Dar es Salaam. Siku 12 tangu alipopotea na baadaye kupatikana akiwa na majeraha, Edgar Mwakabela ‘Sativa’, Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) imeibuka na kuzungumzia sakata hilo huku ukishauri vijana kusimama kwenye misingi ya kidemokrasia na kujadiliana kwa hoja.
Katibu Mkuu wa umoja huo, Jokate Mwegelo amesema kujadiliana kwa hoja ndio msingi wa demokrasia na kunawaweka watu pamoja.
“Serikali imeruhusu mijadala na mikutano ya hadhara, ni vema tuwe tunajadiliana kwa hoja, na vijana tuishi humo,” amesema Jokate leo Alhamisi Julai 4, 2024 alipokuwa akizungumzia uzinduzi wa kampeni ya vijana itakayofanyika Julai 6, 2024 jijini Dar es Salaam.
Jokate amegusia suala la Sativa aliyetoweka Juni 23 jijini Dar es Salaam na kupatikana Juni 27 kwenye Hifadhi ya Katavi akiwa na majeraha katika mwili wake.
Sativa anayeendelea na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, usiku wa kuamkia jana Jumatano, alifanyiwa upasuaji wa taya la kushoto lililosagika baada ya kudaiwa kupigwa risisa alipotekwa na watu wasiojulikana.
“Ni kijana mwenzetu, suala lake tunafarijika kuona Rais Samia amechangia,” amesema Jokate bila kutaka kuingia kwa undani.
Rais Samia Suluhu Hassan, Julai 2, 2024 alikuwa miongoni mwa waliojitokeza kuchangia Sh35 milioni za matibabu ya Sativa.
Hata hivyo, mchango huo ulikosolewa na mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, kuwa hakutakiwa kutoa mchango wa matibabu ya mtu aliyetekwa, bali aagize vyombo vyake vya ulinzi na usalama kuwakamata watekaji na waliotekwa wapatikane.
Kwenye mkutano wake leo na waandishi wa habari uliolenga kuzungumzia uzinduzi wa kampeni ya vijana, Jokate amemshukuru Rais Samia kwa mchango wake huo.
“Tunamshukuru Rais kwa kujitoa kwake kugharamia matibabu ya Sativa, tunaendelea kufarijika kama vijana kwa kuwa yule ni kijana mwenzetu.
“Pia tunashukuru kwa kauli ya Waziri Masauni ya kuanza kulifuatilia suala hilo na kuchukua hatua stahiki kwa watakaogundulika,” amesema Jokate, akiwasisitiza vijana kuwa kipindi hiki ni cha majaribio makubwa, hivyo yataibuka mengi.
“Tuhakikishe tunaiacha Tanzania salama, tusisitize umoja na mshikamo, tunawasihi vijana wenzetu tuishi humo,” amesema.
Hata hivyo, alipoulizwa kwanini UVCCM imezungumzia suala la Sativa mara baada ya Rais kuchangia matibabu yake, Jokate amesema hawezi kulizungumzia hilo.
Jana Jumatano, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni alizungumzia uhalifu wa utekaji watu kuwa haupaswi kukaliwa kimya.
Amesema uhalifu huo kwa sasa umekuwa gumzo na baadhi ya wanasiasa wanaufanyia siasa.
Mbali na hilo, Masauni amesema kibaya zaidi uhalifu huo unahishwa na vyombo vilivyopewa dhamana ya kulinda watu kwa maana Jeshi la Polisi au Serikali.
“Uhalifu huu unahusishwa na wanasiasa na Serikali na kuna Gazeti moja la Mwananchi limeandika suala hili pia kuna maswali ni mengi ya nani mtekaji, nihakikishe tu Tanzania iko salama,” amesema.
Katika hatua nyingine, Jokate amezungumzia kampeni itakayozinduliwa Julai 6, 2024 na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi ambayo inalenga kujadili fursa mbalimbali zilizotengenezwa na zinazotengenezwa kwa vijana katika awamu ya sita.
“Uzinduzi utafanyika uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa moja asubuhi,” amesema.
Amesema kampeni hiyo itawahamasisha vijana kushiriki shughuli za kisiasa kipindi hiki Taifa linapoelekea kwenye mchakato wa kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
“Pia itawahamasisha vijana kugombea kwenye uchaguzi wa serikali za mtaa mwaka huu na kutoa msisitizo kujiandikisha kwenye daftari la makazi,” amesema.