-Shirika la Swiss Aid Laitaja Tanzania kufanikiwa tofauti na nchi nyingine
Dodoma
Ujenzi wa Mifumo bora katika shughuli za Uchimbaji na Biashara ya Madini ikiwemo Sheria nzuri zinazofanyiwa maboresho mara kwa mara, Sera na Usimamizi endelevu, vimetajwa kuwa chachu ya udhibiti wa vitendo vya utoroshaji madini nchini hususan ya dhahabu.
Hayo yalibainishwa Julai 3, 2024 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo katika mahojiano maalum na runinga ya AZAM TV, kufuatia taarifa za utafiti mpya zilizotolewa na Shirika la Kimataifa la Swiss Aid kuitaja Tanzania kama nchi iliyofanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti vitendo vya utoroshaji madini hususan dhahabu ikilinganishwa na nchi nyingine.
Kwa mujibu wa utafiti huo, zaidi ya tani moja hutoroshwa kila siku kutoka mataifa yenye utajiri mkubwa wa madini dhahabu Barani Afrika, huku zaidi ya nusu ya dhahabu inayouzwa kimagendo inatokana na shughuli za uchimbaji mdogo.
Aidha, utafiti huo pia ulionesha kwamba mwaka 2022 pekee dhahabu ya kiasi cha tani 435 zenye thamani ya zaidi ya Dola bilioni 30 zilitoroshwa kupelekewa katika mataifa ya Emirates, Uswis na India.
Pia, Mbibo aliongeza kwamba, sababu nyingine iliyopelekea Tanzania kuwa kinara katika eneo hilo ni kutokana na uwepo wa masoko ya madini na vituo vidogo vya ununuzi wa madini ambavyo vimepelekea kurahisisha biashara ya madini, kuwepo kwa uwazi katika masoko hayo, uhakika wa masoko kwa wachimbaji pamoja na uwepo wa bei elekezi.
‘’ Hivi sasa tuna jumla ya masoko 42 na vituo vidogo 100 vya ununuzi wa madini nchi nzima, suala ambalo limerahihisha kwa kiasi kikubwa biashara ya madini kwa wachimbaji wadogo. Serikali ilifikia uamuzi huu baada ya kufanya utafiti na kubainika kwamba ukosefu wa sehemu za kuuzia madini kwa wachimbaji wadogo unasababisha uwepo wa vitendo vya utoroshaji madini,’’ alisema Mbibo.
Pia, Mbibo alizitaja sababu nyingine ni mazingira wezeshi kwenye biashara ya madini katika kila hatua hadi kumfikia mlaji wa mwisho, uwepo wa kikosi maalum cha udhibiti wa vitendo vya utoroshaji madini kinachofanya kazi nchi nzima pamoja na ukaguzi wa mara kwa mara.
Alisema sababu nyingine ni kutokana na kurasimishwa kwa shughuli za uchimbaji mdogo, utoaji wa elimu endelevu na uhamasishaji wa umma na wadau pamoja na Serikali kuwa mbia na mwezeshaji wa wachimbaji wadogo kupitia huduma za uchorongaji zinazotolewa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na huduma za uchenjuaji kupitia vituo vya mfano.
Vilevile, alisema utaratibu uliowekwa wa Wizara kukutanana kuzungumza na wadau kupitia makundi mbalimbali hatua ambayo kusaidia kujadili changamoto na kutafuta suluhu ya changamoto hizo kwa lengo la kuendelea kuweka mazingira bora ya shughuli za uchimbaji na biashara ya madini.
Akizungumzia mikakati ya kuendeleza Sekta na kuendelea kudhibiti vitendo hivyo, Mbibo alieleza kuhusu mpango wa Serikali kurejesha minada ya madini ya vito na maonesho ya madini ya vito ambayo yatatoa nafasi ya wanunuzi na wauzaji kufanya biashara.
‘’ Hapa Afrika hakuna sehemu inayoendesha minada ya madini isipokuwa kwa Asia na Ulaya, sisi tunataka kurejesha majukwaa haya ya watu kuuza na kununua na hatimaye kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha madini,’’ alisema Mbibo.
Nchini Tanzania, dhahabu inatajwa kuchangia asilimia 80 ya mapato yote ya madini yanayozalishwa kwa sasa nchini.