VIGOGO vya soka nchini, Simba, Yanga na Azam FC vipo bize kushusha na kutambulisha mashine mpya kwa ajili ya msimu utakaoanza Agosti, kiasi huko mtaani na kwenye mitandao ya kijamii mashabiki na wapenzi wanatambiana.
Wale wa Yanga wanawatania Simba wakiwatisha eti labda wasipeleke timu uwanjani kwani badala ya kupigwa 7-2 kama msimu uliopita, safari hii huenda wakala nyingi zaidi, huku wale wa Msimbazi wakisema wamefanya usafi na moto utawaka kwani Mnyama ana hasirai.
Mashabiki wa Simba na Yanga wameibua tambo hizo kutokana na majina ya wachezaji waliotambulishwa na wale wanaotajwa kuwa mbioni kukamilisha dili kabla ya kutambulishwa wakati timu hizo nyingine za Ligi Kuu Bara ikiwamo Azam zikijiandaa kwa kambi.
Msimu uliopita, Yanga iliyotetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa tatu mfululizo, iliitambia Simba kwa kuinyoa mabao 5-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza, kisha kuifumua 2-1 ziliporudiana, huku Yanga na Azam zikigawana pointi tatu kila moja baada ya kila timu kushinda mechi moja. Yanga ilianza kwa ushindi wa mabao 3-2 kisha ikazimwa na Azam 2-1, ilihali Simba na Azam, ya kwanza iliisha kwa sare ya 1-1 jijini Mwanza na ziliporudiana Simba ilishinda 3-0, hivyo kwa sajili zinazofanyika zimekuwa zikitumiwa na mashabiki na wapenzi kutambiana.
Mwanaspoti linakuletea vikosi na maingizo yanayoenda kuboresha timu hizo kabla ya kuanza vita ya kusaka ubingwa wa Ngao ya Jamii sambamba na Coastal Union, kisha Ligi Kuu Bara na michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) mbali na ile ya CAF.
Kwa namna kila ilivyojipanga kuboresha kuelekea msimu huo mpya, lakini hesabu zikiwa kwa timu tatu kubwa Yanga, Simba na Azam, zimeshtua vikali na ni kama kila moja ikisema ‘labda msilete timu’.
Tuanze na watetezi, Yanga ambao hajaitaka kufanya makubwa, lakini kuna mashine nne muhimu imeziongeza katika kikosi, huku ikipigania saini za watu wawili wengine wanakuja.
Yanga imewaongeza beki Chadrack Boka kutoka FC Lupopo ya DR Congo atakayetua kabla ya wiki hii kumalizika akiwa ndiye mashine pekee iliyoongezwa katika ukuta ambao ndio ulikuwa imara msimu uliopita ukiruhusu mabao 14 kwenye mechi 30 Ligi Kuu Bara.
Mbali na Boka, Yanga pia imemuongeza kipa Abubakar Komeni ambaye hata hivyo hawezi kumuondoa Djigui Diarra kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Ukuta wa Yanga utakuwa na Diarra, kulia Yao Kouassi ambaye hakuna anayeweza kumng’oa wakati kushoto atasimama Boka ilhali mabeki wa kati wakiwa nahodha msaidizi Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ huku nahodha mkuu Bakari Mwamnyeto akisubiri. Safu ya kiungo itakuwa na mashine tano ambapo viungo wa chini wanaweza kuwa Khalid Aucho aliyeongeza mkataba na Maxi Nzengeli ambaye amekuwa na ukabaji mkubwa lakini akizunguka eneo kubwa.
Juu ya wawili hao kutakuwa na mafundi watatu ambao lazima wakunyime usingizi kama unakwenda kukutana nao Pacome Zouzoua kulia, Stephanie Aziz KI na kushoto atakuwa mtu hatari mmoja Clatous Chama aliyetua kutoka Msimbazi, ambaye jana alitoa ‘thank you’ kwa mashabiki na wadau wa Simba.
Safu ya ushambuliaji ataanza ‘Mwana Mfalme’ Prince Dube aliyesajiliwa baada ya kutemana na Azam FC, huku nje akiwasubirisha Clement Mzize na Jonathan Sowah ambaye saini yake inapiganiwa.
Kwenye benchi lao kocha Miguel Gamondi ataamua mwenyewe nani asubiri hapa lakini kuna watu wa maana wengi wakiwemo makipa Aboutwalib Mshery, Komeni, Mwamnyeto, Mzize, Jonas Mkude, Nickson Kibabage, Mudathir Yahya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Sowah kama sio Guede Joseph.
