Tabora. Mkuu wa Wilaya ya Chato, Said Nkumba amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora kujaza nafasi ya Hassan Wakasuvi aliyefariki ghafla Februari 22, 2024.
Wakasuvu alifariki ofisini wakati akimsubiri Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Fadhil Maganya, aliyetarajiwa kufanya ziara siku hiyo katika Mkoa wa Tabora.
Kutokana na kifo hicho, nafasi ya mwenyekiti imekuwa wazi hadi walipofanya uchaguzi mdogo leo ili kujaza nafasi hiyo ambapo makada wengi walionyesha nia ya kugombea uenyekiti wa CCM Tabora.
Hata hivyo, wagombea watatu pekee ndiyo waliopitishwa na Kamati Kuu, ambao ni, mbunge wa zamani wa Tabora Kaskazini, Athuman Futakamba, aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, Saada Malunde pamoja na Nkumba.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi huo, Gilbert Sampa ambaye ni mjumbe wa halmashauri kuu ya Taifa ya CCM, amesema wapigakura kwenye uchaguzi huo walikuwa 1,119 na Nkumba ameibuka kidedea kwa kura 1,006.
Amesema Futakamba amepata kura 50 na Saada kura 63 huku kura 3 zikiharibika.
“Ndugu wajumbe, uchaguzi sasa umemalizika, nawaomba mkafanye kazi ya kukijenga chama na kuanzia sasa makundi ambayo yanakuwepo baada ya chaguzi muyaondoe, mshirikiane katika kuhakikisha chama kinapiga hatua kwenda mbele,” amesema.
Akizungumza baada ya matokeo hayo, Futakamba amewashukuru waliompigia kura na kuahidi kumpa ushirikiano mwenyekiti mpya.
“Nawashukuru Kamati Kuu ya CCM kwa jina langu kurudi, hii ni heshima kubwa kwangu na mkoa kwa ujumla, bado nipo kwa ajili ya chama, nimekuwa mkuu wa wilaya, naibu waziri, hivyo kama chama kikinihitaji, nitakuwa tayari kukitumikia,” amesema.
Kwa upande wake, Saada naye amewashukuru wajumbe ambapo amewataka waliokuwa wafuasi wake kuvunja makundi na kumuunga mkono aliyeshinda.
“Nimeridhika na namna uchaguzi ulivyoendeshwa, ulikuwa huru na haki na wagombea wote ni ndugu, hivyo baada ya uchaguzi huu tusitengane.
“Haitapendeza uchaguzi ukimalizika tushindwe hadi kusalimiana, hivyo tumpe ushirikiano mwenyekiti wetu ili chama kiendelee kuwaunganisha,” amesema kada huyo wa CCM.
Akizungumza baada ya ushindi huo, Nkumba amewashukuru viongozi ambao wamefanya kazi kubwa baada ya kuondoka kwa aliyekuwa mwenyekiti na kwamba kama wasingekaa vizuri chama kingepotea njia, lakini walibaki wamoja.
“Uchaguzi umemalizika na viongozi wamepatikana, kilichobaki ni kukipambania chama ili kishike dola,” amesema.
Nkumba ameongeza kuwa maisha yake ni ya kawaida na ataendelea kuishi hivyo na wanaodhani watakuwa marafiki zake baada ya kuchaguliwa wanakosea, kwa kuwa yeye atamthamini kila mmoja kwa kuwa ameshakuwa kiongozi wa wengi.
Anna Changau ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sikonge, amezungumza kwa niaba ya wenyeviti wa CCM wilaya za Tabora, akisema watamuunga mkono mwenyekiti wao aliyechaguliwa.