Profesa Kitila achefukwa taasisi zinazojigeuza polisi kuvizia wawekezaji

Arusha. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema baadhi ya taasisi zimegeuka kuwa polisi na kuwavizia wafanyabiashara na wawekezaji badala ya kuwasaidia kufanya biashara zao kwa uhuru.

Aidha, amewataka wasomi na wafanyabiashara nchini kuchangamkia fursa za kazi na biashara nje ya nchi, ambapo licha ya kuwepo kwa fursa nyingi, wengi hawazichangamkii.

Profesa Mkumbo ameyasema hayo leo Alhamisi, Julai 4, 2024, jijini Arusha, wakati akizindua ofisi ya Kituo cha Pamoja cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Kanda ya Kaskazini kilichopo mkoani Arusha na uzinduzi wa awamu ya pili ya kampeni ya uhamasishaji uwekezaji wa ndani.

Amesema mamlaka hizo zitaunganishwa na kufanya kazi kidijitali kwenye kituo hicho ili kumrahisishia mwekezaji kulipa tozo mara moja na kupata leseni moja badala ya kuwa na utitiri wa leseni kama ilivyo sasa.

Uzinduzi wa kituo hicho ni kufuatia ombi la Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda alilolitoa Aprili 30, 2024, jijini hapa katika kongamano la uwekezaji kwenye sekta ya utalii.

Amesema serikali inaweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, ila kumekuwa na baadhi ya watumishi, ikiwemo taasisi za urekebu, ambazo kazi zao ni kuhakikisha watu wanafanya kazi katika mazingira mazuri na kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa ubora unaotakiwa.

“Kama ni Shirika la Viwango Tanzania (TBS) jukumu lake la msingi ni kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa Tanzania zina kiwango kizuri kisichohatarisha afya ya watu na ziweze kukidhi vigezo vya kitaifa na kimataifa,” amesema.

“Lakini wenzetu hawa wamebadilika kuwa mapolisi badala ya kumsaidia mfanyabiashara afikie viwango vinavyotakiwa. Yeye kazi yake imekuwa kuwa inspekta anakuvizia hamna nembo, aaah nimekupata sasa, badala ya kuwawezesha,” amesema.

“Matokeo yake zimekuwa ni TRA nyingine, yaani taasisi ya kukusanya mapato. Wako busy tunataka tuone mwaka huu hizi TBS, OSHA na nini. Tuweke mfumo ambao mfanyabiashara atalipa tozo mara moja, tufanya mabadiliko eneo hilo,” alieleza.

Amesema miongoni mwa masuala ambayo serikali inataka kuboresha mazingira yake ya uwekezaji ni pamoja na kuhakikisha mazingira ya kisiasa yanakuwa salama hivyo kuvutia wawekezaji waje nchini.

Waziri huyo amewataka wafanyabiashara na wawekezaji kutumia changamoto zinazojitokeza katika nchi za jirani kama fursa kwao kiuchumi.

“Nitoe wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania hapa duniani changamoto huwa zinaandaa fursa, kwa hiyo zinapotokea changamoto sehemu zingine na nyie mchangamkie na iwe fursa kwenu na fursa huwa zinadakwa,” amesema.

Profesa Mkumbo amesema miongoni mwa vipaumbele vya serikali ni pamoja na kuhakikisha kilimo kinakua kwa tija na kuwa kwa sasa utoshelevu wa chakula nchini ni asilimia 124 na kuwa ikitokea njaa serikali ina uwezo wa kulisha Watanzania kwa miezi sita.

Nyingine ni bidhaa zinazotumika kila siku kuzalishwa hapa nchini huku akitolea mfano uzalishaji wa mahindi na mpunga.

Amesema Serikali inachoangalia hivi sasa kwenye kuongeza nguvu ya uzalishaji ni upande wa sukari.

Amesema bado Tanzania inazalisha tani 460,000 kwa mwaka huku mahitaji yakiwa tani 650,000, hivyo amesema kuna haja ya kuongeza nguvu.

“Tunataka katika mwaka 2025/26 tuzalishe sukari ya kutosha ili kelele za kuagiza sukari au tusizalishe ziishe. Kingine tunaangalia mauzo ya bidhaa nje ya nchi, tunataka tuongeze mauzo hayo ili kukuza pato letu,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amewataka watendaji wa serikali katika mamlaka mbalimbali kutowafanya wawekezaji maadui na badala yake kuwawezesha katika kufanya biashara.

“Hatutegemei mambo ya njoo kesho, keshokutwa, nimetuma taarifa zako makao makuu. Tunaamini kituo hiki kitakuwa kituo cha pamoja, hatutarajii watuletee watu ambao nao hawana majibu zaidi ya kupokea business card,” alisema na kuongeza:

“Tunataka watu wenye maamuzi ambao watawasaidia wawekezaji kufanya shughuli zao kwa haraka, tusiwafanye wawekezaji awe wa ndani au wa nje kama maadui, tuwawezeshe tusiwavuruge wawekezaji,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri, alisema uwepo wa kituo hicho mkoani Arusha kitasaidia wawekezaji kufungua miradi yao kwa haraka na kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo na utalii hasa vyumba vya wageni kulala.

Amesema katika kipindi cha mwezi Januari hadi Desemba mwaka jana jumla ya miradi 526 ilisajiliwa ambayo iligharimu Dola za Kimarekani bilioni 5.7 huku ikichangia ajira zaidi ya 137,000.

Related Posts