Washindi wa pili wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, Azam FC hawana moto mdogo kwani wameongeza mashine mpya tano na kati ya hizo nne zitaingia moja kwa moja kikosi cha kwanza cha matajiri hao wanaolisaka taji la pili la Ligi Kuu.
Katika ukuta ikifanikiwa kujimilikisha kipa Msudani Mohammed Mustapha aliyekuwa akiitumikia kwa mkopo kutoka Al Merrikh ya Sudan na sasa atakuwa mali kamili ya matajiri hao wa Chamazi.
Mabeki wa pembeni kama kawaida watakuwa Lusajo Mwaikenda kulia kama sio Nathaniel Chilambo, huku kushoto Pascal Msindo ambao ni zao la timu ya vijana ilhali mabeki wa kati wakiwa ni Mcolombia Yeison Fuentes atakayecheza na ingizo jipya Yoro Diaby kutoka Mali.
Safu ya kiungo itakuwa na watu watano, lakini sura moja itakuwa mpya ambapo viungo wa chini watakuwa Yahya Zayd na Ever Meza Mcolombia mwingine aliyesajiliwa dirisha hili. Juu ya hao kutakuwa na ingizo jipya lingine winga wa kulia Franck Tiesse kutoka Ivory Coast aliyekuja kuchukua nafasi Kipre Junior aliyeuzwa USM Alger ya Algeria.
Wengine ni mfungaji bora wa timu hiyo msimu uliopita, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na winga wa kushoto, Gibril Sillah huku juu ya kutakuwa na mshambuliaji mpya Mcolombia wa tatu ndani ya timu hiyo, Jhonier Blanco.
Benchi la matajiri hao linashtua kwani kuna watu wa kazi kipa wao Zuber Foba, Chilambo kama hataanzishwa kikosi cha kwanza, Sospeter Bajana, Idd Seleman ‘Nado’, Abdul Seleman ‘Sopu’, James Akaminko, Yannick Bangala na mshambuliaji mpya Nassor Saadun ambao kocha Yusuf Dabo ataamua nani aingie kumbadilishia mchezo.
Simba ni kama imeamua kuvua gamba ikizaliwa upya baada ya kufanya usajili wa nguvu uliosimamiwa na tajiri Mohammed ‘Mo’ Dewji aliyerejea akiendelea kumuamini Salim Mhene Try Again na Crescentius Magori aliyerudishwa kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya Wekundu wa Msimbazi.
Jeshi la Simba linaweza kuanza na sura mpya nane ambapo lango litaendelea kulindwa na kipa Mmorocco Ayoub Lakred, beki wa kulia akiendelea mkongwe Shomari Kapombe kama sio Israel Mwenda, ilhali kushoto atakuwa ingizo jipya Valentin Nouma, huku mabeki wa kati wakiwa Che Malone na Fasika Idumba ambaye mabosi wanaendelea kupigania saini yake.
Viungo kutakuwa na watu watano ambapo wawili wa chini watakuwa wote wapya Deborah Fernandez na Augustine Okejepha raia wa Nigeria aliyesajiliwa hivi karibuni.
Juu ya hao wawili kutakuwa na winga Mzambia Joshua Mutale kulia huku kushoto atakuwapo Mkongomani Elie Mpanzu, katikati yao kutakuwa na fundi Jean Charles Ohoua aliyebakiza siku chache kusajiliwa kuchukua nafasi ya Chama, ilhali mshambuliaji wa juu akiwa Mganda mpya Steven Mukwala. Benchi la Wekundu nalo si mchezo kwani kocha mpya wa kikosi hicho kutoka Sauzi ataumiza kichwa akiwa na watu kama kipa Ally Salim, Israel Mwenda kama hataanza kikosi cha kwanza, Fabrice Ngoma, Mzamiru Yassin, Freddy Kouablan, Kibu Denis, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Edwin Balua na Ladack Chasambi.
Beki na kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema bado anasubiri kuona ukamilifu wa mchakato wa usajili wa timu zote, lakini kwa Simba inahitaji kusubiri zaidi kuona makali ya wachezaji waliowasajili a kuunda upya kikosi cha timu hiyo.
Kocha wa zamani wa timu hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alisema: “Simba inahitaji wachezaji bora ambao watakwenda kurudisha hadhi ya kikosi..”