NA MWANDISHI WETU, MICHUZI TV
KATIKA kuunga jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia, Mama Lishe Zuwena Mohamed maarufu Shilole (Shishifood) ametangazwa kuwa balozi mpya wa kampuni ya Gesi ya Oryx kwaajili ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia mitungi ya gesi nchini.
Lengo la Oryx kumpa Ubalozi Shilole unalenga kuunga mkono juhudi za Rais Dk.Samia Suluhu ambaye ameweka malengo kuwa ifikapo mwaka 2032 asilimia 80 ya Watanzania iwe inatuminia nishati safi ya kupikia.
Akizungumza wakati wa tukio hilo lililofanyika Julai 4 kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba yanayofanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, Meneja Mauzo na Masoko wa Oryx Gas Shaban Fundi amesema wameamua kumchagua Shilole kwasababu ni miongoni mwa wadau wanaohamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema kupitia kwa Shilole wanaamini kuna wengine ambao walikuwa nyuma kwenye matumizi ya Nishati Safi ya kupikia kuendelea kutumia gesi za Oryx kupikia.
“Tunafamu Shilole amekuwa mjasiriamali maarufu machi, anamiliki migahawa ya Shishifood katika miji ya Dar es Salaam na Dodoma, amekuwa mama Lishe wa kisasa na muumini mzuri wa kutunza mazingira,hivyo Oryx tunaona fahari kumtangaza Shilole kuwa balozi wetu katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ili kwa pamoja kufikia malengo ya Rais Samia ya kuhamasisha nishati safi ya kupikia nchini.”
Kwa upande wake Shilole ambaye pia ni Msanii maarufu nchini,amesema yupo tayari kushirikiana na wadau wengine kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema Kampuni ya Oryx imekuwa ikiweka jitihada kubwa kuhamasisha matumizi nihati safi ya kupikia kwa Mama lishe na baba lishe nchini, hivyo ameona kuna umuhimu mkubwa wa kutoa ushirikiano.