WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro amethibitisha kwamba Serikali imeanza mchakato wa kuwezesha ujenzi wa uwanja wa gofu katika jiji la Mwanza ili liendane na hadhi ya majiji mengine duniani kwani mchezo huo huvutia utalii wa michezo.
Akizungumza jana jijini hapa, Dk Ndumbaro alisema ameshafanya mazungumzo na wataalam kutoka PGA Legend Golf Tour ambao wameahidi kufika Mwanza kukagua eneo utakapojengwa, huku akiwaelekea viongozi wa mkoa huo kutenga eneo na kukutana na wataalam hao.
“Mwanza ni Jiji la pili kwa ukubwa Tanzania linastahili ubora, nimetembea duniani sijawahi kuona jiji ambalo halina kiwanja cha gofu. PGA Legend Golf Tour waliniambia wanataka kujenga uwanja mahususi wa gofu Zanzibar nikawaomba tujenge pia na Mwanza,” alisema Ndumbaro.
“Sasa kazi yako Mkuu wa Mkoa (Said Mtanda) nitakupa mawasiliano yao leo hii ili waje Tanzania waone hilo eneo watujengee uwanja wa gofu ili sifa ya Mwanza ikitaka kushindana na Dar es Salaam iwe katika kila kigezo. Na utaona gofu inaleta mashindano mengi makubwa na watalii wengi.
“Morogoro, Arusha na Moshi wana viwanja vya gofu haiwezekani watushinde, Mwanza inabidi ipate kimoja kizuri. Kwenye hili tutakuunganisha na hao wataalam na chama cha gofu Tanzania pamoja na baraza la michezo kuhakikisha kwamba tunafanikiwa,” alisema.
Alisema msimu ujao wa mashindano ya michezo ya shule za msingi (Umitashumta) na sekondari (Umisseta), Serikali imepanga kuuongeza mchezo wa gofu kwani mchezo huo na kikapu imekuwa ikiwasaidia wanafunzi kupata ufadhili wa masomo nje ya nchi na kuendeleza vipaji vyao katika ligi kubwa duniani ikiwemo Marekani.
“Vyuo vya Marekani vinachukua watoto wenye vipaji vya gofu na kikapu na kuwasomesha kwahiyo kipaji chako kinaweza kukupeleka mbali. Tumekuwa tukipoteza huo ufadhili kwenye gofu kwa sababu hatuna miundombinu.”