Dodoma. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) imeanza kuchapa upya vitambulisho vilivyochapishwa chini ya kiwango, hivyo imewataka wenye navyo kuviwasilisha katika ofisi zake zilizo karibu nao vichapwe upya.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Julai 4, 2024 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Nida, Geofrey Tengeneza alipozungumza na Mwananchi.
Amesema hatua hiyo imetokana na malalamiko kutoka kwa wananchi wa mikoa mbalimbali kuhusu ubora hafifu wa baadhi ya vitambulisho hivyo.
“Tumekuwa tukipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro Dar es Salaam na mingine, kuwa vitambulisho walivyopewa vimefutika picha na majina,” amesema.
Baada ya kufanya utafiti na kubaini ukweli juu ya changamoto hiyo na Nida imeamua kuvikusanya kutoka kwa wananchi ili kuvichapisha upya.
“Napenda kuchukua nafasi hii kuujulisha umma wa Watanzania kwamba yoyote mwenye kitambulisho kilichofutika picha na maandishi akirejeshe kwenye ofisi za kata yake, au ofisi za Nida zilizopo karibu naye ili achapiwe kipya ndani ya muda mfupi,” amesema.
Kwa mujibu wa Tengeneza, mamlaka hiyo imejipanga kuhakikisha shughuli hiyo inafanyika kwa weledi na ubora ili wananchi wapate vitambulisho ndani ya wiki mbili.
Akizungumzia jinsi tatizo lilivyotokea, amesema “ili kwenda na kasi ya uhitaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi, tulilazimika kuchapisha vingi sana ndani ya muda mfupi, suala ambalo lilisababisha baadhi ya vitambulisho kuchapishwa chini ya kiwango,” amesema.
Amesema mpaka sasa, mamlaka hiyo imechapisha na kutoa vitambulisho kwa asilimia kubwa ya Watanzania na kazi bado inaendelea kuwafikia wachache waliosalia.
“Kimsingi, takwimu zetu zinaonyesha kila Mtanzania aliyeomba kupatiwa kitambulisho cha Taifa na aliyekidhi vigezo vilivyowekwa na Serikali ameshachapishiwa kitambulisho chake,” amesema.
Hata hivyo, Tengeneza amesema changamoto iliyopo hivi sasa ni kwamba watu wengi, hususan mijini, hawajaenda kuchukua vitambulisho vyao, hali ambayo inasababisha mlundikano wa vitambulisho kwenye vituo.
Mmoja wa wakazi wa Nkuhungu, Amina Juma amepongeza hatua hiyo kwa sababu vitambulisho vya awali vilikuwa havionyeshi vizuri picha na hivyo kuleta ugumu katika kutambua uhalali wa kitambulisho.
“Nimeshaona kwa watu wangu wa karibu karibia vitambulisho viwili picha haionekani vizuri na ikitokea ukatoa nakala, ndio kabisa inakuwa shida,” amesema Amina.
Septemba 6, 2023, Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Chilo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alisema bungeni kuwa hadi kufikia Julai 31, 2023 Watanzania 11,242,736 walikuwa wamepewa Vitambulisho vya Taifa.
Alisema idadi hiyo ni sawa na asilimia 55 ya lengo la kuwapatia vitambulisho watu 20,294,910 waliostahili kupewa.
Chilo alisema mpango wa Serikali ni kuwagawia vitambulisho Watanzania 9,052,174 waliobaki ifikapo Machi, 2024 na kuwa mipango yote ilikuwa imekamilika.