Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imeitahadharisha Jamhuri kutokana na kukwamisha usikilizwaji wa awali wa kesi inayomkabili mfanyabiashara na mwanasiasa, Boniface Jacob na mwenzake, mwanaharakati Godlisten Malisa, ikisema inatoa ahirisho la mwisho.
Jacob, maarufu Boni Yai, mkazi wa Mbezi Msakuzi, Dar es Salaam na Malisa, mkazi wa Moshi, mkoani Kilimanjaro wanakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 11805/2024, wanadaiwa kuchapisha taarifa za uongo katika mitandao ya kijamii, kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka wanadaiwa kutoa taarifa za uchochezi kuwa Jeshi la Polisi linaua raia, wakilihusisha na kifo cha mwananchi mmoja, Robert Mushi, maarufu Baba G.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo, ilipangwa leo Alhamisi Julai 4, 2024 kwa ajili ya usikilizwaji wa awali, ambapo washtakiwa wangesomewa maelezo ya awali ya kesi.
Hata hivyo, imekwama kuendelea kutokana na upande wa mashtaka katika kesi hiyo kutokuwa tayari, hii ikiwa ni mara ya tatu inaahirishwa kwa sababu hizo.
Kesi hiyo ilipoitwa, mwendesha mashtaka, wakili wa Serikali Frank Rimoyi ameieleza mahakama kuwa hawana jalada la kesi hiyo na kwamba limeitwa kwa ajili ya kufanyiwa marejeo, bila kubainisha limeitwa na nani. Hivyo, ameiomba mahakama iahirishe na iwapangie tarehe nyingine.
Akijibu hoja hiyo, wakili wa utetezi, Peter Kibatala amesema leo ni mara ya tatu kesi hiyo inaahirishwa kwa sababu hizohizo za upande wa mashtaka.
Kibatala amesema mwaka 2022 Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) ilifanyiwa marekebisho ikaweka sharti kwamba kwa kesi ambazo si kubwa kama hiyo inayowakabili washtakiwa hao, hazipaswi kupelekwa mahakamani kabla ya taratibu zote kukamilika.
“Hii inaonesha walipeleka mahakamani kwa kuharakisha kabla ya mambo kukamilika. Wao ndio walisema tangu siku ya kwanza upelelezi umekamilika na wakaomba tarehe ya PH (usikilizwaji wa awali),” amesema Kibatala.
“Kwa hiyo sisi tunaona hii ni kukiuka taratibu za kisheria na kuichosha mahakama. Kama mahakama yako ikiridhia kuahirishwa, basi iweke wazi kuwa ni ahirisho la mwisho na siku nyingine ikija kama wakishindwa kuendelea nitaomba chini kifungu cha 226 ifutwe kwani watakuwa wameshindwa kuendesha kesi.”
Mahakama imekubaliana na hoja za utetezi kuwa ni mara ya tatu kesi hiyo kuahirishwa katika hatua hiyo, hivyo ikatoa ahirisho la mwisho Julai 30, 2024.
“Mahakama imekubalia maombi ya upande wa mashtaka na kesi hii inaahirishwa mpaka Julai 30. Lakini hili ni ahirisho la mwisho. Kama upande wa mashtaka utashindwa kuendesha kesi yake kwa tarehe hiyo basi mahakama itatoa uamuzi kulingana na mazingira,” amesema Hakimu Swallo.
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Mei 6, 2024 na kusomewa mashtaka matatu, mawili kati ya hayo yanamkabili Jacob pekee yake na Malisa anakabiliwa na shtaka moja.
Shtaka la kwanza linalomkabili Jacob pekee ni la kuchapisha taarifa za uongo kinyume na sheria, akidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 22, 2024 jijiini Dar es Salaam.
Anadaiwa kuwa, alichapisha taarifa katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa Kijamii X (Twitter) wenye jina la Boniface Jacob @ExMayor Ubungo, inayosomeka:
“Wenye leseni ya kuua wameua tena. kijana wetu Robert Mlanga Mushi maarufu kama Babu G amekutwa Hospitali ya Kilwa Road akiwa ameuawa.
Shtaka la pili, ambalo pia linamkabili Jacob pia ni kuchapisha taarifa za uongo, akidaiwa kutenda kosa hilo Machi 19, 2024 katika jiji la Dar es Salaam.
Anadaiwa kuwa alichapisha taarifa katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa Kijamii X (zamani Twitter) kuwa “Mauaji Arusha, Mwananchi mwenzetu na aliyekuwa dereva wa magari ya watalii, Omari Msamo ameuawa na askari wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.
Shtaka la tatu ambalo pia ni la kutoa taarifa za uongo, linalomkabili Malisa pekee yake, akidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 22, 2024 katika jiji la Dar es Salaam.
Malisa anadaiwa siku hiyo ya tukio, alichapisha taarifa ya uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa Kijamii wa Instagram kuwa:
“Tarehe 13 Aprili meya mstaafu wa Manispaa ya Ubungo @Exmyor_bonifacejacob alitoa taarifa ya kupotelewa na ndugu yake Robert Mushi maarufu kama Babu G, ambaye alipotea mapema mwezi Aprili 2024.
Inadaiwa alikamatwa na watu waliojitambulisha kuwa polisi maeneo ya Kariakoo na baada ya hapo hawakuonekana tena….leo wakaambiwa “nendeni Hospitali ya Polisi Kilwa Road, ndugu yenu amefichwa mochwari pale” wakaenda.
La haula! Wakamkuta Robert akiwa kwenye jokofu la baridi. Hakuwa Robert tena bali ni mwili wake ukiwa na majeraha ya kipigo. Ni mauaji ya kikatili. Masikini Robert hajawahi kuwa na ugomvi na mtu kwanini utendewe haya.” mwisho wa maelezo hayo.