumanne) alipofika mahakamani kutoa ushahidi wake.

Mahakama haikukubaliana na utetezi huo ikisema wao ndio walikuwa wakimwakilisha shahidi huyo na kutokutekeleza amri hiyo ni kupuuza amri ya Mahakama.

Hivyo Hakimu Kasebele anayesikiliza kesi hiyo hakutaka kuendelea na ushahidi wa shahidi aliyekuwa ameandaliwa, badala yake aliiahirisha kwa ajili ya kuandika uamuzi wa Mahakama kutokana kwa upande wa mashtaka kushindwa kutekelea amri hiyo, ambao alipanga kuutoa Jumatatu, Julai 8, 2024.

Katika kesi hiyo pia washtakiwa wanakabiliwa na shtaka moja la kufanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa ajili ya kufanya umalaya kinyume na kifungu cha 176 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 Marejeo ya mwaka 2022.

Washtakiwa ni Mariam Yusufu Mkinde (250 mkazi wa Magomeni, Mwazani Nassoro (25) mkazi wa Kigogo, Mwanaidi Salum (25) mkazi wa Mabibo, Faudhia Hassan (35) mkazi wa Ubungo na Tatu Omary (40) mkazi wa Ubungo.

Wanadaiwa kukutwa wakifanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa kusimama hadharani, wakiwa wamevaa mavazi yasiyo ya heshima kwa lengo la kufanya umalay maeneo ya Manzese Tip Top.

Related Posts