Rais Biden agoma kujitoa uchaguzi Novemba, aangukia pua kura za maoni

RAIS wa Marekani, Joe Biden amekataa kujitoa kwenye uchaguzi wa Novemba, wakati kukiwa na shinikizo kumtaka ajitoe kwenye kinyang’anyiro hicho baada ya kushindwa kwenye mdahalo wake na Donald Trump wiki iliyopita. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).

Msemaji wake, Karine Jean-Pierre, amekanusha kuwa Biden alimuambia mmoja wa washirika wake wa karibu kwamba uwezekano wa yeye kuchaguliwa tena upo hatarini, endapo atashindwa kurejesha imani ya umma kwake baada ya matokeo mabaya ya mdahalo huo.

Biden amedai kuwa kushindwa kwake kwenye mdahalo huo kulitokana na kulemewa na majukumu na kuchoka sana katika siku za karibuni.

Baadhi ya magavana wa chama chake cha Democrat waliokutana hapo jana Jumatano na Biden, wamesema bado wana imani naye ingawa wamekiri kuwa mdahalo ulikuwa mbaya kwake.

Jana Jumatano Biden alipata chakula cha mchana kwa faragha na Makamu wa Rais, Kamala Harris katika Ikulu ya White House huku uvumi ukiongezeka iwapo angechukua nafasi yake kama mgombeaji wa chama katika uchaguzi wa Novemba.

Kamala Harris, Makamu wa Rais wa Marekani

Wawili hao walijiunga na kampeni ya Democratic ambapo Biden aliweka wazi kuwa atasalia kwenye kinyang’anyiro hicho na Harris akasisitiza kumuunga mkono. “Mimi ndiye mteule wa Chama cha Democratic. Hakuna mtu wa kuniondoa. Siondoki,” alisema.

Maswali yamekuwa yakiibuka iwapo mzee huyo mwenye umri wa miaka 81 ataendelea na kampeni yake kufuatia mjadala na Trump, ambao ulikuwa na ubabaikaji mkubwa, sauti dhaifu na baadhi ya majibu ambayo yalikuwa magumu kufuatilia. Hilo lilizua wasiwasi katika chama cha Democratic kuhusu uwezo wake kushinda uchaguzi huo.

Shinikizo la kumtaka Biden kujiuzulu limeongezeka siku chache tu kwa sababu kura nyingi zinaonyesha kuwa mpinzani wake wa chama cha Republican anazidi kupata umaarufu. Kura ya maoni ya New York Times iliyofanywa baada ya mjadala huo, ambayo ilichapishwa Jumatano, ilionyesha kuwa Trump alikuwa akishikilia uongozi kwa mbali zaidi akiwa na alama sita.

Na kura ya maoni tofauti iliyochapishwa na mshirika wa BBC wa Marekani CBS News ilionyesha kuwa Trump ana pointi tatu mbele ya Biden katika majimbo muhimu. Kura hiyo pia ilionyesha kuwa rais huyo wa zamani alikuwa anaongoza kitaifa.

Related Posts