SIMBA inaendelea kusajili majembe mapya, ikiwamo jana kumtambulisha Abdulrazak Hamza kutoka Cape Town City ya Afrika Kusini sambamba na mrithi wa Clatous Chama, nyota kutoka Ivory Coast, Ahoua Jean Charles na sasa inapambana kushusha beki wa kuziba nafasi ya Henock Inonga aliyetua FAR Rabat ya Morocco.
Mezani kwa mabosi wa Simba ina majina manne ya nyota wa kigeni, mbali na kuwatambulisha wazawa, Lameck Lawi kutoka Coastal Union na Abdulrazak Hamza aliyewahi kukipiga KMC na Namungo akitokea Afrika Kusini.
Licha ya kupata mkwanja mrefu kwa kumuuza Inonga, Simba inaamini inahitaji beki mwingine atakayekuwa na ubora kama wa Inonga au zaidi ili kufiti moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha Wanalunyasi na kutoa ushindani kwa Che Malone Fondoh na Hussein Kazi atakaowakuta.
Majina ya mabeki wa kigeni yaliyopo mezani kwa Simba sasa ni Muivory Coast Anthony Tra Bi Tra aliyemaliza mkataba na Asec Mimosas, Wakongomani Magloire Ntambwe kutoka TP Mazembe na Fasika Idumba kutoa Cape Town City ya Sauzi na Chamou Karaboue kutoka Racing Club ya kwao Ivory Coast.
Uongozi wa Simba umeamua kutuliza vichwa katika maamuzi ya mwisho nani apewe mkataba kati ya wanne hao kwani kila mmoja tayari wamewasiliana naye na kuzungumzia dili hiyo na kukubaliana na kilichobaki ni Simba kuamua imsainishe nani.
Moja ya viongozi wanaohusika moja kwa moja na usajili wa Simba aliliambia Mwanaspoti kupata changamoto kwenye eneo la beki, lakini wako makini na kabla ya kusafiri kwenda Misri kwa ajili ya kambi maamuzi yatakuwa yamefanyika.
“Tuna mabeki zaidi ya watano, wapo ambao tumewasajili wengine tupo kwenye mazungumzo. Wapo ambao wapo wageni hapa nchini tayari, lakini hawajasaini mkataba na wengine tunawasiliana nao kwa mtandao,” alisema kigogo huyo na kuongeza;
“Hatutaki kufanya makosa kwenye eneo hili. ni eneo nyeti na ukizingatia aliyeondoka (Inonga), alikuwa bora hivyo bado tunawafanyia tathmini na mwisho wa siku kabla ya kambi kuanza tutakuwa tumeamua nani asaini.”
Hata hivyo, Mwanaspoti, limepenyezewa Simba inataka beki ambaye atakuwa na umri mdogo, pia kutokuwa na majeraha ya mara kwa mara huku nidhamu na unafuu wa gharama zikiwa sifa nyingine inazozingatia na Fasika amepewa nafasi kubwa mbele ya Tra Bi Tra na Karoboue.
Wakati mchujo huo wa kimya kimya ukiendelea kwa vigogo wa Simba, gazeti hili linajua Simba itatambulisha mmoja kati ya mabeki hao na itasafiri naye hadi mjini Ismailia kwa maandalizi ya kambi rasmi.
Hadi tunaingia mitamboni, Simba ilikuwa imetambulisha wachezaji wapya watano, Lawi, Hamza, Winga Mzambia Joshua Mutale, Straika Mganda Stephen Mukwala na Kiungo mshambuliaji anayechukua nafasi ya Chama, MVP Ahoua Jean Charles kutoka Ivory Coast, huku Elie Mpanzu ikielezwa huenda akatambulishwa leo.
Simba pia imewapa ‘Thank You’ wachezaji saba, Saido Ntibazonkiza, Shaaban Chilunda, Keneddy Juma, John Bocco, Luis Miquisson, Inonga na Clatous Chama.
Licha ya kwamba Simba ilifanya siri juu ya usajili wa Abdulrazak, lakini baada ya Mwanaspoti kunasa na kudokeza kwenye kurasa za tetesi za Bongo, jana mabosi wa klabu hiyo walimtambulisha rasmi.
Beki huyo wa zamani wa KMC, Mbeya City, Namungo amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Simba na muda wowote kuanzia sasa atatangazwa kama mchezaji wa timu hiyo.
Mtoa taarifa huyo alibainisha sababu za Simba kumuhitaji zaidi Abdurazack ni kwa ajili ya kuwa mbadala wa Kennedy, akiwa pia na uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo kwa ufasaha kama alivyoku beki huyo wa zamani wa Singida United aliyepewa ‘thank you’ sambamba na nyota wengine sita wa Msimbazi.
“Ujio wa mchezaji huyo tuna inani utakuwa na namna nzuri na kutoa mwanya kwa Che Malon kupata muda wa kupumzika kwani aina ya uchezaji wake na uzoefu alionao utaweza kuwa chachu ndani ya eneo hilo pia limekuwa likitumia wachezaji wa aina moja mara kwa mara.” alisema mtoa taarifa huyo.
Mwanaspoti lilipokibana chanzo hicho juu ya dili la beki huyo wa kati mzawa wakati tayari wamemtangaza Lameck Lawi na bado wana Hussein Kazi mtoa taarifa huyo, alisema timu hiyo ina michuano mingi hivyo wanasajili kikosi ambacho kitakuwa kipana huku akisisitiza kuwa suala la Lawi pia ndio limewapa msukumo wa kumsajili Abdulrazak.
“Ishu ya Lawi ina mkanganyiko Coastal wao pia bado wanasema ni wao na sisi tuna thibitisha kuwa ni mchezaji wetu, hivyo wakati hili tunaendelea nalo tumeamua kupata mchezaji ambaye ataanza moja kwa moja na timu wakati changamoto iliyopo baina yetu na timu ya Tanga tunaifanyia kazi,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Sakata la Lawi tutalipambania hadi mwisho hadi kufikishana FIFA kwani haiwezekani mchezaji akasajiliwa na kuamua kurejesha fedha wakati tayari kamwaga wino kwenye mkataba ili kuhakikisha timu inaendelea kujiweka tayari na hakuna mchezaji anaachwa nyuma ndio sababu ya kuongezwa kwa Abdulrazak,” kilisema chanzo hicho. mwenye miaka 21.”